Habari za Punde

Mitandao Chanzo cha Kuwaingiza Watoto Wengi Katika Mukono ya Udhalilishaji

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akiufungua Mkutano wa Kikanda na Kimataifa kwa Nchi zinazotoa huduma Maalum za Simu kwa Watoto na kufanyika katika Hoteli ya Verde Mtoni pembezoni mwa Mji wa Zanzibar kwa niaba ya Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Kukosekana kwa Sheria madhubuti katika udhibiti wa mambo na vitendo vichafu vinavyoonyeshwa na kufanywa kupitia Mitandaoni, kunachochea Watu wasioweza kudhibiti nafsi zao kufanya vitendo vya udhalilishaji popote na kwa yeyote bila ya kuzingatia Ubinaadamu.
Tafiti mbali mbali zilizofanywa kutokana na ukubwa wa tatizo la udhalilishaji imebainika kwamba miaka ya hivi karibuni, mitandao imekuwa chanzo cha kuwaingiza Watoto wengi katika mikono ya wadhalilishaji mbali mbali ndani na nje ya Nchi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein alitoa kauli hiyo katika Hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi katika Mkutano wa Kikanda na Kimataifa kwa Nchi zinazotoa huduma Maalum za Simu kwa Watoto na kufanyika katika Hoteli ya Verde Mtoni pembezoni mwa Mji wa Zanzibar.
Dr. Shein alisema Madhalimu, Wahalifu na Makatili hao wamekuwa wakiitumia Mitandao kwa kuwashawishi baadhi ya Watoto na hatimae kuwafanyia vitendo vya udhalilishaji na unyanyasaji uliopindukia mpaka ambao kamwe haukubaliki katika Jamii.
Alisema ni jambo la kusikitisha kuona kwamba Sheria zilizopo katika udhibiti wa Mitandao zinaonekana kuwa dhaifu, na wakati mwengine zimegubikwa na changamoto nyingi katika utekelezaji wake kutokana na Nchi kutofautiana kwa mitazamo ya itikadi za Kisiasa na utashi wa maslahi tofauti ya Kijamii na Uchumi.
Rais wa Zanzibar aliwaeleza Washiriki wa Mkutano huo kwamba Watoto wengi  hivi sasa wamezunguukwa na vishawishi vingi vinavyoweza kuwaingiza katika wimbi la udhalilishwaji na unyanyaswaji wa Kijinsia.
Alieleza inatia huruma kuona baadhi ya Watoto ambao kwa umri na walivyo bado hawajajifahamu, wanadhalilishana wenyewe kwa wenyewe kwa kuiga yale wanayoyaona Mitandaoni. Hivyo kwa mnasaba huo Jamii itaendelea kushuhudia mmong’onyoko wa Maadili kutokana na matumizi mabaya ya Mitandao.
Dr. Shein alisema tafiti mbali mbali zilizofanywa katika ngazi ya Kitaifa, Kikanda na Kimataifa zimeonyesha kwamba changamoto ya udhalilishaji na unyanyasaji wa Watoto bado inaendelea kuwa kubwa na sugu.
Alisema taarifa zilizotolewa na Shirika la Afya Duniani {WHO} zimeeleza kwamba Watoto wapatao Bilioni Moja wenye umri kati ya Miaka Miwili na Kumi na Saba walikumbwa na aina tofauti za udhalilishaji na unyanyasaji ndani ya Mwaka 2018.
Alisema kwa upande wa Mataifa ya Bara la Afrika, Nchi zilizopo Kusini mwa Jangwa la Sahara hazitoi taswira ya kuridhisha  katika suala hilo jambo ambalo Waafrika wenyewe wanapaswa kutafakari katika kupata njia ya kuyatafutia dawa  matatizo yanazotokana na vitendo vya udhalilishaji ndani ya Nchi hizo.
“ Si vyema kuanza kutaja hali ya kila Nchi katika Mkutano huu wa Kikanda na Kimataifa, ila sote tunapaswa kutafakari, ili tuone umuhimu wa kuyaandaa na kuyapatia maazimio yatakayotuonyesha njia ya kupata ufumbuzi”. Alisisitiza Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar alitanabahisha kwamba hali iliyopo hivi sasa inaonyesha umuhimu wa kuwa na Mipango ya pamoja iliyoambatana na Sera na Sheria madhubuti zitakazoongoza kwenye mapambano dhidi ya Vitendo hivyo viovu na matumizi mabaya ya Mitandao.
“ Ni lazima Nchi zote za Bara la Afrika tuwe na Mikakati ya pamoja, ili tuweze kuondokana na changamoto zote hizo”. Alifahamisha  Rais wa Zanzibar Dr. Ali Mohamed Shein.
Alishauri uwepo wa Muungano katika kutoa Elimu juu ya namna bora ya kutoa Taarifa ya vitendo vya udhalilishaji  kupitia uhamasishaji wa matumizi bora ya Teknolojia ya Kisasa ya Habari na Mawasiliano kwa kuimarisha Maendeleo.
Dr. Shein alipendekeza njia sahihi ya kupiga vita udhalilishaji  unaofanywa kupitia Mitandaoni, ni kutumia njia hiyo hiyo katika kupambana na Watu hao katika mfumo wa kuwadhibiti ndani ya Mitandao yenyewe.
