Habari za Punde

Elimu Inahitajika Kulitokomeza Suala la Udhalilishaji

Na Masanja Mabula ,PEMBA 
JUMLA ya kesi kumi na moja za wanafunzi kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji katika skuli ya Konde msingi  Wilaya ya Micheweni zimeripotiwa kwa kipindi cha kuanzia mwezi agosti hadi oktoba mwaka huu.
Matukio hayo pia yamo yanayodaiwa kufanywa na baadhi ya walimu ambapo mmoja wa walimu anayetuhumiwa tayari anaendelea kusota rumande baada ya kufikishwa mahakamani.
Matukio hayo wanayofanyiwa wanafunzi wa skuli ya msingi yameshtua Mkuu wa Wilaya ya Micheweni Salama Mbarouk Khatib , ambaye amekutana na waalimu , kamati ya skuli pamoja na wajumbe wa kamati ya maadili wilaya ili kutafuta ufumbuzi wa tatizo.
“ Hili ni janga la kitaifa , hivyo kunahitajika nguvu ya pamoja ili kuweza kulitokomeza ,kila mmoja anatakiwa  kumchunga mtoto wake na wa wenzake” alisema .
Katika hatua nyengine Mkuu huyo wa Wilaya ameligiza jeshi la Polisi wilayani humo, kuwafuatilia na kuwachukulia hatua wananchi ambao wanashindwa kufika kwenye vyombo vya sheria kutoa ushahidi dhidi ya watuhumiwa wa matendo ya udhalilishaji ikiwa ni pamoja na kuwaweka mahabusu.
Alisema uwepo wa baadhi ya wananchi wanaoshindwa kwenda kutoa ushahidi wanarudisha nyuma harakati za serikali za kuyatokomeza matendo ya udhalilishaji.
“Kuanzia leo naliagiza Jeshi la Polisi (OCD) kuhakikisha wanawakamata na kuwaweka mahabusu wale wote wanshindwa kufika kutoa ushahidi, hawa wanachangia kuendelea kutokea matando haya”alisisitia.
 Naye katibu wa chama cha walimu Zanzibar Mussa Omar alisema chama hakitakuwa tayari kumtetea mwalimu ambaye atakiuka maadili ya uwalimu na kujihusisha na matendo  ya udhalilishaji.
“Chama Cha walimu –ZATU-kinaungana mkono juhudi za Mkuu wa Wilaya , na kwamba na sisi chama hatutakuwa tayari kumtetea mwalimu mwenye tabia hiyo”alisema.
Msaidizi wa Afisa Ustawi wa Jamii Wilaya hiyo Asha Omar Abeid  aliwataka wananchi kwa kila mmoja na kwa mujibu wa nafasi aliyonayo, kuhakikisha anachukua hatua za kuwaelimisha watoto  ili watambue madhara ya kufanyiwa matendo hayo wakiwa bado wanafunzi.
“Mwalimu achukuwe nafasi yake, Afisa Ustawii naye awajibike kwa mujibu wa majukumu yake na mzazi naye anatakiwa kuzungumza na watoto bila ya kuficha, hii itasaidia kuwalinda watoto wetu”alisisitiza.
Walimu wa ushauri nasaha katika skuli hiyo walisema idadi inaweza kubwa kutokana na baadhi ya jamii kushindwa kutoa ushirikiano.
“Hivi juzi kuna mtuhumiwa ambaye tayari taarifa zake tumezifikisha kituo cha Polisi, lakini wametokea baadhi ya wananchi wamemkimbiza, tunaelekea wapi wazazi?” alihoji mmoja wa walimu.
Tayari mmoja wa walimu katika Skuli ya Konde Sekondari ambaye pia ni mwalimu wa Madrasa ya Quran amefikishwa mahakama ya Mkoa wa Kaskazini Pemba akidaiwa kuhusika na matendo hayo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.