Habari za Punde

Hutuba ya Maadhimisho ya Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar 12-1-2020.Hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein. Katika Sherehe za Mapinduzi Kuadhimisha Miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar. Uwanja wa Amaan Jijini Zanzibar 12-1-2020.

Mabibi na Mabwana, Assalam Aleikum.
Tuna wajibu wa kumshukuru Mwenyezi Mungu, Muumba wa Mbingu na Ardhi na vyote vilivyomo ndani yake, kwa kutujaaliya afya njema na kutuwezesha kujumuika katika Uwanja huu wa Amaan, kwa ajili ya kuadhimisha kilele cha Sherehe za miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar, ya tarehe 12 Januari, 1964. Natoa shukurani zangu za dhati kwaviongozi wote wa Kitaifa wakiongozwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,kwa kuja kuungana nasi katika kilele cha Sherehe za Miaka 56 ya Mapinduzi yetu.Kadhalika, natoa shukurani kwa viongozi wengine wote wa Serikali ya Jamhuriya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar mliopo madarakani na mliostaafu, Waheshimiwa Mabalozi na Wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa, wageni wetu pamoja na Viongozi wa Dini na  Vyama vya Siasa kwa kuja kujumuika nasi katika sherehe hizi adhimu na muhimu. Kwenu nyote, nasema Ahsanteni sana.
Shukurani za pekee nazitoa kwenu, ndugu wananchi,kwa kuhudhuria kwa wingi katika Maadhimisho haya ya miaka 56 ya Mapinduzi, mkionesha  furaha kubwa mliyonayo; ambayo ni kielelezo cha kuzithamini sherehe hizi. Sote tuna wajibu wakutambua thamani ya maadhimisho ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964, kwa sababu Mapinduzi ndio yaliyoikata minyororo ya ubaguzi na aina zote za dhulma zilizokuwa zikiwakabili wafanyakazi na wakulima wa Zanzibar.  Kwa hivyo, Mapinduzi ndio yaliyoikomboa Zanzibar na watu wake na kuleta uhuru wa kweli kwa wananchi wote wa Zanzibar.  Ni ukweli uliowazi kwamba Mapinduzi ndio yaliyofungua ukurasa mpya wa maendeleo ya Zanzibar na watu wake na tutaendelea kuyasherehekea maadhimisho haya kwa furaha, vifijo na nderemo kila mwaka.


Ndugu Wananchi,
Kila tunaposherehekea maadhimisho ya Siku hii muhimu, inatupasa tuwakumbuke waasisi wa Mapinduzi, walioongozwa na Jamadari wetu, Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, pamoja na viongozi wenzake waliojitoa muhanga kwa ajili ya kuikomboa Zanzibar. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awalaze mahali pema Peponi waasisi wetu wa Mapinduzi waliokwishatangulia mbele ya haki. Vile vile, Mola awape afya njema na umri mrefu, waasisi wetu walio hai,ili tuendelee kunufaika na  hekima na busara zao, katika kuyadumisha malengo ya Mapinduzi yetu.
Ni dhahiri kwamba mafanikio tuliyoyapata katika sekta zote za maendeleo katika kipindi cha miaka 56 ya Mapinduzi, yametokana na kuendelea kuwepo sababu za msingi za kufanyika kwa Mapinduzi hayo kwa kuondoa ubaguzi na dhulma, kuendeleza umoja, mshikamano na usawa kwa watu wote; pamoja na  amani na utulivu. Kwa hivyo, ni jukumu letu sote tufahamu kwamba hakuna mbadala wa amani katika maendeleo ya mtu mmoja mmoja, jamii na taifa kwa jumla.
Ni wajibu wetu sote tuisimamie amani, na tuifuate misingi ya sheria, kwa sababu matukio ya uvunjaji wa amani huanza na vitendo vinavyopingana na sheria za nchi. Kwa hivyo, natoa wito kwenu ndugu wananchi, kila mmoja wetu azingatie umuhimu wa amani na usalama kuwa ni jambo la msingi na lazima.

Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, ya Awamu yaSaba, tangu iliopoingia madarakani tarehe 3 Novemba, mwaka 2010, imepata mafanikio ya kuridhisha. Tunafarajika na mafanikio tunayoyapata katika utekelezaji wa mipango yetu mikuu, ikiwemo MKUZA Awamu ya I, II na III, Ilani ya Uchaguzi Mkuu ya CCM ya2010 na 2015, Dira ya Maendeleo ya 2020 pamoja na Mipango ya Maendeleo ya Kimataifa.Mafanikio hayo yanatokana na jitihada mbali mbali za pamoja zinazofanywa na Serikali, Mashirika na Taasisi mbali mbali za Kitaifa na Kimataifa zinazotuunga mkono, utendaji mzuri wa viongozi wa ngazi zote, mamlaka mbali mbali, watumishi wa umma pamoja na ushirikiano wa kizalendo kutoka kwa wananchi. Kwenu nyote nasema, Ahsanteni sana.

Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Awamu ya Saba, katika kipindi cha miaka tisa, imeendelea na juhudi za kutekeleza mipango ya mageuzi ya kiuchumi, ili kuhakikisha kwamba uchumi na ustawi wa wananchi wa Zanzibar unaimarika. Juhudi hizo ni pamoja na kuiimarisha na kuiendeleza hali ya amani na utulivu  zilizopelekea kuongezeka kwa Pato Halisi la Taifa kwa mara 1.6 zaidi kutoka thamani ya TZS Bilioni 1,768 mwaka 2010, hadi kufikia thamani ya TZS Bilioni 2,874 mwaka 2018. Vile vile, kasi ya ukuaji wa uchumi imeongezeka kutoka asilimia 4.3 mwaka 2010 hadi kufikia asilimia 7.1 mwaka 2018. Kadhalika, Pato la Mwananchi nalo limeongezeka kutoka TZS 942,000, sawa na Dola za Kimarekani 675 mwaka 2010, hadi kufikia TZS 2,323,000, sawa na Dola za Kimarekani 1,026, mwaka 2018. Hilo ni ongezeko la asilimia 147 kwa thamani ya fedha za Tanzania.  Haya ni mafanikio makubwa tuliyoyapata.
Kadhalika, mfumko wa bei nao kasi yake imepungua  kutoka asilimia 14.7 mwaka 2011 hadi asilimia 3.9 mwaka 2018. Hatua hio imewawezesha wananchi kupata bidhaa muhimu kwa bei inayoridhisha.
Vile vile, kuimarika kwa uchumi kumepelekea ongezeko la ukusanyaji wa mapato mwaka hadi mwaka. Kwa mwaka wa fedha 2018/2019, mapato ya ndani yalifikia TZS Bilioni 748.9, ikilinganishwa na jumla ya TZS Bilioni 181.1 zilizokusanywa mwaka 2010/2011. Hili ni ongezeko la makusanyo la mara 4.1.  Utegemezi wa bajeti umepungua na umefikia wastani wa asilimia 5.7 mwaka 2018/2019, kutoka wastani wa asilimia 30.2 mwaka 2010/2011. Natoa pongezi kwa Bodi ya Mapato Zanzibar (ZRB) pamoja na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa kutekeleza vizuri majukumu yao kwa kipindi chote cha miaka tisa. Hongereni sana.
Jitihada za kuendeleza uwekezaji zimefanikiwa katika kipindi cha  miaka 9 ambapo Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA), imeweza kuwavutia wawekezaji katika miradi ya maendeleo kwa sekta mbali mbali.  Hadi kufikia mwaka 2018, jumla ya miradi ya uwekezaji 304 yenye mtaji waDola za Kimarekani Bilioni 3.74 imetekelezwa. Miradi hio imetengeneza ajira zipatazo 16,866.

Ndugu Wananchi,
Jitihada kubwa za kuimarisha sekta ya elimu zimefanywa na Serikali katika awamu mbali mbali, katika kipindi cha miaka 56 iliyopita, kwa madhumuni ya kuyatekeleza malengo ya Mapinduzi ya kutoa elimu bure bila ya ubaguzi kama ilivyotangazwa na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume, tarehe 23 Septemba, 1964. Katika kutekeleza uamuzi huo, Serikali imeongeza Bajeti ya Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali, mara 3.8, kutoka TZS Bilioni 47.093 mwaka 2010/2011 hadi TZS Bilioni 178.917 mwaka 2019/2020.

Ndugu Wananchi,
Ongezeko la idadi ya skuli, taasisi nyengine za elimu na wanafunzi katika ngazi zote, ni miongoni mwa mafanikio yaliyofikiwa katika Sekta ya Elimu. Hadi mwaka 2019, idadi ya Skuli za Maandalizi imefikia 382 zenye wanafunzi 85,974; ikilinganishwa na skuli 238, zilizokuwa na jumla ya wanafunzi 29,732 katika mwaka 2010. Skuli za msingi zimeongezeka na zimefikia skuli 381, zenye wanafunzi 290,510 mwaka 2019, kutoka skuli 299 zilizokuwa na jumla ya wanafunzi 226,812, mwaka 2010. Hadi kufikia mwishoni mwa mwaka 2019, zipo jumla la Skuli za Sekondari 284 zenye wanafunzi 130,713 ikilinganishwa na skuli 105 zilizokuwa na wanafunzi  80,008, mwaka 2010.Majengo kadhaa ya ghorofa ya skuli za Msingi na Sekondari yamejengwa, Unguja na Pemba.
Hivi sasa tunapoadhimisha miaka 56 ya Mapinduzi ya Zanzibar, elimu ya juu inatolewa katika  vyuo vikuu vitatu; Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA), Chuo Kikuu cha Zanzibar(ZU) na Chuo Kikuu cha Al-Sumeit. Vyuo hivi vina idadi ya wanafunzi 7,090, wanaosoma kuanzia ngazi ya Cheti hadi Shahada ya Uzamivu (PhD), ikilinganishwa na wanafunzi 3,572waliokuwepo katika mwaka 2010/2011. Katika kipindi cha miaka tisa (9) cha uongozi wa Awamu ya Saba, jumla ya wanafunzi 9,648 walihitimu katika Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) kwa kupata vyeti, stashahada na shahada mbali mbali.
Ndugu Wananchi,
Wanafunzi wa elimu ya juu, masomo yao yanagharamiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu ya Zanzibar na baadhi yao wanalipiwa na Bodi ya Mikopo ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.Bodi  ya Mikopo ya Zanzibar imeshatumia jumla ya TZS Bilioni 60.2, kwa ajili ya kuwadhamini wanafunzi 4,145 wa elimu ya juu katika vyuo vikuu mbali mbali vya ndani na nje ya nchi. Serikali inawalipia gharama  zote wanafunzi wanaofaulu daraja kwanza katika mitihani ya kidato cha sita, kutoka wanafunzi 10 mwaka 2016 hadi 60 mwaka 2019.

Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inatekeleza kwa mafanikio makubwa Sera yake ya kutoa matibabu bure kama ilivyoanzishwa mara tu baada ya Mapinduzi ya tarehe 12 Januari, 1964.
Kutokana na kuongezeka kwa bajeti ya Wizara ya Afya kwa mara 9.6 kutoka TZS Bilioni 10.81 mwaka 2010/2011 hadi TZS Bilioni 104.24 mwaka 2019/2020, huduma za afya zimeimarika sana na zinaendelea kutolewa bure. Ongezeko la fedha za bajeti zimesaidia sana katika kuziimarisha  huduma za tiba na kinga katika hospitali, vituo vya afya na zahanati zote kwa Unguja na Pemba.  Serikali imeziimarisha huduma za Hospitali ya Mnazi mmoja hadi kufikia hadhi ya hospitali ya rufaa na sasa inatambuliwa rasmi kuwa ni hospitali ya kufundisha madaktari, miongoni mwa hospitali za Jumuiya za Nchi za Afrika ya Mashariki.
Jitihada za Serikali za kusomesha madaktari, wakiwemo madaktari bingwa, zimewezesha kuongeza idadi ya madaktari na watumishi wengine wa afya.  Jitihada hizi zimeimarisha uwiano wa madaktari na watu wanaohudumiwa. Hivi sasa daktari mmoja anawahudumia watu 6,276 (1:6,276) kutoka daktari mmoja kuwahudumia watu 31,838 (1:31,838), mwaka 2010.  Kwa hivyo, kutokana na kuongezeka kwa idadi ya madaktari na wataalamu wengine mbali mbali wa fani za afya, upatikanaji wa vifaa vya kisasa vya uchunguzi wa maradhi na nyenzo mbali mbali za kufanyia kazi, pamoja na kuimarishwa kwa maeneo ya kufanyia kazi kumepelekea huduma zatiba na kinga zizidi kuimarika.
Jitihada za Serikali za kupambana na Malaria zinaendelezwa na kasi ya kuenea kwake bado ipo chini ya asilimia moja (0.4%), ingawa baadhi ya maeneo machache ya Mjini yamebainika kuongezeka wagonjwa wa Malaria.Juhudi zinaendelezwa za utoaji elimu kwa wananchi, ugawaji wa vyandarua vyenye dawa ya muda mrefu na upigaji wa dawa za ndani ya nyumba na maeneo yenye mazalia ya mbu.

Ndugu Wananchi,
Kadhalika, maambukizo ya UKIMWI yameendelea kushuka na  hivi sasa yamefikia kiwango cha asilimia 0.4 kutoka asilimia 0.6 mwaka 2010. Kuhusu vifo vinavyotokana na uzazi vimepungua na vimefikia 155 kwa kila vizazi hai 100,000, ikilinganishwa na vifo 288 kwa kila vizazi hai 100,000 katika mwaka 2010.  Jitihada za kuwaelimisha wajawazito wajifungulie hospitali badala ya majumbani, zimesaidia sana, ambapo mwaka 2010 wajawazito 51,912 walijifungulia majumbani ikilinganishwa na 37,803 mwaka 2019.
Pamoja na mafanikio niliyoyaelezeakatika hotuba yangu hii, kwa kudhibitiwa kwa baadhi ya maradhi, lakini zipo changamoto zilizobainika katika hospitali zetu za Unguja na Pemba; ambazo ni kuongezeka kwa maradhi yasiyoambukiza kama vile maradhi ya sukari, matatizo mbali mbali ya maradhi ya moyo, maradhi ya figo, saratani ya shingo ya kizazi na saratani nyengine.  Matarajio yangu ni kwamba wataalamu wa Taasisi ya Utafiti ya Afya na wengine waliopo katika Idara mbali mbali za hospitali zetu na kwa kuendelea kushirikiana na wataalamu wengine wa Kimataifa; watafanya kazi zao za utafiti kwa bidii, ili Serikali iweze kuchukua hatua za kukabiliana na maradhi hayo.

Ndugu Wananchi,
Serikali imeendelea kuziimarisha huduma za maji safi na salama katika Mikoa yote ya Unguja na Pemba. Utekelezaji wa mradi wa maji wa Mkoa Mjini Magharibi, kwa mkopo wa Dola za Kimarekani Milioni 21.246 kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika, niliouelezea katika hotuba yangu ya miaka miwili iliyopitaumekamilika na umezinduliwa tarehe 6 Januari, 2020.Mradi huu  unatarajiwakuwanufaisha wananchi wanaoishi katika Shehia 11 za Mji Mkongwe na Shehia 16 za maeneo mingine, kwa kupata kiwango cha maji cha uhakika katika matumizi yao ya kila siku.
Kwa upande wa Mkoa wa Kaskazini Unguja, hivi sasa vijiji vya Mkoa huo  vinaendelea kupata huduma bora za maji safi na salama,tangu mwezi wa Aprili 2018, ulipokamilika mradi  uliotekelezwa na Kampuni ya “First Highway Engineering of China”. 
Kwa upande wa Pemba, huduma za maji safi na salama zinapatikana kwa kiwango kizuri, ingawa bado zipo baadhi ya changamoto katika baadhi ya maeneoambayo zinaendelea kufanyiwa kazi.
Mradi wa maji wa Wilaya ya Magharibi “A” na “B” na maeneo mengine, wa mkopo wa Benki ya Exim kutoka India wa Dola za Kimarekani Milioni 92 unatarajiwa kuanza baadae mwaka huu.

Ndugu Wananchi,
Kwa lengo la  kuwawezesha wananchi kiuchumi na kukabiliana na tatizo la ajira, Serikali ilianzisha Mfuko wa Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi katikamwaka 2014, ambaounatoa mikopo isiyo na  riba na yenye masharti nafuu kwa wananchi.Hadi kufikia tarehe 30 Juni, 2019, jumla ya mikopo 2,997 yenye thamani ya TZS Bilioni 4.0, imeshatolewa kwa wananchi wa Unguja na Pemba.
Vile vile, katika jitihada hizo, mnamo mwezi wa Septemba, 2019, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, imeanzisha Mfuko wa Vijana, ili kuwawezesha kiuchumi, utakaokuwa na jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 20, sawa na TZS Bilioni 46 kwa kipindi cha miaka 5 ijayo.  Katika fedha hizo, Dola za Kimarekani Milioni Kumi ni msaada kutoka kwenye Mfuko wa Khalifa Fund wa Sheikh Khalifa Bin Zayed Al Nahyan,  Rais wa UAE na Dola Milioni Kumi zimetolewa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar. Hatua hio itasaidia sana katika juhudi zinazochukuliwa na Serikali katika kukuza ajira na ustawi wa vijana.  Mipango ya matumizi ya fedha hizo imekamilika na utekelezaji wa mpango huo utaanza, baadae mwaka huu.
Kuhusu vikundi vya ushirika na SACCOS, Serikali imeviendeleza, ambapo kuanzia mwaka 2010/2011 hadi Oktoba 2019, jumla ya vyama 39 vya Ushirika vya Akiba na Mikopo na vyengine 1,652 vya uzalishaji mali vimesajiliwa.Hatua hio, imeongeza idadi ya vyama vya ushirika vilivyosajiliwa kufikia 3,676 hadi mwezi Oktoba 2019.Mwamko wa wananchi wa kujiunga na SACCOS umepelekea kuongezeka kwa mitaji ya taasisi hizo  kutoka TZS Bilioni 3.5 mwaka 2013,hadi  TZS Bilioni 14.3 mwaka 2019.

Ndugu Wananchi,
Katika kukabiliana na changamoto zinazowakabili vijana, katika kipindi cha miaka tisa iliyopita, Serikali imechukua hatua ya kuviwezesha vikundi 796 vya vijana kwa kuvipatia mikopo kupitia Mfuko wa Uwezeshaji, ili wajiajiri katika shughuli za kilimo, ufugaji na ushonaji. Kadhalika,katika mwaka 2015, Serikali ilianza kutekeleza azma ya kuanzisha Mabaraza ya Vijana katika ngazi zote, ambayo yamekuwa ni taasisi muhimu za ushirikishwaji wa masuala ya vijana nchini. Hadi kufikia Disemba 2019, jumla ya vijana 16,340 wakiwemo wanawake 8,537 na wanaume 7,803 wamesajiliwa katika Mabaraza hayo.
Serikali kupitia Programu ya Ajira kwa Vijana inakamilisha hatua za kuwaingiza vijana 660 katika mafunzo maalumu ya amali ya miezi sita (6), na baada ya mafunzo hayo vijana watapewa zana za kilimo, vifaa vya uvuvi na ufugaji pamoja na vifaa vya ushonaji. Jumla ya vijana 220 wamepewa mafunzo maalumu ya kazi, kwa msaada wa Serikali na Shirika la Kazi Duniani (ILO), ili waweze kujiajiri katika sekta ya utalii.

Ndugu Wananchi,
Mpango kazi wa miaka mitano wa kumaliza vitendo vya ukatili na udhalilishaji wa wanawake na watoto uliozinduliwa mwezi Agosti, 2017, umeanza kuonesha mafanikio na mwamko wa wananchi umeongezeka katika kuyaripoti matukio hayo.  Jumla ya matukio 1,091 ya udhalilishaji yaliripotiwa katika vituo vya Polisi Unguja na Pemba kwamwaka 2017/2018 ikilinganishwa na matukio 2,449 yaliyoripotiwa mwaka 2016/2017.  Matukio haya yalipungua kwa idadi ya 1358, sawa na asilimia 124.5.  Kwa mwaka 2019, matukio ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji vilivyoripotiwa katika vituo vya Polisi vya Mikoa yote na yalikuwa ni 941.  Idadi hii ni upungufu wa matukio 150  ambayo ni sawa na asilimia 15.9. Jumla ya mashauri 1028 ya udhalilishaji wa kijinsia yalifunguliwa katika mahakama za Mkoa katika kipindi cha miaka 9 iliyopita.  Mashauri 630 yalitolewa uamuzi na mashauri 398 yanaendelea.  Serikali itaendelea kuwachukulia hatua za kisheria wanaowadhalilisha wanawake na watoto.

Ndugu wananchi,
Kwa kutambua kuwa Wazee ni hazina kubwa ya nchi yetu na wana mchango mkubwa kwa  maendeleo ya nchi yetu, Serikali imeendelea kutoa huduma mbali mbali katika kuwatunza wazee kwenye maisha yao ya kila siku, kwa wale wanaoishi katika nyumba za wazee Unguja na Pemba.  Jumla ya wazee 28,022 waliofikia umri wa miaka 70 na zaidi wameendelea kulipwa posho la TZS 20,000 kwa kila mwezi ikiwa Pencheni ya Jamii.
Kutokana na Sera ya Hifadhi ya Jamii iliyoandaliwa mwaka 2014, hivi sasa Serikali inaandaa Mswada wa Sheria kuhusu wazee ambao tayari umepelekwa Baraza la Wawakilishi. Kadhalika, kupitia mfuko wa TASAF, jumla ya wananchi 31,993 wamepatiwa fedha kwa ajili ya shughuli za ujasiriamali, biashara ndogo ndogo, kilimo na ufugaji.  Vile vile, jumla ya TZS Bilioni 40 zimetumika, ili kugharamia miradi 656, yenye kuzinufaisha familia maskini kuhusiana  na masuala ya  afya na elimu.
Kwa upande wa watu wenye Ulemavu, Mfuko wa Watu wenye Ulemavu, ulioanzishwa katika mwaka 2012, ili kuwawezesha kiuchumi, wenye jumla ya TZS Milioni 167,unatarajiwa kuanza kutoa huduma hivi karibuni baada ya kukamilika kwa taratibu za kuuendesha mfuko huo. Vile vile, katika kipindi hiki cha miaka tisa, watu wenye Ulemavu walisaidiwavifaa na nyenzo 2,226 ambavyo viligawiwa Unguja na Pemba.

Ndugu Wananchi,
Katika kipindi cha miaka tisa, shughuli za biashara nchini zimeendelea vyema.  Jumla ya bidhaa zenye thamani ya TZS Bilioni 1,923.49 ziliingizwa nchini ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya TZS Bilioni 710.5 zilizosafirishwa kwenda nje ya nchi.
Kadhalika, biashara baina Tanzania Barana Zanzibar imeendelea kufanyika. Bidhaa zenye thamani ya TZS Bilioni 71.3zilisafirishwa kwenda Tanzania Baramwaka 2011 ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya TZS Bilioni 24.2 zilizosafirishwa mwaka 2018.  Vile vile bidhaa zenye thamani ya TZS Bilioni 114.4 ziliingizwa nchini kutoka Tanzania Bara mwaka 2011 ikilinganishwa na bidhaa zenye thamani ya TZS Bilioni 269.66 zilizoingizwa nchini mwaka 2018. Serikali zetu mbili zitaendelea kuhakikisha kwamba biashara baina ya pande zetu mbili za Muungano inaendelea kufanyika na inaimarishwa, kwa kila upande.

Ndugu Wananchi,
Kuhusu biashara ya karafuu, jumla ya tani 33,549.79za karafuu kavu zenye thamani ya TZS Bilioni 448.684  zimenunuliwa kutoka kwa  wakulima katika kipindi cha mwaka 2010 hadi 2019, na  jumla ya  tani za karafuu 32,142.17 zenye thamani ya Dola za Kimarekani 297,707,844, sawa na TZS Bilioni 553.89 zimeuzwa nje ya nchi.  Katika kipindi cha miaka tisa (9) mfululizo Serikali ilimlipa mkulima kiwango cha asilimia 80 ya bei ya karafuu katika soko la dunia, ambayo ni sawa na TZS 14,000; kwa kilo moja ya karafuu kavu za daraja la kwanza. Vile vile,  Serikali imeanzisha bima  maalumu kwa wakulima wanaopata ajali na kutoa zawadi kwa wakulima bora. Hatua hizo zimewaongezea wakulima wa karafuu ari na juhudi ya kukiendeleza kilimo hicho.
Mpango Mkakati wa Miaka 10  wa kuliendeleza zao  hilo umefanikiwa sana, ambapo jumla ya miche ya mikarafuu 2,617,994 imeoteshwa kuanzia mwaka 2011 hadi  2017, na baadhi ya mikarafuu hio, hivi sasa imeshaanza kuzaa. Vituo vipya na vikubwa vya kununulia karafuu vilijengwa na utaratibu mpya wa kuishughulikia biashara ya karafuu ulitekelezwa kwa mafanikio makubwa.
Nawashukuru wakulima wa karafuu wa Unguja na Pemba kwa kuziuza karafuu zao katika ZSTC na nawapongeza wananchi, ZSTC, Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Vikosi vya Ulinzi na Usalama na Idara Maalum za SMZ na Vikosi Kazi vyote, kwa kuliendeleza na kuliokoa zao la karafuu, kupambana na magendo ya karafuu na kuyadhibiti.

Ndugu Wananchi,
Sekta ya viwanda imeendelea kutoa mchango mkubwa katika kipindi hiki cha Awamu ya Saba. Mchango wa sekta hio katika  Pato la Taifa umeongezeka kutoka asilimia  8.2 mwaka 2013, hadi kufikia asilimia 17.8 mwaka 2018. Utengenezaji wa bidhaa katika baadhi ya viwanda vilivyokuwepo awali na vingine  vilivyoanzishwa katika miaka ya hivi karibuni na wawekezaji binafsi, unazidi kuimarika. Kiwanda cha Mafuta ya Makonyo  na Arki za Mimeakilichopo Wawi – Pemba, kimeimarishwa kwa kufunga mitambo mipya, mashine na vifaa vyengine vipya na vya kisasa, vilivyogharimu jumla ya TZS Bilioni 5.4.  Mipango ya Serikali ya kuanzisha kiwanda cha kusarifu mwani kitakachoendeshwa kwa njia ya ubia na wawekezaji wa Indonesia,  sasa imekamilika.  Kiwanda hicho kitajengwa huko Chamanangwe Wete Pemba, hivi karibuni.
Wakala wa Maendeleo ya Viwanda Vidogo Vidogo, na vya Kati (Small and Medium Industries Development Agency - SMIDA) umeanzishwa, baada ya kutungwa kwa  Sheria Namba 2 ya  Wakala wa Maendeleo ya Viwanda Vidogo  Vidogo, na vya Kati Zanzibar ya mwaka 2018. Jumla ya watu 180,851 wameajiriwa au kujiajiri katika sekta ya viwanda. Natoa pongezi maalum kwa wawekezaji katika sekta binafsi kwa kuendelea kuziunga mkono juhudi za Serkiali  za kuiimarisha sekta hio.

Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,  ya  Awamu ya Saba, imefanya juhudi  za kukuza Sekta ya Utalii kwa kushajiisha uwekezaji na ujenzi wa  hoteli zinazohitajika kwa maendeleo ya sekta hio. Tangu mwaka 2010  hadi 2019, jumla ya hoteli 153 za daraja mbali mbali zimejengwa katika maeneo mbali mbali ya Unguja na Pemba. Hadi kufikia Novemba 2019, Zanzibar  ilikuwa na jumla ya  hoteli  509 zilizosajiliwa  na zinazotoa huduma, ambazo miongoni mwao, 26 ni za nyota tano na 20 za nyota nne.
Kadhalika, juhudi kubwa zimefanywa za kuitangaza Zanzibar katika masoko mapya ya Ulaya na Asia.Idadi ya watalii wanaowasili Zanzibar imeongezeka mara 4 kutoka  133,000 mwaka 2010 hadi kufikia watalii 538,264 mwaka 2019. Hapana shaka lengo lililowekwa katika Ilani ya CCM kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 la kuhakikisha kwamba ifikapo mwisho wa mwaka 2020 watalii wanaoingia Zanzibar wanafikia 500,000, hivi sasa lengo hili limevukwa kwa zaidi ya watalii 38,264 kabla ya kufikia mwisho wa mwaka 2020.  Serikali itaongeza jitihada za kuiimarisha sekta hio, ili idadi ya watalii hasa wa daraja la juu, wanaotembelea nchi yetu izidi kuongezeka.


Ndugu Wananchi,
Kwa lengo la kukuza uchumi, kupata lishe bora na kuwa na usalama wa chakula nchini, Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha kilimo cha mazao mbali mbali. Katika kipindi cha miaka minane iliyopita, Serikali imeendelea kuimarisha kilimo cha mpunga kwa kutoa ruzuku ya asilimia 75  za pembejeo mbali mbali.  Teknolojia ya kisasa ya kilimo cha mpunga cha Shadidi ilitumika kupitia Mradi wa kuongeza uzalishaji na tija (ERPP) ambayo imechangia kuongezeka kwa mavuno ya zao la mpunga. Jitihada hizo za Serikali,  kwa jumla zimepelekea kuongezeka kwa mavuno ya mpunga kutoka tani 21,014 mwaka 2010 hadi tani 47,507 mwaka 2018.  Ongezeko hili ni mara 2.3 zaidi.  Mazao mengine ya chakula, matunda na mboga nayo yaliongezeka kutoka tani 289,481 mwaka 2010 na kufikia tani 375,837 mwaka 2018, sawa na ongezeko la asilimia 30. Hali hio imetuwezesha kujitosheleza kwa chakula kwa asilimia 60 mwaka 2018 kutoka asilimia 51 mwaka 2011 ambapo asilimia nyengine 40 za mahitaji yetu ya chakula yanaingizwa nchini na wafanyabiashara mbali mbali.  Nawapongeza wafanyabiashara wote kwa kuendelea kufanya kazi na Serikali yao na kuiunga mkono.
Katika kukiimarisha na kukiendeleza kilimo cha umwagiliaji maji cha mpunga, tarehe 2 Januari, 2020 ulizinduliwa rasmi Mradi wa ujenzi wa Miundombinu ya Umwagiliaji Maji katika mabonde saba ya mpunga; manne yapo Unguja na matatu Pemba.  Mabonde hayo yana ukubwa wa hekta 1,524.  Mradi wa ujenzi wa miundombinu ya umwagiliaji maji Unguja na Pemba, umegharimu Dola za Kimarekani Milioni 50 ikiwa ni mkopo wa Benki ya Exim ya Jamhuri ya Korea na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imechangia Dola za Kimarekani Milioni 14.
Vile vile, Mpango wa Maendeleo ya Sekta ya Kilimo ya Zanzibar (Zanzibar Agricultural Development Programme - ASDP) utakaogharimu Dola za Kimarekani Milioni 148 kwa muda wa miaka 10, tayari umeanza kutekelezwa na baadhi ya Washirika wa Maendeleo wameanza kusaidia.
Ndugu Wananchi,
Kwa lengo la kuongeza kasi ya mapinduzi ya ufugaji, mwaka 2017 Serikali ilianzisha Taasisi ya Utafiti wa Mifugo, ili kuzishughulikia changamoto za wafugaji na kuzitafutia ufumbuzi.  Vituo vinne vya huduma za mifugo vimefanyiwa matengenezo makubwa.  Kwa lengo la kuimarisha huduma za kinga, tiba na huduma za ugani,jumla ya vijana 224 wamepatiwa mafunzo ya kitaaluma pamoja na vifaa vya kutolea huduma katika shehia zao.  Vile vile, jumla ya vikundi 18 vya ufugaji wa ng’ombe wa maziwa na vikundi 16 vya ufugaji  wa mbuzi wa maziwa vimeanzishwa ambapo ng’ombe wa maziwa wenye mimba 368 na mbuzi wa maziwa 720 walitolewa bure kwa vikundi hivyo. 

Ndugu Wananchi,
Katika kuendeleza sekta ya uvuvi,Serikali ilianzisha Kampuni ya Uvuvi, ZAFICO mwaka 2017. Kampuni hio tayariimenunua meli mpya ya uvuvi iitwayo Sehewa II, iliyotengenezwa Sri Lanka ambayo imegharimu  TZS Bilioni 1.13.Meli hio ilizinduliwarasmi tarehe 2 Disemba, 2019 na itaanza kazi ya uvuvi kwenye Bahari Kuu hivi karibuni.   Vile vile, Kampuni ya ZAFICO katika muda mfupi ujao itaanza ujenzi wa chelezo na mtambo wa kusarifu samaki hapo kwenye bandari ya Malindi.
Jitihada za kuimarisha sekta ya uvuvi zimewezesha kuongezeka kwa kiwango cha samaki kinachovuliwa kutoka tani 25,396 mwaka 2010 hadi tani 35,441 mwaka 2018.  Jitihada hizi za Serikali zitapata mafanikio makubwa baada ya kukamilika mradi wa ujenzi wa soko jipya la kisasa la samaki pamoja na bandari ya kushushia samaki katika eneo la Malindi.  Mradi ambao uliwekewa jiwe la msingi tarehe 3 Januari, 2020.  Ujenzi huu wa jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 11.529 sawa na TZS Bilioni 26.4 ni msaada uliotolewa na  Shirika la JICA la Japan.  Kwa mara nyengine natoa shukurani zangu za dhati kwa uongozi wa JICA na Serikali ya Japan kwa msaada huu mkubwa wenye lengo la kuimarisha sekta ya uvuvi ya Zanzibar. 

Ndugu Wananchi,
Katika kipindi hiki cha Awamu ya Saba, Serikali imepanga na kutekeleza mikakati mbali mbali, ikiwemo kuanzishwa kwa Idara ya Mipango Miji na Vijiji, mwaka 2013, kutayarisha na kuandaa Mpango Mkuu Mpya wa Kuendeleza miji mbali mbali ya Zanzibar pamoja na Jiji la Zanzibar (Zanzibar City).
Hivi sasa, tunashuhudia maendeleo makubwa ya ujenzi wa nyumba za kisasa za makaazi, biashara na za kutoa huduma mbali mbali hapa Zanzibar. Mradi wa ujenzi wa Mji wa Kisasa wa Fumba unatekelezwa na Kampuni ya S.S Bakhresa, Mradi wa ujenzi wa nyumba za Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (ZSSF)huko Mbweni, ambao unakaribia kumalizika  na Mradi wa Ujenzi wa  nyumba katika eneo la Nyamazi unaotekelezwa na Kampuni ya CPS, inaendelea vizuri. Vile vile, Serikali imeanzisha mradi wa ujenzi wa nyumba za makaazi za kisasa za ghorofa sita, majengo ya matumizi mengine, barabara na kadhalika, katika mtaa wa Kwahani, ambapo tarehe 9 Januari, 2020 mradi huo uliwekewa jiwe la msingi.
Mradi wa ujenzi wa maduka makubwa ya biashara hapo Michenzani niliouelezea miaka miwili iliyopita ambao unajengwa na Mfuko wa Hifadhi ya Jamii Zanzibar (ZSSF), hivi sasa unaendelea vizuri. Katika majengo hayo mawiili yanayojengwa, jengo la kwanza litajulikana kwa jina la ”Michenzani Shoping Mall” na lile la pili linalojengwa katika kiwanja cha Maskani Kaka ya Muembe Kisonge, litajulikana kwa jina la ”Sheikh Thabit KomboMall”.  Tarehe 4 Januari, 2020 Mawe ya Msingi yaliwekwa kwa ajili ya ujenzi huu.  Ujenzi huu unatarajiwa kukamilika katika kipindi cha miezi sita (6) ijayo na utagharimu jumla ya TZS Bilioni 36.94 kwa yote mawili.  Pembeni mwa maduka haya makubwa litajengwa jengo jengine kwa ajili ya kuegesha gari (car park), za wananchi watakaokwenda kwenye maduka hayo.  Vile vile, katika kipindi hiki majengo kadhaa ya Ofisi mbali mbali za Serikali Unguja na Pemba, yalijengwa.

Ndugu Wananchi,
Serikali imeweza kuufikisha umeme katika shehia zote za Unguja na Pemba. Hadi sasa, umeme umefikishwa kwenye vijiji 518, pamoja na visiwa vidogo vidogo vitano (5), vilivyoko Pemba. Visiwa hivyo niKisiwa Panza, Makoongwe, Shamiani (Mwambe), Fundo na Uvinje. Hivi sasa, jitihada zinafanywa za kupeleka umeme katika kisiwa cha Kokota na Njauhuko Pemba na kazi hiyo, inatarajiwa kuanza baadae  mwaka huu.
Hivi sasa, Serikali imeanza kutafuta njia mbadala za kupata vyanzo vya nishati ya umeme, kutokana na ongezeko la mahitaji ya nishati hio. Kutokana na utafiti  uliofanywa kwa kushirikiana na Umoja wa Ulaya (EU), umebaini kuwepo kwa uwezekano mkubwa wa kupata umeme kutokana na nishati ya jua.  Serikali inalifanyia kazi suala hili.

Ndugu Wananchi,
Sekta ya Mafuta na Gesi Asilia ni eneo jengine la nishati ambalo Serikali inaendelea kulishughulikia. Baada ya Kampuni ya RAK GAS ya Ras Al Khaimah na Kampuni ya Mafuta na Gesi Asilia ya Zanzibar (ZPDC), kutia saini Mkataba wa Uzalishaji naMgawanyo wa Mafuta na Gesi Asilia  tarehe 23 Oktoba, 2018, kazi za utafutaji wa mafuta na gesi asilia katika kitalu cha Pemba - Zanzibar zimeendelea vizuri.  Taarifa za utafiti uliofanywa angani, kwenye kina kikubwa cha bahari, kina kidogo nanchi kavu kwa Unguja na Pemba. Taarifa hizo zinaendelea kufanyiwa uchambuzi na wataalamu.  Majadiliano kati ya wataalamu wa Zanzibar na Ras Al Khaimah yanaendelea kuhusu utafiti huo uliofanywa.  Serikali itaendelea kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu maendeleo ya kaziya uchimbaji wa mafuta na gesi asilia, hatua kwa hatua.

Ndugu Wananchi,
Mafanikio yamepatikana katika kuimarisha miundombinu ya barabara ambapo, jumla ya kilomita 129 za barabara zimejengwa kwa kiwango cha lami, Unguja na Pemba. Hivi sasa kazi ya ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Unguja, zenye urefu wa kilomita 62.9 zinaendelea kujengwa, pamoja na kilomita 15 zilizobakia za Ole-Kengeja. Kadhalika, ujenzi wa barabara ya Bububu-Mahonda-Mkokotoni (kilomita 31) umekamilika na tayari barabara hio imezinduliwa tarehe 10 Januari, 2020.  Vile vile, Serikali imejenga daraja na barabara yenye urefu wa mita mia nne hapo Kibonde Mzungu, kwa lengo la kukabiliana na changamoto zilizokuwa zikitokea katika maeneo ya Kibondemzungu.Taa za barabarani zimewekwa kwenye daraja hilo. Mradi huo umekamilika na umezinduliwa tarehe 9 Januari, 2020; ambapo kazi inayoendelea sasa ni kuunganisha barabara ya eneo hilo na barabara iliyoishia kituo cha Polisi Fuoni.

Ndugu Wananchi,
Katika kuongeza ufanisi wa shughuli za  bandari, Serikali imefanya jitihada  ya kununua  zana za kisasa za kazi kwa ajili ya kuimarisha huduma za bandari za Unguja na Pemba. Kwa upande wa bandari ya Malindi,hatua hiyo imeongeza kasi  ya utoaji wa huduma  ambapo hivi sasa, meli kubwa zinazofika katika bandari hio, zenye uwezo wa kubeba makontena 6,000, zinaweza kuhudumiwa kwa siku tatu tu badala ya wiki moja, kama ilivyokuwa hapo kabla.
Uamuzi wa Serikali wa kujenga Bandari mpya ya Mpigaduri upo pale pale.  Ujenzi huo umechelewa kutokana na uamuzi wa Serikali wa kuziangalia upya gharama za ujenzi zilizokisiwa mwanzo pamoja na kuandaa michoro na ramani ya ujenzi huo.  Ujenzi huo unatarajiwa kuanza baadae mwaka huu.
Ujenzi wa bandari ya Mafuta na Gesi Asilia huko Mangapwani niliouelezea mwaka jana nao unaendelea vizuri.  Miundombinu ya barabara, umeme na maji inaendelea kutekelezwa. Wananchi wanaoishi katika maeneo hayo tayari wamejengewa nyumba mpya kwenye eneo jengine kwa ajili ya makaazi yao.  Kazi inayoendelea hivi sasa, ni kuandaa michoro ya bandari hio, na kukamilisha majadiliano ya mkopo wa fedha wa Dola za Kimarekani Milioni 140 kwa ajili ya ujenzi wa wa Bandari ya Mpigaduri na Mangapwani.
Katika kipindi cha miaka tisa iliyopita, Shirika la Bandari la Zanzibar lilitoa huduma kwa meli za kigeni 1,509 kwa kuchukua mizigo mchanganyiko yenye uzito wa tani milioni 2.6.  Kadhalika abiria 20,499,164 waliitumia bandari ya Unguja na abiria 9,541,686 walizitumia bandari ya Pemba.
Mbali ya meli ya MV Mapinduzi II iliyonunuliwa kwa gharama ya Dola za Kimarekani Milioni 30.4 kutoka katika Kampuni ya Daewoo ya Korea kuwa inaendelea kutoa huduma vizuri,tarehe 1 Oktoba, 2019, Serikali ilizindua meli nyengine mpya ya mafuta inayoitwaMT Ukombozi II, iliyotengenezwa na Kampuni ya “Damen Shipyard”ya Uholanzi, kwa gharama za EuroMilioni 14.3, sawa na wastaniwa TZS Bilioni 36. Meli hio ina uwezo wa kuchukua tani 3,500 za mafuta kwenye visima vinne vilivyomo ndani ya meli hio.  Baada ya kununuliwa meli hii na ile meli ya zamani ya MT Ukombozi I iliyopo, nnatarajia tatizo la kuadimika kwa mafuta halitokuwepo.

Ndugu Wananchi,
Katika kuziimarisha huduma za Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume, kazi zote zilizopangwa kwa asilimia kubwa tayari zimekamilika; isipokuwa ujenzi wa Jengo la Abiria “Terminal 3” ambao unaendelea.  Jengo hili lilichelewa baada ya kukosekana fedha za ziada za Mradi.  Fedha hizo sasa zimetengwa kwenye Bajeti ya mwaka 2019/2020.  Kazi ya ujenzi imeanza tena baada ya kusita kwa muda wa miaka mitatu na tunatarajia kwamba jengo hilo litakabidhiwa Serikali katika mwezi wa Septemba, 2020.
Kwa upande wa Uwanja wa ndege wa Pemba, Serikali imeuimarisha kwa kutia taa kwenye njia ya kurukia, kutulia na maegesho ya  ndege na yamefanyika matengenezo makubwa ya jengo la abiriapamoja na kuongeza eneo la maegesho ya ndege. Hivi sasa urefu wa njia ya kurukia na kutulia ndege umeongezwa kutoka mita, 1,500 hadi mita 2,300. Hatua hizi zimesaidia kuuongezea hadhi uwanja huo kutoka daraja la nne hadi la tatu.
Pamoja na jitihada za kuimarisha Uwanja wa Pemba, zilizofanywa na Serikali, Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), imesaidia kufanyika kwa  kazi ya upembuzi yakinifu pamoja na michoro yote “design” kwa ajili ya ujenzi wa Uwanja mpya wa kisasa wa Pemba.  Ripoti yaupembuzi yakinifu tayari ishapelekwa AfDB kwa ajili ya kuombewa fedha za ujenzi, kwa kuzingatia taratibu ziliopo.

Ndugu Wananchi,
Kwa  lengo la kuimarisha sekta ya habari na kuongeza ufanisi, katika mwaka  2011, Serikali ilianzisha Shirika ka Utangazaji la Zanzibar (ZBC), lenye kushughulikia kwa pamoja matangazo ya redio na  televisheni ya Zanzibar. Juhudi kubwa zimefanywa katika kuubadilisha mfumo wa urushaji wa matangazo ya redio na televisheni kutoka kwenye analojia na kwenda dijitali, ili kwenda sambamba na mabadiliko ya dunia katika teknolojia ya habari.
Hivi sasa Shirika la  ZBC linawahudumia wananchi kwa kurusha matangazo saa 24,na linaongeza programu mpya  za vipindi vinavyohusu masuala muhimu ya kiuchumi na kijamii. Hatua nyengine ya mafanikio ni kuanza kuonekana kwa ZBC TV kupitia king’amuzi cha DSTV katika chaneli ya 291, jambo ambalo limeongeza idadi ya watazamaji wa televisheni ya ZBC katika nchi mbali mbali za Afrika.
Kwa upande wa Shirika la Magazeti la Zanzibar, Shirika limefanikiwa kulichapisha Gazeti la Serikali la Zanzibar Leo, hapa hapa Zanzibar katika Wakala wa Serikali wa Uchapaji. Gazeti hilo sasa linapatikana na kusambazwa kwa urahisi, ikiwemo kupitia mitandaoni. Kuanzia mwezi Novemba 2019, Shirika limeanza kuchapisha gazeti la Kiingereza liitwalo “Zanzibar Mail”,ili kuwawezesha watumiaji wa lugha ya Kiingereza, wakiwemo watu mbali mbali pamoja na watalii, wanaokuja Zanzibar, kufuatilia taarifa muhimu za maendeleo ya Zanzibar.

Ndugu Wananchi,
Katika kuendeleza sekta ya utamaduni na sanaa,  ilestudio mpya ya kisasa  iliyozinduliwa Rahaleo mwaka 2016, kwa ajili ya wasanii wa filamu na muziki inatumika vizuri.Vile vile, kuanzia mwaka 2010 hadi sasa, bado wasanii wanaendelea kulipwa  mirahaba. Tangu kuanzishwa kwa mfumo huo, jumla ya TZS  Milioni 402.80 zimekusanywa na kugawiwa kwa wasanii na wabunifu.   Vile vile, Tamasha la Filamu la Kimataifa (ZIFF), Sauti za Busara, Tamasha la Utamaduni la Mzanzibari na mengine ya asili yamefanyika.
Kwa lengo la  kuienzi na  kuiendeleza Lugha ya Kiswahili, jumla ya  makongamano matatu ya kimataifa ya Kiswahili yamefanywa katika kipindi cha miaka mitatu mfululizo iliyopita ambayo yaliwashirikisha wataalamu kutoka nchi mbali mbali duniani. Makongamano hayo, yameongeza hamasa na ari kwa wataalamu chipukizi kujifunza kutoka kwa wataalamu wakongwe katika nyanja za isimu na fasihi ya Kiswahili.

Ndugu Wananchi,
Uwanja wa michezo wa Mao-Zedong ambao ulizinduliwa rasmi tarehe 3 Januari, 2018 baada ya kufanyiwa matengenezo na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China,hivi sasa unatumika kwa michezo mbali mbali.Kadhalika, mpango wa Serikali wa kujenga viwanja vya michezo vya wilaya hivi sasa  unaendelea vizuri, katika Wilaya tano. Kadhalika, Serikali imeendeleakuwahamasisha wananchi wafanye mazoezi ya viungo  hasa baada ya kuitangaza tarehe mosi ya Januari ya kila mwaka, kuwa siku ya mazoezi hayo kwa Unguja na Pemba. Hivi sasa, idadi ya vikundi vya mazoezi vinavyoshiriki Bonanza la Mazoezi hapa Zanzibar vimeongezeka kutoka vilabu 12 mwaka 2010/2011 kutoka Unguja tu na kufikia vilabu 82 kutoka Unguja, Pemba na Tanzania bara katika mwaka 2019.

Ndugu Wananchi,
Katika kulisimamia suala la hifadhi ya mazingira na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi, jitihada kadhaa zimefanyika, ikiwemo ujenzi wa kuta na matuta ya kuzuwia  uingiaji wa maji ya bahari katika maeneo ya kilimo na makaazi ya watu.Kadhalika, jumla ya hekta 337 za mikoko zimepandwa katika maeneo mbali mbali yaliyoingia maji ya bahari, Unguja naPemba.
Katika kukabiliana na maafa,  Serikali inaendelea na mradi wa ujenzi wa nyumba 30, kituo cha afya, soko, msikiti na skuli, huko Nungwi, kwa ajili ya kuwahifadhi kwa kuwapatia makaazi bora wananchi walioathiriwa na mvua za Masika mwaka 2017. Mradi kama huo utatekelezwa katika eneo la Tumbe huko Pemba. 

Ndugu Wananchi,
Mradi wa Mji Salama, uliozinduliwa tarehe 3 Oktoba, 2018, kwa awamu ya kwanza ambao ulihusisha ufungaji wa kamera za uangalizi (CCTV) 877, zilizofungwa katika maeneo ya Mji Mkongwe, Uwanja wa Ndege, bandarini na maeneo mengine ya mji Unguja.  Mradi huo umeendelea vizuri ambapo sehemu yake ya pili,iliyohusisha uokozi na uzamiaji kwenye majanga ya baharini, ilizinduliwa rasmi tarehe 2 Januari, 2019.   Mradi huu hivi sasa, unaendelezwa kwa upande wa Pemba na unatarajiwa kuanza hivi karibuni, katika mji wa Chake Chake.


Ndugu Wananchi,
Serikali imeendelea kuchukua hatua za kuimarisha hali ya utendaji, maslahi  na mazingira yaMahakama ya Zanzibar, Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali ikiwa ni hatua muhimu za kuimarisha utawala bora na demokrasia. Vile vile, Tume ya Maadili ya Viongozi wa Umma iliyoanza kazi rasmi mwaka 2016 inatimiza wajibu wake vizuri na watumishi wa umma nao wamehimizwa watekeleze wajibu wao kwa kuwasilisha fomu zao za Tamko la Mali na Madeni kwa wakati uliowekwa.
Serikali imeunda Mamlaka ya Kuzuia Rushwa na Kuhujumu Uchumi Zanzibar (ZAECA) mwaka 2012 kwa lengo la kudhibiti matumzi mabaya ya madaraka na mali ya umma. Tangu kuundwa kwake,Mamlaka hii, imepokea jumla ya tuhuma 592 za makosa ya rushwa na uhujumu uchumi yakiwemo, kuomba rushwa, matumizi mabaya ya ofisi na mali za Serikali, utakasishaji fedha, mgongano wa maslahi, dawa za kulevya na mengineyo.  Tuhuma 482 kati yake, zinaendelea na uchunguzi; tuhuma 82 zimepelekwa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka na tuhuma 45 zipo Mahkamani. Tuhuma nyenginezo zilihamishiwa katika Taasisi nyengine.
Kwa upande wa Mahakama, Serikali imeyafanyia  matengenezo majengo na ofisi za mahakama pamoja na kuyapatia vitendea kazi. Idadi ya Majaji imeongezeka kutoka wanne mwaka 2010, hadi tisa mwaka 2019. Idadi ya Mahakimu hivi sasa imefikia 65 na Makadhi ni 12.Hivi sasa, Serikali imeendelea na ujenzi wa jengo la kisasa  la Mahakama Kuu huko Tunguu, ili kukidhi mahitaji ya Mahakama Kuu ya Zanzibar.  Vile vile, Sheria ya Utawala wa Mahakama Namba 11 ya 2018, imetungwa na imeanza kutumika. Aidha, sheria ya kuanzishwa “Law School” imetungwa na Baraza la Wawakilishi na mafunzo hayo yanatarajiwa kuanza hivi karibuni.


Ndugu Wananchi,
Katika kuimarisha utumishi wa umma na maslahi ya wafanyakazi, Serikali imefanya mageuzi  makubwa ya Utumishi wa Umma hapa Zanzibar, baada ya kupitishwa kwa Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 2 ya mwaka 2011, na kanuni za Utumishi wa Umma za mwaka 2014. Marekebisho ya maslahi ya Wafanyakazi ya mishahara yalifanywa mwaka 2011, 2013, 2015 na 2017 kwa lengo la kuwapa motisha wafanyakazi kwa kuzingatia ukuaji wa mapato yetu.  Nina matumaini makubwa kwamba kutokana na hali ya uchumi wetu unavyoendelea ndugu wafanyakazi vile vile, msishangae kuwa mwaka huu nikakuongezeni chochote.
Kutokana na juhudi hizo za kuimarisha maslahi ya watumishi wa Serikali, matumizi yetu katika ulipaji wa mishahara yameongezekakutoka  TZS Bilioni 83.1 mwaka 2010/2011 hadi kufikia TZS Bilioni 417.9, mwaka 2018/2019,  sawa na ongezeko la mara 5.1.Hata hivyo, licha ya ongezeko hilo, kasi ya ukuaji wa uchumi wetu imetuwezesha kulipa mishahara kwa wakati kwa kipindi chote hicho. Kwa upande wa watumishi wa umma wastaafu, malipo yao ya pencheni yameongezeka kutoka TZS 25,000kwa mwezi katika mwaka 2017 na kufikia TZS 90,000 kwa mwezi hivi sasa.
Kwa upande wa ajira katika utumishi wa umma, kuanzia mwezi Septemba 2011 hadi mwezi Juni 2019, Serikali, kupitia Tume ya Utumishi Serikalini, imetoa fursa za ajira 11,823 katika ngazi na sekta mbali mbali Serikalini. Vile vile, katika utaratibu wa kuratibu upatikanaji wa ajira zenye staha ndani na nje ya nchi, Serikali imeshirikiana na sekta binafsi na kuwezesha kupatikana kwa fursa za ajira 18,826 kati ya mwaka 2011 hadi 2019.

Ndugu Wananchi,
Kwa lengo la kupanua demokrasia na kuongeza ushiriki wa wananchi katika mipango na utekelezaji wa shughuli za maendeleo, Serikali iliamua kuanzisha mfumo wa ugatuzi wa madaraka kwa wananchi; ambao utekelezaji wake ulianza  rasmi mwaka 2017, kwa kuanza na sekta ya elimu, afya na kilimo. Mafanikio ya kuridhisha yanaendelea kupatikana katika sekta hizo zilizogatuliwa na katika ukusanyaji wa mapato.
Kadhalika, natoa shukurani zangu za dhati kwa Waheshimiwa Wajumbe wote wa Baraza la Wawakilishi kwa kazi kubwa waliyoifanya kupitisha Bajeti za Serikali pamoja na miswada ya sheria,kwa lengo la kuimarisha na kusimamia sheria na utawala bora.  Jumla ya Sheria  92 zilizotungwa  ndani ya vipindi viwili vya  Serikali ya Awamu ya Saba, ni pamoja na sheria ya Utawala wa Baraza la Wawakilishi. Haya ni matunda ya juhudi za Waheshimiwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.Nnawapongeza kwa dhati kwa kazi nzuri.

Ndugu Wananchi,
Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar itaendelea kushirikiana  na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuuendeleza na kuudumisha Muungano wetu.  Mimi na Dkt. John Pombe Joseph Magufuli tutahakikisha kuwa Muungano wetu unadumu kwa dhamira ile ile ya Waasisi wetu wa Muungano, Marehemu Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na Marehemu Mzee Abeid Amani Karume na viongozi wetu wa awamu zilizotangulia, ili nchi yetu iendelee kupiga hatua kubwa zaidi na ibaki kuwa ya amani na utulivu.  Tutaendelea kutekeleza wajibu wetu wa Kikatiba na Kisheria katika kuilinda amani, utulivu na maisha ya wananchi na mali zao.  Hatutomchelea kumchukulia hatua mtu yeyote atakayejaribu kuhatarisha amani ya nchi yetu.

Ndugu Wananchi,
Kabla sijamaliza hotuba yangu,natoa  shukurani kwa viongozi  wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania  pamoja na Mabalozi na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa na Binafsi na wageni wengine, kwa kuja kuungana na wananchi katika maadhimisho haya ya miaka 56 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar. Kadhalika, nawapongeza makamanda na wapiganaji wa  Vikosi vyetu vya Ulinzi na Usalama, Idara Maalum za SMZ, kwa kuzifanikisha sherehe zetu kwa gwaride zuri la ukakamavu lililozipamba sherehe zetu za leo.  Vile vile, natoa shukrani kwa wasanii waliotuburudisha, vijana wetu, pamoja na wafanyakazi wa vyombo vya habari kwa kuzitangaza sherehe zetu kwa wananchi ambao kwa sababu mbali mbali hawakuweza kuhudhuria kwenye sherehe hizi katika Uwanja huu wa Amaan.
Natoa shukurani za dhati kwa Viongozi na Wafanyakazi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, kwa jitihada na uzalendo wao katika kuyatekeleza majukumu ya kuwatumikia wananchi, hatua ambayo imetuwezesha kupata mafanikio makubwa ya kiuchumi na katika huduma za jamii. Ni vyema tuziendeleze jitihada hizo kwa kasi zaidi, ili tuzidi kupata mafanikio makubwa zaidi. Shukrani zangu maalum nazitoa kwako, Mheshimiwa Balozi Seif Ali Iddi, Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwa kunisaidia na kwa ushauri wako katika kuiongoza Zanzibar.
Kadhalika, natoa pongezi zangu za dhati kwa Halmashauri ya Maadhimisho inayoongozwa na Mheshimiwa Makamo wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Iddi kwa uongozi wake mahiri ambao umezifanikisha sherehe hizi.  Shukurani na pongezi maalumu nazitoa kwenu ndugu wananchi, kwa mara nyengine, pamoja na wanafunzi kwa kujitokeza kwa wingi kusherehekea maadhimisho ya miaka 56 ya Mapinduzi. Hongereni Sana.

Ndugu Wananchi,
Kama mnavyofahamu kwamba Tume ya Uchaguzi ya Taifa ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, hivi sasa zinaendelea na matayarisho ya Uchaguzi Mkuu, katika tarehe itakayotangazwa hapo baadae.  Kwa hivyo, nakuhimizeni mwende mkajiandikishe kwa ajili ya uchaguzi huo; ili muweze kuitumia haki yenu ya kidemokrasia ya kupiga kura, kwa kuwachagua viongozi mnaowataka; utakapofika wakati.
Nakutakieni nyote kila la kheri na baraka za mwaka mpya wa 2020. Mwenyezi Mungu atuzidishie amani, umoja na mshikamano. Nakutakieni safari njema za kurejea nyumbani.
MAPINDUZI DAIMA
MUNGU IBARIKI ZANZIBAR
MUNGU IBARIKI TANZANIA
MUNGU IBARIKI AFRIKA
Ahsanteni kwa kunisikiliza.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.