Habari za Punde

Vijana 40 wapatiwa mafunzo ya Utalii

Na Mwashungi Tahir             Maelezo                   
Waziri wa Habari Utalii na Mambo ya Kale Mahmoud Thabit Kombo amewataka vijana kuhakikisha wanapata elimu itakayowawezesha kuajirika katika sekta ya Utalii.
Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Golden Tulip wakati akifunga mafunzo ya vijana ya kuongeza elimu ili waweze kupata nafasi za juu za ajira katika mahoteli ya kitalii ikiwa ni kilio cha vijana wengi wa Zanzibar kukosa ajira na kupewa wageni.
Amesema baada ya kufanya uchunguzi kwa vijana kuhusu masuala ya elimu imeonekana kuwa vijana wengi wanakosa nafasi za ajira kutokana na kiwango kidogo cha elimu.
“Tunataka vijana wazalendo wasome ili wapate kushika nafasi muhimu kwenye mahoteli yetu ili kuhakikisha hazichukuliwi na wageni,” alisema Waziri Kombo.
Alikumbusha kuwa moja ya lengo la kuanzishwa Vyuo vya  mafunzo ya utalii Zanzibar ni kuwafunza vijana taaluma hiyo ili waweze kushika nafasi za juu katika mahoteli mbali mbali.
Mkufunzi wa mafunzo ya utalii kutoka Chuo cha Zanzibar Center Excellence raia wa Malaysia Talal Attur Khan na mkewe Jasmine amesema wanakusudia kuanzisha chuo cha mafunzo ya utalii kwa vijana ili wapate kushika nafasi za uendeshaji wa hoteli.
Amesema mafunzo hayo yatalenga kuwajengea uwezo wa kujiamini katika utendaji wao wa kazi ndani ya mahoteli ili wageni waweze kuridhika.
Mmoja kati ya vijana waliopata mafunzo ya muda mfupi katika Hoteli ya Golden Tulip Ali  Khamis kutoka Kamisheni ya Utalii amesema amejifunza mambo mengi ikiwemo usuluhisho wa matatizo yanapotokea na uongozi wa juu.
Amesema hivi sasa yuko vizuri na atahakikisha elimu aliyoipata ataitumia vizuri na ataelimisha wenziwe ili waweze kufanya kazi zao kwa ufanisi zaidi.
Zaidi ya Vijana 40 wamepatiwa mafunzo hayo ya ya muda mfupi katika Hoteli ya Golden Tulip na yamewasaidia kutekeleza majukumu yao.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.