WAZEE wa
CCM Wilaya ya Dimani Kichama wameeleza kuridhishwa na uongozi wa Rais wa
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein ambaye
pia, ni Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na kukiri kwamba anawatendea haki.
Wazee hao wa CCM, Wilaya ya Dimani Kichama waliyasema hayo
leo huko katika ukumbi wa Afisi ya CCM
Mkoa wa Mjini iliyopo Amani, Mkoa wa
Mjini Magharibi katika Mkutano aliouandaa Rais Dk. Shein ambaye pia ni Makamo
Mwenyekiti wa CCM Zanzibar kwa ajili ya wazee hao ikiwa ni muendelezo wa
mikutano hiyo iliyoanza jana hapa Unguja ambapo tayari kwa upande wa kisiwani
Pemba imeshafanyika.
Katika hotuba yao wazee hao walikiri kuwa Rais Dk. Shein katika
kipindi chake cha uongozi wa Awamu ya Saba amekuwa akiwatendelea haki katika
kuleta maendeleo huku akiwa anasimamia vyema utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi
ya CCM ya mwaka 2015-2020 sambamba na kustawisha huduma za jamii.
Walieleza kuwa katika Wilaya yao wamefaidika kwa mambo
makubwa mno kama vile huduma za elimu bure ambapo tayri katika Wilaya yao wana
skuli 6 za Ghorofa za Sekondari hivi sasa, huduma za miundombinu ambapo tayari
kero za barabara ya Kibondemzungu na Mwanakwerekwe zimeshatatuka na hivi sasa
zinapitika.
Aidha, walieleza kuwa barabara ya Kiembesamaki kuelekea
Uwanja wa Ndege ambayo ilikuwa na tatizo la kutuwama maji wakati wa mvua tatizo
ambalo limeshaondoka baada ya kutengenezwa mtaro mkubwa wa maji wa kisasa.
Waliongeza kuwa huduma za afya, maji safi na salama, umeme
pamoja na huduma nyengine za kijamii zinapatikana bila ya wasi wasi katika
Wilaya yao.
Wazee hao walitoa shukurani na pongezi kwa Rais Dk. Shein
kwa kuendelea kuwajali mno ikiwa ni
pamoja na kuwahudumia wao pamoja na wananchi wote kwa ujumla na kuamua kwa
makusudi kuwatunza wazee kwa kuwapatia Pencheni Jamii.
Pamoja na hayo, wazee hao walimpongeza Rais Dk. Shein kwa kuamua
kufanya jambo hilo kubwa tena bila ya kuangalia itikadi ya kisiasa jambo ambalo
limewaonesha upendo wake wa dhati kwa wananchi anaowaongoza na kueleza kuwa
katika Wilaya yao, wastani wa wazee 1,663 wanalipwa kwa kila mwezi.
Katika hotuba yao hiyo wazee hao wa Wilaya ya Dimani
walieleza kuwa kwa kufuata Ibara ya 5 kifungu cha (1) cha Katiba ya CCM
inaeleza malengo na madhumuni ya chama hicho ni kushinda katika chaguzi zote.
Walieleza kuwa ushindi huo ni kwa ajili ya kushinda katika
Uchaguzi wa Serikali Kuu na Serikali za Mitaa Tanzania Bara na Zanzibar ili kuunda na kushika Serikali Kuu na Serikali
za Mitaa katika Jamhuri ya Muungano wa Tanzania upande mmoja na Zanzibar upande
wa Pili.
Hivyo, wazee hao walieleza mikakati waliyoiweka katika
kuhakikisha chama chao cha CCM kinaendelea kushika hatamu na kuwaletea
maendeleo wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Nae Makamo Mwenyekiti wa CCM Zanzibar na Rais wa Zanzibar
na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein alisema kuwa wazee
ni vyema wakasikilizwa kwani wana mambo mengi ambayo yatasaidia katika
kukiimarisha chama hicho na hatimae kuendelea kupata ushindi katika chaguzi
zake zote.
Alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imewaweka
wazee katika programu zake zote za maendeleo ukiwemo Mkakati wa Kukuza Uchumi na
Kupunguza Umasikini (MKUZA) na mipango mengineyo ya kiuchumi kwa lengo la
kuendelea kuwatunza.
Alisisitiza kuwa CCM ina kila sababu ya kuwatunza na
kuwaenzi wazee na kuwataka viongozi wa chama hicho kuwa karibu na wazee na kuchukua
maoni yao pale wanapoyahitaji.
Alisema kuwa ni vyema viongozi wa Chama hicho ukawatumia
wazee katika shughuli zao za kichama hasa ikizingatiwa kwamba Chama hicho kina
mtandao mkubwa wa uongozi.
Rais Dk. Shein alisema kuwa wazee wanayajua mambo mengi na
wana historia kubwa ya kabla na baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 hivyo,
ni vyema wakathaminiwa kwani Mapinduzi ndiyo yaliyomkomboa mnyonge.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuna kila
sababu ya kuulinda, kuuenzi na kuutunza Muungano wa Tanganyika na Zanzibar hasa
ikizingatiwa kwamba Zanzibar inafaidika kwa kiasi kikubwa na Muungano huo.
Pamoja na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa kuwepo kwa
wazee imara na uongozi madhubuti wa CCM ndio utakaopelekea ushindi wa chama
hicho.
Makamo Mwenyekiti huyo wa CCM Zanzibar alieleza haja kwa
wazee kuwaeleza vijana jinsi ya kuwaheshimu na kuwathamini wazee kwani wazee
ndio kila kitu.
Rais Dk. Shein alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi ya
Zanzibar inathamini na inazijali juhudi walizozichukua wazee hadi kupatikana kwa
uhuru wa Tanganyika na Zanzibar.
Katika hotuba yake aliyoitoa mbele ya wazee hao wa CCM
pamoja na viongozi wengine wakuu wa chama hicho Rais Dk. Shein alieleza kuvutiwa
na taarifa yao waliyoisoma ambayo imeonesha jinsi wazee wa Wilaya hiyo
walivyoweka mikakati ya kukiimarisha chama chao ili kiendelee kupata ushindi wa
kishindo.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi
alitoa pongezi kwa Rais Dk. Shein kwa azma yake ya kukutana na wazee na
kuupongeza utamaduni wake wa kukutana na wanachama wa ngazi za chini wa chama
hicho wakiwemo wazee.
Alieleza kuwa CCM imeanza muda mrefu kuwathamini wazee
kwani Baraza la Wazee ndio ngome madhubuti ya chama hicho kwani Baraza la asili
la Wazee wa Ofisi Kuu ya CCM Kisiwandui ambalo limeundwa siku ya pili baada ya
kuundwa chama cha ASP.
Alisema kuwa katika miaka tisa ya uongozi wake mambo mengi
ameyafanya Rais Dk. Shein kutokana na hikma na uzalendo wake mkubwa wa kuendesha
Serikali na Chama hali ambayo imeleta maendeleo makubwa sambamba na amani na
utulivu nchini.
Nae Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Dimani Hussein Ali Mgema
Kimti alieleza kuwa mafanikio makubwa yamepatikana katika Awamu ya Saba
inayoongozwa na Rais Dk. Shein na kusisitiza kuwa mashirikiano makubwa
yamepatikana kati ya viongozi wote wa Chama, Serikali pamoja na wananchama wa
chama hicho.
Alieleza kuwa hatua hiyo inatokana na miongozo, maelekezo
na uongozi mzuri wa Makamo Mwenyekiti wao, Rais Dk. Shein jinsi anavyowaongoza.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment