Habari za Punde

Msanii wa Kizazi Kipya Ali Kiba (King Kiba) Apongezwa Kwa Ubunifu Wake na Kuisaidia Jamii Kutenga Sehemu ya Kipato Chake.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akizungumza na Msanii Maarufu wa Kizazi Kipya Tanzania King Ali Kiba wa kwanza Kushoto aliyepo Zanzibar na Kampeni yake ya Un Forgettable. Aliye katiu kati ni Mkurugenzi Mkuu wa Zanzibar Cable Television {ZCTV} Mohammed Abdullah Al – Jabir.
Msanii Maarufu wa Kizazi Kipya Tanzania King Ali Kiba akielezea azma ya Kampeni hiyo katika lengo la kuendelea kusaidia Jamii katika Huduma muhimu za Afya.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi wan ne kutoka Kulia akiwa katika Picha ya pamoja na Timu ya Msanii wa Kizazi Kipya Tanzania King Ali Kiba pamoja na wenyeji wake wa Zanzibar.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis.OMPR.                                                                             
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Wasanii Nchini lazima wakumbuke kwamba wanabeba jukumu kubwa ndani ya Jamii katika sanaa yao wanayopaswa zaidi kuifanya katika misingi ya Kuelimisha.
Alisema sanaa licha ya kuchukuwa nafasi kubwa katika njia ya kutoa burudani lakini  pia ina nafasi pana zaidi iwapo itatumiwa katika kutoa Taaluma ambayo hufika kwa haraka kwa Wananchi waliowengi.
Balozi Seif Ali Iddi alisema hayo Ofisini kwake Vuga Mjini Zanzibar wakati akizungumza na Msanii Maarufu Tanzania King Ali Kiba aliyepo Zanzibar kusaidia Jamii akiwa katika Kampeni yake Maalum aliyoianzisha iitwayo Ali Kiba un forgettable.
“ Itapendeza zaidi kama Jamii itaendelea kushuhudia Sanaa inatumiwa vyema katika kuelimisha Jamii kwa vile ni moja ya sehemu inayoweza kufundisha kwa urahisi”. Alisisitiza Balozi Seif.
Alisema Wasanii wengi wa Kikazi Kipya hivi sasa wamekuwa wakilenga zaidi kujishughulisha na nyimbo zinazokiuka maadili hasa eneo la mavazi jambo ambalo ni hatari kuigwa mara moja na Watoto Wadogo  wanaotegemewa kuwa Taifa la hapo baadae.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alimpongeza na kumshukuru Msanii huyo wa Muziki wa Kizazi Kipya King Kiba kwa ubunifu wake wa kuisaidia Jamii na kuamua kutenga sehemu ya Kipato chake  kutokana na Sanaa anayoiendeleza.
Balozi Seif alimuhakikishia Msanii huyo kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa vile inafahamu mchango mkubwa unaotolewa na Wasanii wa fani mbali mbali Nchini kwa Jamii itaendelea kushirikiana nae katika kuona Kampeni yake inafanikiwa na kufikia Malengo yake.
Balozi Seif ambae pia ni mwenyekiti wa Kamati ya Sherehe na Maadhimisho ya Kitaifa Zanzibar alitoa pongezi Maalum kwa Msanii huyo kwa uamuzi wake wa kushiriki kwenye Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya Mwaka 1964 kutimia Miaka 56.
Mapema Msanii huyo wa Muziki wa Kizazi Kipya Nchini King Ali Kiba alisema uamuzi wa kuunda Kampeni hiyo umelenga kuondoa dhana iliyojengeka kwa baadhi ya Watu kufikiria kwamba Muziki ni sehemu ya uhuni.
King Kiba alisema Muziki hutoa ajira nyingi kwa kundi kubwa la Vijana walioamua kuendesha maisha yao kupitia Sanaa zilizomo ndani ya sekta ya ujasiri Amali.
Alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba Kampeni yao kwa jamii iliyolenga zaidi kutoa huduma za Afya katika upimaji bure pia huwatembelea Wanafunzi wa Vyuo Vikuu katika dhana nzima ya kuwajengea uwezo zaidi wa kukabiliana na Mafunzo yao.
Naye Meneja wa Kampeni hiyo Anti Esi Mgimba alisema watafuaria kuona wanaendelea kushikwa mkono katika Kampeni hiyo inayowagusa moja kwa Moja Wananchi wa Maisha ya kawaida.
Esi alisema King Ali Kiba amepewa Ubalozi wa Utalii Zanzibar kazi aliyoikubali na kuiridhia kutokana na mapenzi yake makuwa kwa Wananchi wa Zanzibar lakini bado amekuwa na ushirikiano mdogo kwa baadhi ya wadau katika kufanikisha jukumu hilo kubwa la Taifa.
King Ali Kiba yupo Zanzibar na Kampeni yake ya Ali Kiba Un forgettable chini ya uenyeji wa Mkurugenzi Mkuu wa Zanzibar Cable Television {ZCTV} Mohammed Abdullah Al - Jabir.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.