Alitahadharisha kwamba ni lazima kwa vyombo vya kutunga Sheria  pamoja na vile vya Ulinzi na Usalama viwe mstari wa mbele  na kuendelea kuwa madhubuti na imara katika matumizi ya Teknolojia ya Habari.
Dr. Shein alisema ni wajibu wa Mashirika na Taasisi zinazotoa huduma za Mitandao ya Simu kuongeza ubunifu kwa kutafuta njia nyengine mbadala na ya kisasa zitakazowawezesha Watoto na makundi mbali mbali ndani ya Jamii kutoa Taarifa ya vitendo vya udhalilishaji kwa urahisi na haraka zaidi.
Alifahamisha kwamba Taasisi na Mashirika hayo yasisubiri kutafutwa kwa kupigiwa simu maofisini mwao na kupokea Taarifa za udhalilishaji bali ziwe na utaratibu utakaotumika katika kufuatilia na kuzipata Taarifa hizo.
Alisema katika kumthamini Mtoto, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imeweka kipaumbele  suala la kuimarisha Haki  na Ustawi wa Mtoto kwa kupanga na kutekeleza Mikakati mbali mbali ya Kisera na Kisheria.
Dr. Shein aliweka wazi kwamba Mipango Mikuu ya Maendeleo ya Kitaifa imeeleza bayana juu ya namna Serikali ilivyojizatiti katika kupambana na vitendo vya udhalilishaji na kusimamia haki za Watoto katika ngazi ya Kitaifa na Kimataifa.
Alisema upo mfano hai wa Sheria iliyotungwa na Serikali ya Mtoto nambari  6 ya Mwaka 2011 ambayo tayari imeshinda Tuzo iliyotolewa na Shirika la World Future Council kwa kuwa miongoni mwa Sheria bora  inayozingatia maslahi na ustawi wa  Watoto kwa upana zaidi.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alizipongeza Taasisi na Mashirika Binafsi kwa kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika utoaji wa huduma hizo za simu maalum za kuwasaidia na kuwalinda Watoto dhidi ya udhalilishaji.
“ Wito wangu ni kuwa sote kwa pamoja tuendelee kupaza sauti zetu na kuziunganisha Jamii zetu ili tuwe na msimamo mmoja katika kuvitokomeza vitendo hivyo”. Alisisitiza Dr. Ali Mohamed Shein.
Alisema juhudi zilizofanywa na Mashirika na Taasisi hizo zimesaidia sana katika kutoa  mwamko na elimu juu ya mapambano dhidi ya vitendo vya udhalilishaji na kushajiisha  makundi mbali mbali kushiriki katika kuondosha kabisa  ukatili huo.
Akitoa salamu za shirika C – Sema lililoratibu Mkutano huo wa Kikanda na Kimataifa Mtendaji Mkuu wa Taasisi hiyo Balozi Nyasagara  Kadege  alisema Utamaduni wa Wananchi wa Zanzibar  umekuwa kigezo cha kufuata Maadili sahihi ya ulezi wa Watoto.
Balozi Nyasagara alisema uwepo wa Mkutano huo wa Kikanda na Kimataifa iliyojumuisha Washiriki kutoka Mataifa 35 ya Afrika Mashariki, Kati, Magharibi, Kaskazini, Mashariki ya Kati na Taasisi na Mashirika ya Kimataifa ni muhimu kwa vile unaweza kusaidia mbinu za upatikanaji wa ulinzi wa Watoto.
Nao Wawakilishi wa Mashirika na Taasisi za Kikanda na zile za Kimataifa walitanabahisha kwamba jukumu la kuwasimamia Watoto kujiepusha na ajira wakiwa bado wadogo bado liko mikononi mwa Wazazi, Walezi pamoja na Viongozi kwa msaada wa Taasisi za Kijamii.
Walisema ajira za Watoto zimebainika kuwa njia nyepesi inayotoa ushawishi kwa Watoto wengi kujiingiza katika vitendo vya kudhalilishwa kwa tamaa ya kipato kinachotolewa kama mtego kwao bila ya kuelewa athari yake.
Walieleza kwamba yapo matukio mengi yaliyoripotiwa yakiwahusisha wadhalilishaji kutumia uwezo na nafasi zao kama maeneo ya Mipakani, mila na Imani potovu kuendeleza vitendo hivyo viovu.
Akimkaribisha Mgeni Rasmi kuufungua Mkutano huo Naibu Waziri wa Kazi, Uwezeshaji Waze Wanawake na Watoto Mheshimiwa Shadya Mohamed alisema ushiriki wa Taasisi tofauti za Kitaifa na Kimataifa kwenye mapambano dhidi ya kumlinda Mtoto na matukio ya udhalilishaji utaleta  matumaini kwa kundi kubwa la Watoto.
Mh. Shadya alisema huduma za Simu Maalum kwa Watoto hapa Zanzibar zimeanzishwa mnamo Tarehe 15 Juni Mwaka 2015 na tayari ymepatikana mafanikio makubwa baada ya kupokelewa kwa Simu 5,159 ambazo kati ya hizo simu 159 ndizo rasmi na kuchukuliwa hatua za kisheria zilizohusisha matukio ya kutelekezwa kwa Watoto, udhalilishaji na unyanyasaji wa Kijinsia.
Ujumbe wa Mwaka huu unaeleza “ unyanyasaji na udhalilishaji wa Watoto Kingono Mtandaoni: Ni wito kwa Afrika kuweka nguvu katika kuzuia na kupambana na vitendo hivyo Mtandaoni.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.