Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe.Balozi Seif Ali Iddi Asaini Kitabu Cha Maombolezi Kufuatila Kifo cha Mtawala wa Oman Sultan Qaboos Bin Said Al Said.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi Kulia akimpa pole Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Al Hafi Hamid alipofika Ubalozi Mdogo wa Nchi hiyo uliopo Migombani kutia Saini Kitabu cha Maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Mfalme wa Oman Qaboos Bi Said Al Said.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi akitia saini Kitabu cha Maombolezo kwenye Ubalozi wa Oman Zanzibar hapo Migombani kufuatia kifo cha aliyekuwa Mfalme wa Oman Qaboos Bi Said Al Said.
Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed Al Hafi Hamid Kushoto akisisitza umuhimu wa Nchi yake kuendelea kuimarisha Uhusiano wa Kidugu na Zanzibar katika Nyanja tofauti.
Picha na – OMPR – ZNZ.
Na.Othman Khamis OMPR.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ametia saini kitabu cha Maombolezo kufuatia kifo cha aliyekuwa Mtawala wa  Oman Qaboos Bin Said Al Said kilichotokea Usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita kwenye Qasri yake ya Beit Al Baraka Nchini Oman.
Marehemu Qaboos Bin Said Al Said aliyefikisha umri wa Miaka 79 aliitawala Oman kwa miaka 50 ambapo Utawala wa Nchi hiyo unaoongozwa na Mrithi Mpya Binamu wake Haitham Bin Tariq aliyekuwa Waziri wa Mirathi na Utamaduni wa Oman ulitenga siku Tatu za Maombolezo.
Balozi Seif Ali Iddi alitia Saini Kitabu hicho cha Maombolezo ya Kifo cha Kiongozi huyo wa Miaka mingi wa Oman kwenye Ofisi ya Ubalozi Mdogo wa Nchi hiyo uliopo Migombani Mjini Zanzibar.
Akimpa pole Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar Dr. Ahmed  Al  Hafi Hamid kufuatia kifo hicho Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif alisema kifo cha Kiongozi huyo kimewagusa Watu wengi wa Visiwa vya Zanzibar na Oman kwa ujumla.
Balozi Seif alisema Oman na Zanzibar zimekuwa na mafungamano makubwa ya uhusiano wa Kihistoria wa muda mrefu unaotokana na maingilioano makubwa ya Damu baina ya Wananchi wa pande hizo mbili.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwataka Wananchi wa Oman kuendelea kuwa na moyo wa subra katika kipindi hichi kigumu cha Msiba kwa kuondokewa na Kiongozi wao aliyesimamia kuleta mageuzi makubwa ya Kiuchumi ndani ya Taifa hilo la Ghuba.
Akitoa shukrani zake naye Balozi Mdogo wa Oman aliyepo Zanzibar  Dr. Ahmed Al  Hafi Hamid alisema Wananchi wa Oman wamezipokea salamu hizo za Rambi rambi kutoka kwa Ndugu zao wa Zanzibar akiamini kwamba  msiba huo kwa njia moja au nyengine pia imewagusa Wazanzibari walio wengi.
Dr. Ahmed alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba licha ya Oman kupata pengo kubwa la kuondokewa na Kiongozi wao mahiri Marehemu Qaboos lakini bado Nchi hiyo itaendelea kushirikiana na Zanzibar katika kuona zile fursa zilizotolewa hasa katika masuala ya Elimu zinazidi kuimarishwa.
Mfalme Mpya wa Utawala wa Oman  Haitham bin Tariq mbali ya kuwa Waziri alieshughulikia Masuala ya Mirathi na Utamaduni lakini pia alikuwa mjumbe wake maalumu wa Marehemu Qaboos katika shughuli muhimu na aliwahi kufanya kazi ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Oman.
Oman inaendelea kupeperusha Bendera nusu mlingoti kwa muda wa siku 40 kama heshima Maalum kwa kiongozi huyo wa zamani aliyefariki ambaye ataendelea kukumbukwa na wengi kwa mchango wake wa kuleta maendeleo na ufanisi mkubwa katika nchi hiyo ya Kiarabu.

1 comment:

  1. Kwa kweli wazanzibari tumeguswa na msiba huo na tunamtakia marehemu makaz mema huko aliko

    ReplyDelete

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.