Waziri wa Katiba na
Sheria, Balozi Augustine Mahiga akiongea katika kongamano la kutathimini na
kutafakari jitihada zilizofanywa na Serikali ya awamu ya tano katika kuwakomboa
watanzania kwenye haki za kiuchumi, kijamii na kiutamaduni lililofanyika jijini
Arusha.
Waziri wa Katiba na
Sheria, Balozi Augustine Mahiga akiwa katika picha ya pamoja na viongozi
mbalimbali wa Serikali, taasisi za umma na binafsi pamoja taasisi za kimataifa.
Na Mbaraka Kambona,
Waziri wa Katiba na
Sheria, Balozi Augustine Mahiga amesema kuwa ili serikali iweze kutimiza haki
za msingi za binadamu kwa wananchi wake kikamilifu inahitaji nguvu ya kifedha
ili kujenga uchumi imara utakaoweza kutimiza haki hizo.
Balozi Mahiga alitoa
kauli hiyo kwenye kongamano la kitaifa la kutathimini hali ya haki za kiuchumi,
kijamii na kiutamaduni lililofanyika jijini Arusha Desemba 13-14, 2019.
Mahiga alisema katika
kongamano hilo kuwa ili serikali iweze
kutekeleza na kutimiza haki za
binadamu ni lazima ijenge mfumo wa uwajibikaji na uwazi ambao utajenga uchumi
imara utakaosaidia kutekeleza haki za msingi za binadamu na utawala bora.
Mahiga alisema kuwa kwa
kutambua hilo serikali ya awamu ya tano iliamua kwa dhati kabisa kuimarisha
mfumo wa ukusanyaji kodi kwa kuziba mianya yote iliyokuwa inapoteza mapato ili
kupata fedha za kutosha kutoa huduma kwa
jamii.
“Serikali ya awamu ya
tano imeleta sio tu mageuzi bali imeleta mapinduzi, kuna vitu ambavyo
vilihitaji ujasiri wa pekee kuvitekeleza, huwezi kujenga uchumi kama huna
fedha, bila kodi huwezi”,alisema Mahiga
“Kutimiza haki za
binadamu kunahitaji mtaji, lazima ujenge mfumo wa serikali bora, serikali
ambayo inajenga uchumi wake kupitia mapato yake ya ndani kama serikali ya awamu
hii inavyofanya”,aliongeza
Mahiga aliendelea
kusema kuwa serikali imepambana na mianya ya kuvuja kwa mapato na ndio maana
leo tunashuhudia haki za kijamii, kiutamaduni na kiuchumi zinatekelezwa kwa vitendo.
Alisema serikali
imeendelea kuwapa watu wake fursa mbalimbali za kiuchumi ili kuboresha hali za maisha yao
kwa mtu mmoja mmoja hata vikundi.
Mahiga alisema serikali
itaendelea kutekeleza mpango wa taifa wa miaka mitano (2016, 17-2020/21) ambao
umelenga kujenga uchumi wa viwanda ili kuchochea mageuzi ya uchumi na maendeleo
ya watu.
Alisema kuwa uamuzi wa
serikali wa kujenga uchumi wa viwanda unalenga kuleta maendeleo jumuishi na
endelevu kwa kutumia ipasavyo rasilimali zilizopo na hivyo kuchangia katika
kukuza pato la taifa na kutoa nafasi nyingi na endelevu za ajira.
Aidha, alisema kuwa katika
kutimiza haki ya elimu, serikali imechukua hatua kadhaa ikiwemo utekelezaji wa
sera yake ya elimu ya msingi na sekondari bila malipo. Sera hii imesaidia kuongeza
idadi ya wanafunzi wanaoandikishwa kutoka milioni 1.57 mwaka 2015 hadi milioni
2.08 mwaka 2016 sawa na ongezeko la asilimia 35.2.
Kuhusu haki ya afya, Mahiga
alisema serikali imeendelea kuimarisha vituo vya afya, imeongeza bajeti ya dawa
kutoka bilioni 31 mwaka 2015/16 kufikia bilioni 270 mwaka 2018/19. Ongezeko
hilo limeongeza upatikanaji wa dawa muhimu kufikia asilimia 96 kwa mwaka 2018/19. Tiba za
kibingwa zinatolewa katika hospitali ya taifa ya Muhimbili, hospitali mpya za
rufaa za Benjamini Mkapa na Mloganzila. Hospitali hizo zinatoa huduma za
kibingwa zikiwemo upasuaji wa moyo, ubongo na uti wa mgongo ambazo awali
zilikuwa zinapatikana nje ya nchi .
Awali , Mwenyekiti wa
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB), Jaji Mstaafu Mathew Mwaimu alisema
kuwa lengo la kongamano hilo ni kutathimini na kutafakari jitihada zilizofanywa
na Serikali ya awamu ya tano katika kuwakomboa watanzania kwenye haki za
kiuchumi,kijamii na kiutamaduni.
No comments:
Post a Comment