Habari za Punde

Serikali Kutokuwavumilia Wanaotumia Vibaya Fani ya Ununuzi wa Ugavi.

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Shaaban, akizungumza wakati akifunga Kongamano la Kumi la Waatalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), ambapo  amewataka wataalamu hao kuzingatia miiko na maadili ya fani ya Ununuzi na Ugavi kama sheria inavyosema, Jijini Dodoma.

Na: Peter Haule na Josephine Majura – WFM Dodoma
Serikali imesema kuwa haitamvumilia mwanataaluma ya Ununuzi na Ugavi atakayesababisha upotevu  wa rasilimali za nchi kwa kutozingatia kanuni na sheria.

Hayo yamesemwa Jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Amina Shaaban, alipokuwa akifunga Kongamano la 10 la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB) zaidi ya 600 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Bi. Amina Shaaban alisema kuwa fani ya Ununuzi na Ugavi ni adhimu na inalojukumu kubwa katika kuhakikisha Tanzania inakuwa na uchumi wa kati uliojikita katika Viwanda ambapo fani hiyo ni muhimu upatikanaji wa bidhaa na huduma.

“Yeyote atakayepata nafasi ya kiutendaji, anapaswa kuzingatia miiko na maadili ya fani ya ununuzi na ugavi kama anavyoongozwa na sheria katika kusukuma juhudi za maendeleo. Atakaye kwamisha juhudi za Serikali katika kukuza uchumi wa viwanda na kutoa huduma bora kwa wananchi asifumbiwe macho wala kuhurumiwa”, alisema Bi. Amina Shaaban.

Alisema kuwa anafurahishwa na hatua ya Bodi ya PSPTB ya kuwajengea uwezo Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi ili waweze kushiriki kikamilifu katika hatua mbalimbali za kukuza uchumi wa viwanda.

Amewataka wataalamu wote waliohudhuria katika Kongamano hilo, kutekeleza maazimio yote waliyokubaliana nayo  na  kufanya tathimini ya kiutendaji.

Kwa upande wake Kamishna wa Idara ya Sera ya Ununuzi wa Umma, Dkt. Fredrick Mwakimbinga alisema kuwa washiriki wamejadili mada mbalimbali na kuelekezana kuhusu umuhimu wa fani hiyo katika kukuza uchumi wa viwanda na pia wamekumbushwa kufanya kazi kwa kuzingatia maadili, weledi, uzalendo na kufuata sheria.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.