Habari za Punde

Ufunguzi wa Kongamano la Umoja wa Wanawake Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi akizungumza na Viongozi na Wanachma wa UWT katika kilele cha maadhimisho ya Wili ya Umojawa Wanawake Tanzania Mkoa Kaskazini Unguja.
Na.Kassim Salum Abdi.OMPR.
Viongozi na wanachama wa Umoja wa wanawake Tanzania {UWT} Mkoa Kaskazini wametakiwa kubadilika kwa kufanya maamuzi sahihi ya kuwachagua viongozi wenye uwezo wa kuwatumikia na kukijenga chama ili kwenda sambamba na hadhi ya chama chenyewe.
Uamuzi  huo wa kuwachagua vingozi bora na wenye uwezo utakisaidia chama cha mapinduzi kuendelea kushika Dola kutokana na kushinda kwa kishindo kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alieleza hayo wakati akilifungua kongamano maalum la umoja wa wanawake Tanzania Mkoa wa kaskazini lililofanyika katika Tawi la Mchenza Shauri kuadhimisha wiki ya umoja wa wanawake ambayo hufanyika kila ifikapo tarehe 26 Septemba hadi tarehe 04 Oktoba.
Mama Asha alisema kupatikana kwa kiongozi bora kunatokana na uwamuzi wa wanachama wenyewe kupitia demokrasia ya chama kwa kuwapa fursa ya kuwachagua viongozi wanaowataka na alisema kiongozi mzuri ana uwezo wa kuwaunganisha wanachama na kuwaletea maendeleo wanayoyahitaji.
Aliwataka akina Mama hao wa Mkoa wa Kaskazini kutumia muda wao kwa kuyatangaza yale yote mazuri yaliotekelezwa na serikali ya chama mapinduzi kupitia viongozi wake  Dk. John Pombe Magufuli na  Dk. Shein wakiwa watekelezaji wakuu wa ilani ya uchaguzi waliyoinadi kupitia kampeni zao za Mwaka 2015.
Mama Asha alieleza kwamba kuelekea kwenye uchaguzi mkuu ipo haja kwa wanachama kudumisha utaratibu wa  kujenga utamaduni wa kupendana, kuheshimiana na kudumisha mshikamano miongoni mwao sambamba na kuachana na tabia ya majungu kuyayoenezana sumu kwa kupeana sifa mbaya.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa wanawake Tanzania Bibi Tunu Kondo alisema lengo la kuadhimisha wiki ya umoja wa wanawake ni kuwakumbuka wazazi, wanachama na waasisi waliotangulia mbele ya haki ambao wametoa mchango mkubwa katika taifa hili.
Bibi Tunu Kondo alisema  kuna kila sababu ya kuwakumbuka waasisi hao kwa vile walijitoa muhanga na kupigania uhuru wa kweli hasa wanawake kwa kupata fursa mbali mbali ikiwemo fursa ya kupiga kura , kushiriki katika vyombo vya maamuzi na kujitokeza hadharani kujinadi mambo ambayo hapo awali hakukuwa na fursa kama hiyo.
Mapema Makamu Mwenyekiti wa Umoja wa Wanawake Tanzania  Bibi Thwaiba Edington Kisasi aliwapongeza wanawake wa Mkoa wa kaskazini kwa kuongoza katika kuibeba dhana ya kufanya makongamano kufuatia ngazi ya Taifa kutekeleza suala hilo katika mikoa tofauti ya Nchini Tanzania.
Alisema kutokana na kujipanga kwao vizuri ana imani kubwa ya kufanya vizuri kwa kukisaidia chama  caha Mapinduzi kuendelea kupata ushindi mnono kwenye uchaguzi ujao wa Mwaka 2020 na kuendelea kuifanya kaskazini kuwa ngome ya chama hicho.
Katika Kongamamano hilo mada tano ziliwasilishwa ikiwemo umuhimu wa daftari la kudumu la wapiga kura, kupinga vitendo vya udhalilishaji, umuhimu wa Jumuiya ndani ya chama, lishe bora na mada ya kuhamasisha magauni manne.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.