Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Ali Mohamed Shein (kulia) akizungumza na mgeni wake Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro Mhe. Azali Assoumani wakati alipofika Ikulu Mjini Zanzibar leo kwa ajili ya kusalimiana,
ZANZIBAR na Comoro zimeahidi kuendeleza uhusiano na
ushirikiano wa kidugu na kihistoria uliopo ambao una lengo la kuzidisha
mashirikiano katika sekta za maendeleo kwa manufaa ya pande mbili hizo.
Ahadi hiyo imetolewa
leo katika mazungumzo kati ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alipofanya mazungumzo na Rais wa Comoro Azali
Assoumani ambaye yupo Zanzibar kwa mapumziko.
Katika mazungumzo yao
viongozi hao kwa pamoja waliahidi kuendeleza uhusiano na ushirikiano wa
kihistoria baina ya pande mbili hizo
ambao umeimarika kwa muda mrefu na kuleta manufaa kwa nchi na wananchi wake
ambao wana udugu wa damu.
Viongozi hao walieleza
kuwa licha ya kuwa ni majirani lakini pia, ni ndugu wa damu hivyo, kuna haja ya
kuendeleza uhusiano na ushirikiano wao uliopo kwa manufaa ya nchi zao hasa
katika kuendeleza sekta za maendeleo kwa mashirikiano ya pamoja.
Akizungumza kwa upande
wake Rais Dk. Shein alimueleza Rais Azali Assoumani kuwa Zanzibar inathamini sana
uhusiano huo na ushirikiano uliopo sambamba na kuendeleza Mkataba wa Makubalino
uliosainiwa mwaka 2014 na pande mbili hizo kwa lengo la kukuza udugu uliopo.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa katika Mkataba huo wa Makubaliano masuala mbali mbali yalitiliwa nguvu
yakiwemo mashirikiano katika sekta ya afya, elimu, mila na utamaduni pamoja na masuala
mengineyo ambayo tayari yameshaanza kufanyiwa kazi na kuleta tija.
Alieleza kuwa mbali ya
uhusiano wa kimaendeleo kati ya pande mbili hizo pia, Zanzibar na Comoro zina
historia katika kukuza mila na tamaduni sambamba na mafunzo hasa katika elimu
ya dini ya Kiislamu ambapo historia inaonesha kwamba wananchi wa Comoro walio
wengi wamepata elimu ya dini ya Kiislamu hapa Zanzibar.
Akitolea mfano maelezo
hayo, Rais Dk. Shein alisema kuwa miongoni mwa Masheikhe wakuu wa Comoro akiwemo Marehemu Sheikh Mwinyi Baraka
walipata elimu yao ya dini hapa Zanzibar na hatimae kuwa balozi mzuri wa
kuitangaza Zanzibar katika uhai wake hadi kufariki kwake mwaka 1988.
Kutokana na umuhimu
huo Rais Dk. Shein alieleza hatua alizozichukua katika kuhakikisha katika ziara
yake aliyoifanya nchini humo mwaka huo wa 2014 alipata fursa ya kulizuru kaburi
la Sheikh Mwinyi Baraka ambaye alikuwa ni mwanachuoni mashuhuri.
Katika kuhakikisha
Mkataba wa Makubaliano hayo yaliosainiwa katika ziara ya Rais Dk. Shein nchini
Comoro mnamo mwezi Septemba mwaka 2014 yanafanyiwa kazi Chuo Kikuu cha Taifa
cha Zanzibar (SUZA) kilitiliana saini Mkataba wa Makubaliano juu ya
mashiriikiano na Chuo Kikuu cha Comoro mnamo Januari 19 mwaka 2016.
Aidha, katika
mazungumzo hayo, Rais Dk. Shein alieleza juhudi zinazoendelea kuchukuliwa
katika kuhakikisha Mkataba huo wa Makubaliano unatekelezwa vyema ikiwa ni
pamoja na kufundishwa kwa lugha ya Kiswahili nchini Comoro sambamba na kuwepo
kwa kubadilishana uzoefu na utaalamu kati ya Chuo Kikuu cha Comoro na Chuo
Kikuu cha (SUZA).
Rais Dk. Shein aliongeza
kuwa makubaliano hayo pia, yanaeleza jinsi Chuo Kikuu cha Comoro
kitakavyoshirikiana na (SUZA) katika kutoa mafunzo ya lugha ya Kifaransa.
Sambamba na hayo, Rais
Dk. Shein alimpongeza Rais Azali Assoumani kwa uwamuzi wake wa kuja kupumzika
Zanzibar, na kumueleza kuwa Zanzibar ni salama. “Karibu sana Zanzibar jisikie
uko nyumbani kwani Zanzibar ni sehemu salama ya kupumzika”,alisisitiza Dk.
Shein.
Nae Rais wa Muungano
wa Visiwa vya Comoro Azali Assoumani alimpongenza Rais Dk. Shein kwa
kumkaribisha vizuri Zanzibar jambo ambalo alisema huo ni utamaduni uliojengeka
kwa watu wa pande mbili hizo ukiwa ni urithi wa Waasisi wao.
Rais Assoumani
alimueleza Rais Dk. Shein kuwa Comoro na Zanzibar zina mambo mengi ya
kushirikiana licha ya yale yaliotiwa saini ambayo tayari yameshaanza
kutekelezwa na kuanza kuleta manufaa.
Alieleza kuwa wananchi
wa Comoro wanafarajika na uhusiano na ushirikiano mwema uliopo kati yao na
ndugu zao wa Zanzibar hasa ikizingatiwa kwamba wapo Wakomoro waliozaliwa
Zanzibar wananchi Comoro na wale waliozaliwa Comoro ambao wanaishi Zanzibar.
Rais Assoumani
alieleza kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwemo Zanzibar ina mambo mengi
ya kushirikiana hasa ikizingatiwa ukaribu na udugu uliopo baina ya pande mbili
hizo na kueleza kuwa kuchaguliwa kwa Rais John Pombe Magufuli kuwa Mwenyekiti
mpya wa (SADC) kutazidi kujenga mustakbali mwema wa nchi mbili hizo.
“Sisi ni ndugu wa damu
hivyo, kuna haja ya kufanya kazi kwa pamoja”,alisema Rais Assoumani na
kusisitiza kuyafanyia kazi yale yote yaliotiwa saini katika Mkataba wa
Makubaliano kati ya Zanzibar na Comoro mnamo mwaka 2014.
Katika maelezo yake,
Rais Azali Assoumani alimuhakikishia Rais Dk. Shein kuwa nchi yake pamoja na
wananchi anaowaongoza wataendelea kuthamini udugu wa kihistoria uliopo na
kuzidisha uhusiano na ushirikiano wao.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment