RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein,
akimsikiliza Mkurugenzi wa Idara ya Kilimo cha Umwagiliaji Maji Ndg. Haji Hamad
Salum, akitowa maelezo ya Ujenzi wa Mradi wa Miundombinu ya Kilimo cha
Umwagiliaji wa Maji (kulia kwa Mkurugenzi) Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
Mhe.Balozi Seif Ali Iddi,wakiwa katika eneo la ujenzi wa Mradi huo katika Kijiji cha Kinyasini Kisongoni Wilaya
ya Kaskazini “A” Unguja, (kushoto kwa Rais) Waziri wa Kilimo Maliasili Mifugo
na Uvuvi.Mhe.Mmanga Mjengo Mjawiri na Naibu Waziri wa Kilimo Maliasili Mifugo
na Uvuvi Mhe.Dkt. Makame Ali Ussi. Wakiwa katika eneo la ujenzi huo
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.
Ali Mohamed Shein amesisitiza kuwa ardhi iliyotengwa kwa ajili ya kilimo hapa Zanzibar ni vyema ikatumika kwa ajili ya
shughuli hiyo na si vyenginevyo.
Rais Dk. Shein
aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika uwekaji wa jiwe la
msingi la ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji huko Kinyasini Kisongoni,
Wilaya ya Kaskazini B, Mkoa wa Kaskazini Unguja.
Alieleza kuwa kilimo
ni ardhi, hivyo endapo ardhi haitokuwepo kilimo hakitofanyika kwani hata
historia ya Zanzibar inaonesha wafanyakazi na wakulima walishindwa kulima kabla
ya Mapinduzi kutokana na kunyanganywa ardhi yao.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa hapa Zanzibar hivi sasa ardhi imekuwa ndogo sana kutokana na matumizi
mabaya ya ardhi yanayofanywa na baadhi ya wananchi.
Akieleza historia ya
ardhi, Rais Dk. Shein alisema kuwa miaka mingi kabla ya Mapinduzi matukufu ya
Januari 12, 1964 Wazanzibari waliteseka katika kutafuta ardhi na pale
walipotaka kulima ilibidi wakapige magoti kwa wakoloni.
Alisema kuwa madhila
ya kunyanyaswa katika ardhi yao yaliondoshwa na Mapinduzi yaliyomg’oa Sultani
mnamo Januari 12, 1964 ambapo ni miaka 56 tokea kutokea Mapinduzi hayo.
Alisema kuwa uhuru wa
Zanzibar unahisabika rasmi kuanzia Januari 12, 1964 na kupelekea sekta zote
ikiwemo ardhi kuwa huru na tarehe 8 Machi 1964 hayati mzee Karume alitoa
tangazo rasmi la SMZ ikiwa ni amri na sheria ya Serikali ambayo ilitengenezwa
utaratibu wa sheria na katiba juu ya sekta hizo ikiwemo ardhi.
Rais Dk. Shein
aliyanukuu maneno ya Hayati mzee Karume aliyoyasema kwamba “shamba lolote
lililokuwa asili yake ni serikali halafu serikali ile ya kifisadi imelichukua
shamba hili na imemuuzia jamaa yake kwa njia ya hadaa shamba hili litarudi
serikalini, ardhi yote ya Unguja na Pemba ni mali ya serikali na kila mtu wa
Unguja na Pemba ana haki ya kuitumia..”
Rais Dk. Shein alisema
kuwa mashamba 745 yalihodhiwa na watu wachache kabla ya Mapinduzi ambapo kuna
mmoja alikuwa na mashamba 300 pekee yake na mtu wa chini alikuwa na mashamba
matatu ambapo waliuziana kwa matabaka na hakukuwa na Mwafrika aliyekuwa na
shamba.
Wananchi wa Zanzibar
hawakuwa na shamba la kulima na badala
yake aliyekuwa akitaka kulima alitakiwa kujiunga na chama cha Hizbu hali ambayo
Chama Cha ASP kilipelekea kununua shamba la Kilombero ambalo lilinunuliwa chini
ya uongozi wa Marehemu Mzee Karume.
Alieleza kuwa mnamo
tarehe 11 Novemba 1964 Marehemu Mzee Karume aligawa heka tatu tatu kwa wananchi
ambapo walitakiwa walime katika maisha yao yote na sio wajenge au wakate
viwanja.
Alieleza azma ya
Serikali ya Awamu ya Saba ya kuongeza idadi ya matrekta ili wananchi wapate
kulima kwa ufanisi zaidi na kuweza kuwasaidia wakulima wa mpunga hasa akina
mama ambao wamekuwa wakifanya kazi kubwa katika kilimo hicho.
Aliongeza kuwa
Serikali imekuwa ikiongeza mazingira mazuri zaidi hasa katika kilimo cha mpunga
ili kulima kwa faida ambapo pia, juhudi zimechukuliwa katika kuhakikisha
kiwanda cha matreka kinafufuliwa.
Alisema kuwa Serikali
imetayarisha Sera ya Kilimo pamoja na Mpango Mkuu wa Kilimo ambavyo ndio vitu
vikubwa ambavyo vimepelekea kubuniwa miradi mbali mbali kama huo uliozinduliwa
hivi leo.
Rais Dk. Shein alisema
kuwa Serikali ya Awamu ya Saba imekuwa ikiwafidia wakulima kwa asilimia 75 ya
gharama zote na asilimia 25 zinabaki kwa wananchi kwenye pembejeo kama vile
matreka, mbolea, mbegu bora na dawa za kuulia magugu.
Aidha, Rais Dk. Shein aliwashajiisha
wananchi wa Zanzibar kutumia mchele wa Zanzibar ambao ni mzuri na una sifa
zote.
Pia, Rais Dk. Shein
alieleza kuwa kilimo ni maji hivyo, lazima maji yawepo ili kuweza kulima kilimo
cha kisasa cha umwagiliaji maji ambacho ni cha uhakika na ndio maana Serikali
ikaanzisha miradi hiyo.
Sambamba na hayo,
alieleza hatua za Serikali zilizochukuliwa katika kuimarisha sekta ya kilimo
ikiwa ni pamoja na kuanzisha Taasisi ya Utafiti ya Kilimo Zanzibar kwa lengo la
kuuendeleza utafiti wa mazao mbali mbali hapa nchini.
Alieleza hatua
zinazochukuliwa katika kukiimarisha Chuo cha Kilimo cha Kizimbani ikiwa ni
pamoja na kukiunganisha na Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA).
Pia, alieleza hatua
zitakazochukuliwa katika kuondosha matumizi ya majembe ya mikono na badala yake
alieleza hatua zitakazochukuliwa katika kuhakikisha matrekta yanaongezeka.
Alisema kuwa mradi huo
umechelewa kutokana na urasimu uliokuwepo ndani ya Wizara hiyo lakini hatimae
imewezekana na kuanza vyema.
“Nayasema haya
wananchi wajue kwamba tumejichelewesha wenyewe kutokana na
urasimu......tumechelewa kuanza lakini hatimae tumeanza vizuri sana na kwa
umakini mkubwa”, alisema Dk. Shein.
Aidha, Rais Dk. Shein
aliitaka Wizara ya Kilimo kuongeza kasi kwenye kazi zao na kundoa mivutano
miongoni mwao na wawe wamoja na pale wanapopewa maelekezo na Serikali
wayafanyie kazi na wasishindane kwani ushindani hauna tija.
Alisema kuwa mambo
hayo hayampi matumaini na badala yake yanamtia hofu kwani lengo lake ni kuhakikisha
asilimia 80 ya chakula kinapatikana hapa nchini kutokana na mikakati ya
Serikali kinyume na hivi sasa ambapo kinapatikana kwa asilimia 40.
Alieleza kuwa Mradi
huo ni vyema ukaenda vizuri na baada ya miezi 24 uweze kufanya kazi na kuleta
tija kwa wananchi wa Zanzibar huku akisisitiza umuhimu wa kushauriana.
Nae Waziri wa Kilimo ,
Maliasili, Mifugo na Uvuvi Mmanga Mjengo Mjawiri alisema kuwa azma ya Wizara hiyo
ni kuhakikisha kuwa kilimo kinacholimwa hapa nchini kinakuwa na tija kubwa huku
akieleza agizo la Serikali katika sekta ya kilimo.
Alisema kuwa katika
kutekeleza Ilani ya uchaguzi ya CCM Wizara hiyo imepiga hatua kubwa juhudi
ambazo zinatokana na ushauri mzuri wa Rais Dk. Shein.
Alisema kuwa Wizara
hiyo itaendelea kuwatumia wataalamu hao katika sekta ya kilimo hasa katika
kilimo cha mpunga huku akisisitiza hatua zitakazochukuliwa ili wakulima walime
kwa faida na thamani.
