Habari za Punde

Wanawake Wabunifu Wajasiriamali Kukuza Fikra Zao Ili Kusarifu Bidhaa

Na.AKassima Salum Abdi
Umoja wa wanawake Tanzania kupitia chama cha Mapinduzi umetakiwa kuendeleza utaratibu wa kutoa mafunzo kwa akina Mama wajasiriamali waliojikusanya katika vikundi mbali mbali ili  wawe na nguvu zaidi za kuwawezesha kujitegemea.
Kufanya hivyo kutawawezesha wanawake wajasirimali kuwa wabunifu, kukuza fikra zao pamoja na kusarifu bidhaa zao kwa ufanisi zaidi ili ziweze kupandishwa thamani wakati zitapoingia sokoni.
Mke wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mama Asha Suleiman Iddi alieleza hayo katika warsha ya wajasiriamali wanawake kutoka mikoa miwili ya Pemba katika Ukumbi wa Kiwanda cha Mafuta cha Makonyo Wawi Kisiwani Pemba.
Alieleza kuwa, Kazi ya ujasiriamali katika kuitekeleza kwake inahitaji elimu na taaluma ambayo itawawezesha wanawake hao kuweza kupanga na kuweka hesabu zao kwa uweledi jamba ambalo litapelekea wizara yenye dhamana na wanawake, vijana na watoto waweze kukopesheka.
Mke huyo wa Makamu wa Pili wa Rais aliwataka wanawake hao wajasiriamali kubadilika kulingana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia kwa kutumia muda wao mwingi na nafasi zao katika suala zima la kujifunza na kubadilishana uzoefu ili waweze kuimarisha bidhaa na huduma zao kwa jamii inayowazunguka.
Akizungumzia fursa zilizopo Mama Asha alisema kwa sasa wajasirimali wana fursa nyingi zitakazowasaidia kujikwamua kiuchumi endapo watazitumia vizuri akizitaja fursa hizokuwa ni pamoja na benki, taasisi mbali mbali za serikali na zisizo za kiserikali zinazowawezesha wajasiriamali wanawake kupata mikopo nafuu, ruzuku pamoja na pembejeo.
Kuhusu tatizo la udhalilishaji Mama Asha aliwaeleza wanawake hao kutoka mikoa miwili ya Pemba kuwa wakiwa kama wazazi hawana budi kutafakari namna bora ya kukomesha tatizo hilo ndani ya jamii inayowazunguka kwa kushirikiana pamoja
Alisema kwamba serikali ya mapinduzi Zanzibar inaendelea kuunda sheria, taratibu na mikakati mbali mbali pamoja na kuanzishwa madawati kwa lengo la kupiga vita tatizo la udhalilishaji.
Mama Asha Suleiman Iddi amewataka wanawake hao wajasiriamali kuepuka aibu pamoja na muhali kwa kutowaonea haya wale wote wanaowadhalilisha wanawake na watoto kwa kuwafikisha katika vyombo vya sheria ili waweze kuchukuliwa hatua.
Akisoma Taarifa Mwenyekiti wa kamati ya malezi, mafunzo na elimu Bibi Mwaka Abdulrahman alisema akina mama hao wameamua kufanya warsha hiyo kwa lengo la kuwapatia mafunzo wanawake hao wajasiriamali ili kuzifanya bidhaa wanazozalisha ziwe na ubora na kupata soko la urahisi.
Bibi Mwaka alisema kufanyika kwa mafunzo hayo kiswani Pemba ni muendelezo wa mafunzo hayo kwa wajasirimali kwani wamekwishafanya mafunzo kama hayo kwa wajasiria mali wanawake kwa upande wa Unguja.
Nae Naibu Katibu Mkuu wa umoja wa wanawake Tanzania (UWT) Bibi Tunu Kondo alisema wakati umefika sasa kwa wanawake kujikomboa kutokana na umaskini kwa vile chama cha mapinduzi tayari kimekuja na falsafa ya uchumi na kujitegemea kwa wanachama na wananchi wake. Hivyo wataendeleza jitihada za kuwapatia mafunzo na elimu wanawake wajasiriamali.
Pamoja na mambo mengine Naibu Katibu huyo aliwaomba wanawake hao wajasirimali kutoisahau ibara ya tano ya chama cha mapinduzi ya kukipatia ushindi chama, hivyo amewaomba kujitokeza kwa wingi kwenda kujiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura muda utakapofika.
Mapema Mama Asha alipata fursa ya kutembelea mabanda ya maonesho ya wajasirimali wanawake kutoka mikoa miwili ya Pemba na kujionea bidhaa wanazozidhalisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.