Habari za Punde

Mkutano na Msemaji Mkuu wa Serikali na Waandishi wa Habari leo.


Mkurugenzi wa Idara ya Habari-MAELEZO na Msemaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi, akikaribisha swali kutoka  kwa Mwandishi wa Habari (hayupo pichani), wakati wa Mkutano wake na Waandishi wa Habari kuhusu utekelezaji wa kazi mbalimbali za Serikali, ulifanyika leo Oktoba 3, 2019 Jijini Dar es Salaam.
(Picha na Idara ya Habari-MAELEZO) 

Na: Mwandishi Wetu – MAELEZO, Dodoma
Tanzania yapiga hatua katika usambaji wa huduma za upatikanaji wa maji safi na salama mijini toka asilimia 45 mwaka 2015 hadi 95 mwaka huu na asilimia 46 mwaka 2015 hadi asilimia 65 mwaka huu kwa vijijini.

Hayo yamebainishwa na Mkrugenzi wa Idara ya Habari –MAELEZO na MSEMAJI Mkuu wa Serikali, Dkt. Hassan Abbasi wakati akizungumza na Waandishi wa Habari leo Jijini Dar es Salaam kati mkutano wake wa kawaida wa kila mwezi kuelezea utekelezaji wa miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali.

Kwa uwekezaji huu, wastani wa jumla wa upatikanaji wa maji vijijini umepanda kutoka chini ya asilimia 46 mwaka 2015 hadi asilimia 65 mwaka huu huku kwa upande wa mijini, mwaka 2015 Serikali iliweka lengo la kufikisha maji kwa asilimia 95 kwa wakazi wa mijini kutoka wastani wa asilimia 67;

Katika hatua nyingine Dkt. Abbasi alitumia mkutano huo kuwaondoa hofu wakulima wa zao la Korosho akisema kuwa kumeanza kuibuka wasiwasi katika jamii na baadhi ya watu kuanza kuwatisha wakulima kuwa msimu mpya wa korosho unakuja, watakosa maghala ya kuhifadhi korosho zao.

“Niwahakikishie wakulima kuwa hadi kufikia Septemba 30, 2019, Serikali imeshauza korosho zote kwa jumla ya wanunuzi 21 wa ndani na nje ya nchi. Kuna tani zaidi ya 4,595.90 zitabanguliwa nchini na zaidi ya tani 211, 587 ambapo tani 107,187 zitapitia Bandari ya Dar na tani 104,400 kupitia Bandari ya Mtwara zitasafirishwa kwenda nje ya Tanzania,” alisisitiza Dkt. Abbasi.

Alifafanua kuwa hadi sasa zaidi ya tani 98,860 zimekwishachukuliwa na kusafirishwa nje ya nchi kupitia Bandari za Mtwara na Dar sawa na asilimia 41 ya korosho zote na zoezi la kuondoa korosho iliyobaki kupelekwa kwa wanunuzi linatarajiwa kukamilika ifikapo Oktoba 21 mwaka huu.

“Naomba kusisitiza tena, faida kubwa ya mchakato huu ni kwa wakulima kupata bei ya haki katika zao la korosho lakini funzo la korosho si tu limeweka mazingira mazuri zaidi katika misimu ijayo ambapo korosho itanunuliwa kwa mfumo madhubuti lakini pia mazao mengine yamepata nguvu ya kuwekewa mifumo na hivyo wakulima kupata bei inayowanufaisha kwa kuwapa faida.”Alisema Dkt. Abbasi.

Msemaji Mkuu wa Serikali amekuwa na utamaduni wa kuzungumza na wananchi kila mwanzoni mwa mwezi kupitia vyomba vya habari kwa lengo la kuhabarisha umma juu ya hatua mbalimbali za utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Pombe Magufuli ili wananchi taarifa sahihi za namna Serikali yao inavyowajali katika kuwaletea maendeleo.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.