Nae Naibu Mwakilishi
Mkuu wa Benki ya Exim ya Korea Bwana Kang Sang Jin alieleza jinsi ya umuhimu wa
mradi huo ambao utasaidia kwa kiasi kikubwa kukuza uchumi wa Zanzibar sambamba
na kuendeleza mashirikiano kati ya nchi hiyo na Zanzibar.
Alieleza mashirikiano
yaliopo kati ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo
pamoja na Mkandarasi wa Mradi ambaye anafanya kazi vizuri huku akieleza kuwa
mradi huo utaimarisha sekta ya kilimo na kuongeza uzalishaji chakula.
Nae Katibu Mkuu wa
Wizara ya Kilimo, Malisiali, Mifugo na Uvuvi katika risala yake alieleza kwamba
uwekeaji wa jiwe la Msinmgi wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji
unadhihirisha kuanza rasmi utekelezaji wa Mradi huo unaotekelezwa na Serikali
ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia mkopo kutoka Benki ya Exim-Korea.
Alisema kuwa mradi huo
utaendelezana kujenga miundombinu katika eneo la hekta 1,524 katika mabonde 7
ya umwagiliaji maji kwa Unguja na Pemba.
Akitaja mgawanyo wa
mradi huo aliyataja maeneo ya Cheju hekta 803, Kinyasini hekta 217, Kobokwa
hekta 194, Kilombero hekta 100, Chaani hekta 71, Makwararani hekta 78 na
Mlemele hekta 61.
Alisema kuwa mradi huo
pia, utajumuisha ujenzi wa miundombinu ya misingi ya umwagiliaji, mabwawa manne
makubwa ya kukinga na kuhifadhi maji ambapo moja kati ya hayo ni hilo la
Kinyasini, Chaani kwa upande wa Unguja na mabonde ya Mlemele na Makwararani.
Aliongeza kuwa mradi
huo utachimba visima 49 na kuweka pampu zake ambapo visima 33 vitachimbwa
katika bonde la Cheju, visima 33 Cheju, visima 10 Kibokwa na visima 6
vitachimbwa katika bonde la Kilombero.
Kwa upande wa gharama
za utekelezaji mradi huo, Katibu Mkuu huyo alisema kuwa jumla ya dola za
Kimarekani takriban milioni 64.304
ambapo kati ya fedha hizo dola milioni 50 ni mkopo kutoka Benki ya Exim-
Korea NA Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inachangia kiasi cha dola za Kimarekani
milioni 14.804.
Alisema kuwa mpaka sasa
tayari Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo kwa
kushirikiana na Wizara ya Fedha na Miango imeshaweza kulipa fidia kwa wananchi
takriban 327 yenye thamani ya jumla ya TZS Bilioni 1.145.
Aidha, alisema kuwa
mradi huo utaongeza uzalishaji wa mpunga katika maeneo ya umwagiliaji maji
kutoka tani 5,400 kwa mwaka 2018 na kukadiriwa kufikia tani 2,384 kwa mwaka
ifikapo mwaka 2021 ambapo ongezeko litafikia uzalishaji wastani wa tani 60,000
za mpunga na kugunguza kwa asilimia 70 ya uagiziaji wa mvheke ncje ya nchi.
Mapema Rais Dk. Shein
alipata maelezo kutoka kwa Mkurugenzi wa Idara ya Umwagiliaji Haji Hamid ambaye
alimueleza kwamba mkataba wa ujenzi wa mradi huo ulitiwa saini tarehe
06.12.2018 baina ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Wizara ya Kilimo,
Maliasi, Mifugo na Uvuvi na Kampuni ya ujenzi ya KOLON-HANSONL kutoka Jamhuri
ya Watu wa Korea.
Pia, alieleza kuwa
Kampuni ya KRC-DASAN JV ambayo inatoka Korea ndio Mshauri Mwelekezi wa Mradi huo
wa umwagiliaji maji ambao ni mkubwa kabisa kuwahi kutekelezwa hapa Zanzibar
huku akitumia fursa hiyo kumueleza uendelezaji wake.
Viongozi wa Jimbo la
Kiwengwa kwa niaba ya wananchi wa Jimbo hilo nao kwa upande wao walitoa pongezi
kwa Rais Dk. Shein kwa juhudi kubwa anazozichukua katika kuwapelekea miradi ya
maendeleo ikiwa ni pamoja na kutekeleza kwa vitendo Ilani ya Uchaguzi ya CCM
huku wakieleza mafanikio yatakayopatikana kutokana na mradi huo.
Rajab
Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail:
rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment