Habari za Punde

Katibu Mkuu wa CCM Taifa Dkt. Ally Bashiru Awasili Zanzibar kwa Ziara ya Siku Kumi

KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Bashiru Ally Kakurwa, akivishwa shada la maua na Vijana Maalum baada ya kuwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume wa Zanzibar kwa ajili ya ziara ya kikazi na  kuimarisha Chama ya Siku Tisa Zanzibar.NA IS-HAKA OMAR,ZANZIBAR.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Dkt. Bashiru Ally Kakurwa amewasili Zanzibar kwa ziara ya kikazi ya kuimarisha Chama.  
Ziara hiyo itakayoanza Novemba 26 hadi Disemba 4 mwaka huu kwa upande wa Unguja na Pemba ambapo atashiriki shughuli mbali mbali za kichama kwa kuzungumza na Viongozi wa ngazi mbali mbali sambamba na kuzindua miradi ya maendeleo.
Akizungumza mara baada ya kuwasili nchini hapo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mzee Abeid Amani Karume, alishukru kwa mapokezi makubwa yaliyofanywa na Viongozi na Wanachama wa CCM.
 Katika maelezo yake Dkt.Bashiru mara baada ya kukutana na wenyeji wake, alisema ushindi wa CCM katika uchaguzi wa serikali za mitaa uliopatikana kwa upande wa Tanzania bara ni kielelezo tosha cha ushindi wa mwaka 2020.
Alisema ushindi huo wa asilimia 99 umepatikana kutokana na kukubalika kwa Chama Cha Mapinduzi kwa wananchi wanaonufaika na utekelezaji wa Ilani ya CCM Mijini na Vijijini.
Aidha, Dkt.Bashiru akizungumzia ziara yake alifafanua kuwa lengo la ziara hiyo ni kushauriana na Wana CCM masuala mbali mbali yatakayosaidia kuendelea kuimarisha CCM.
“Nitaanza ziara yangu Unguja kasha kumalizia Pemba, nitakutana na Wanachama mbali mbali nizungumze nao kuhusu masuala ya kuendelea kukijenga Chama chetu kwani tupo kwa ajili ya kuwatumikia wananchi.”,alisema Dkt.Bashiru.
Dr Bashiru ataanza ziara zake leo (jana) kwa kukutana na kuzungumza na Makamu Mwenyekiti wa CCM Zanzibar DK. Ali Mohamed Shein ambaye pia ni Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi.
Naye Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao, aliwasihi Wanachama, Viongozi na makada wa Chama hicho kujitokeza kwa wingi katika maeneo mbali mbali ambayo Dkt.Bashiru atafanya ziara zake.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Bashiru Ally Kakurwa, akizungumza na Viongozi na Watendaji mbali mbali wa Chama Cha Mapinduzi walioshiriki katika Mapokezi mara baada ya kuwasili Zanzibar kwa ajili ya ziara ya Siku Tisa, inayotajia kuanza Novemba 26 hadi Disemba 4 Mwaka huu.
KATIBU Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Dkt.Bashiru Ally Kakurwa,akisalimiana na Wanachama wa CCM pamoja na Vijana mbali mbali walioshiriki katika mapokezi yake mara baada ya kuwasili Zanzibar kwa ajili ya ziara ya Siku Tisa inayotajia kuanza Novemba 26 hadi Disemba 4 Mwaka huu.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.