Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akiwahutubia Wananchi na Wafanyakazi wa Shirika la Meli Zanzibar, wakati wa hafla ya Uzinduzi wa Meli Mpya ya Kisasa ya Mafuta MT.Ukombozi II, uliofanyika katika bandari ya Malindi.
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali
Mohamed Shein, amelitaka Shirika la Meli Zanzibar kuwa na mipango madhubuti ya
mafunzo kwa watendaji na waongozaji wa vyombo vya baharini, ili kuweza
kufanyakazi zao kwa weledi.
Dk. Shein amesema hayo katika sherehe za uzinduzi wa Meli mpya
ya Mafuta ya MT. Ukombozi ll, zilizofanyika Bandarini Malindi, mjini hapa.
Alisema wafanyakazi wanaoendesha vyombo baharini wana jukumu
kubwa katika utekelezaji wa kazi zao, hivyo ni vyema kwa Shirika hilo likawa na
mipango madhubuti katika upatikani wa mafunzo
ya muda mrefu, kati na muda mfupi ili waweze kutekeleza kazi zao kwa ufanisi.
Aliutaka uongozi huo kutotosheka na utaalamu walionao
watendaji wake, hivyo akataka ratiba maalum za mafunzo ziandaliwe, sambamba na
kuwapa mishahara na stahiki zote zinazoendana na ukubwa wa kazi wanazofanya.
“Hawa wanafanya kazi
nzito sana, sio rahisi kuranda na meli baharini kila siku, nasisistiza
upatikanaji wa taaluma katika kuendesha vyombo hivi”, alisema.
Aidha, aliutaka uongozi huo kuhakikisha watendaji hao wanajuwa
kanuni na sheria za nchi pamoja na zile za kimataifa, ili waweze kutekeleza
vyema kazi zao.
Dk. Shein alitumia fursa hiyo kusisitiza umuhimu wa
wafanyakazi wa meli hiyo kufanyakazi kwa misingi ya uwajibikaji, uadilifu na nidhamu, kwa kigezo kuwa hatua
hiyo itawajengea heshima.
“Lazima tuzingatie nidhamu ya kazi zetu, mfanye kazi kwa
kuzingatia imani, nidhamu na uwajibikaji kikamilifu”, alisema.
Vile vile, Dk. Shein aliwataka watendaji wa meli hiyo
kuendeleza ushirikiano uliopo kati yao, sambamba na kusisitiza umuhimu wa kuwepo
uangalifu na umakini ili uwepo usalama
wa wafanyakazi na mali za serikali.
Aidha, alisifia ubora wa meli hiyo kwa kuwa katika viwango vya
kimataifa, kama ilivyo kwa meli ya MV, Mapinduzi ll.
Dk. Shein aliwatanabahisha wananchi akiwataka kuwa wazalendo
kwa kuwa na utamaduni wa kuvipenda na
kuvitukuza vilivyo vyao, badfala ya kuviponda.
“Hii ni meli yetu sote watu wa Zanzibar……imenunuliwa na
Serikali yetu kwa manufaa yetu”, alisema.
Alieleza kuwa ujio wa meli hiyo unatarajiwa kuondoa kabisa
tatizo la upungufu wa mafuta linalojitokea mara kwa mara nchini, akibainisha
kuwa hivi sasa Serikali italazimika kuhoji pale nishati hiyo itakapoadimika.
Aidha, alisema uaptikanaji wa meli hiyo ni kichocheo katika
uharakishaji wa ujenzi wa Bandari mpya ya Mpigaduri,
Katika hatua nyengine, Dk. Shein alisema uamuzi wa Serikali wa
kujenga Bandari ya Mpigaduri upo pale pale, ukitarajiwa kuanza mishoni mwa
mwaka huu au mapema mwakani.
Alisema serikali tayari imefanikisha maandalizi ya ujenzi wa
Bandari mpya kwa ajili ya Mafuta na Gesi katika eneo la Mangapwani, kwa kuweka
miundombinu, ikiwemo uwekaji wa umema, ujenzi wa barabara pamoja na nyumba kwa ajili
ya wakaazi wa Dundua.
Aidha, alisema Serikali imefanikisha ununuzi wa meli za MV
Mapinduzi 11, MT Ukombozi 11 ambapo kwa ujumla zimegharimu zaidi ya shilingi
Bilioni 136 , pamoja na mambo mbali ya maendeleo, kutokana na kuimarika kwa uchumi
wake, hatua inayotokana na ukusanyajii mzuri wa mpato.
Mapema, Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji, Sira
Ubwa Mamboya alisema ujenzi wa meli hiyo ni utekelezaji wa Ilani ya CCM ya
2015-2020, na kubainisha kuwa kwa kiasi kikubwa serikali imekamilisha ahadi
zake.
Alisema Wizara hiyo inalenga kuaanda utaratibu maalum kwa Wazanzibari
wote wenye nia ya kuiona meli hiyo
kupata fursa hiyo, sambamba na kuahidi kuitunzwa ili iweze kuleta tija kwa
Taifa.
Nae, Waziri wa Fedha na Mipango, ambae pia ni Mwenyekiti wa
Kamati ya Ujenzi wa Meli hiyo, Balozi Mohamed Ramia, alisema meli hiyo ni bora
na kubainisha kuwa thamani yake inaendana na hali halisi ya mahitaji, hivyo kuwa
kichocheo katika uingizaji wa mapato na kukuza uchumi wa Taifa.
Aidha, akitowa salam
mjenzi wa meli hiyo kutoka Kampuni ya DAMEN ya nchini Uholanzi Ronald Maat,
alisema meli hiyo imeundwa kwa kufuata viwango vya kimataifa na kuzingatia
usalama baharini.
Alitowa pongezi kwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa uamuzi
wake wa kujenga meli hiyo na kubainisha azma ya Kampuni kuiunga mkono Serikali kwa
juhudi zake za kuifanya kuwa na vyombo vya uhakika vya usafiri baharini, hususan katika usafirishaji wa mafuta.
Mapema, Katibu Mkuu Wizara ya ujenzi, Mawasiliano na
Usafirishaji, Mustafa Aboud Jumbe alisema ujenzi wa meli hiyo iliyotengenzwa na
Kampuni ya DAMEN kutoka Uholanzi, umegharimu shilingi Bilioni 36 hadi
kukamilika kwake.
Alisema ujenzi huo umegharamiwa na serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar na kubainisha kuwa fedha zote zimeshalipwa katika Kampuni husika.
Alisema meli hiyo yenye urefu wa mita 86.21 ina uwezo wa kubeba
tani 3,500 za mafuta ya aina nne, ikiwemo mafuta taa, Dizeli, Petroli na mafuta
ndege.
Katika hafla hiyo,pamoja na mambo
mengine kulifanyika tukio la makabidhiano ya meli hiyo baina ya mjenzi kutoka
Kampuni ya DAMEN na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024
2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment