Habari za Punde

MHE. MKUCHIKA AKUTANA NA MAKAMISHNA WA TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA KUJADILIANA NAMNA YA KUFANYA KAZI KWA USHIRIKIANO KATIKA MASUALA YA UTAWALA BORA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akizungumzia namna ya kufanya kazi kwa ushirikiano katika masuala ya utawala bora na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora waliomtembelea ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma.

Na Happiness Shayo - Dodoma. 24.01.2020
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) amekutana na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kwa lengo la kujadiliana namna ya kufanya kazi kwa ushirikiano hasa katika masuala ya utawala bora ili kuboresha utendaji kazi na kutoa huduma bora kwa wananchi.

Akizungumza katika kikao kazi hicho kilichofanyika ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma leo, Mhe. Mkuchika amesema ofisi yake iko tayari kushirikiana na Tume hiyo kwani ni wajibu na pia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amekuwa akisisitiza kushirikiana kwa pamoja kabla ya kupeleka hoja mezani kwake.

Aidha, Mhe. Mkuchika amesema kuwa idadi ya malalamiko ya wananchi yanayofanyiwa kazi na ofisi yake yanaongezeka kila mwaka kutokana na utandawazi, kuwapo kwa uwazi serikalini na kutolewa kwa elimu juu ya umuhimu wa wananchi kudai haki zao za msingi.

Mhe. Mkuchika ameweka bayana kuwa ofisi yake inashughulikia masuala ya utawala bora katika sekta zote hivyo malalamiko yote akitolea mfano wa sekta ya maji, madini n.k. yamekuwa yakiwasilishwa ofisini kwake.

Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu za Utawala Bora, Jaji (Mst.) Mathew Mwaimu amesema kuwa lengo la ziara hiyo ni kuomba ushirikiano wa utendaji kazi kati ya ofisi yake na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa sababu kwa pamoja ofisi hizo zinashughulikia masuala ya utawala bora.

Akizungumzia majukumu ya Tume hiyo, Jaji (Mst.) Mathew Mwaimu amesema kuwa, ofisi yake imekuwa ikipokea malalamiko katika eneo la haki za binadamu, ukiukwaji wa misingi ya utawala bora na malalamiko yanayohusu sekta nyinginezo kutoka kwa wananchi, hivyo imekuwa ikiwasaidia walalamikaji kutatua changamoto zinazowakabili kwa kuwasiliana na taasisi husika.

Jaji (Mst.) Mathew amesema kuwa pamoja na changamoto mbalimbali inazokumbana nazo katika utekelezaji wa majukumu yake, ofisi yake itaendelea kufanya kazi kwa bidii na kuhakikisha kunakuwa na matokeo chanya katika kuwahudumia wananchi.

Kikao hicho kimehudhuriwa na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu za Utawala Bora na baadhi ya Watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, ikiwa ni sehemu ya kufahamiana na kuboresha utendaji kazi wa ofisi hizo.  
Kaimu Katibu Mtendaji, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bi. Fatuma Muya akitoa maoni yake wakati wa kikao kazi cha Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) na Makamishna wa Tume hiyo kilichofanyika ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma leo kilichokuwa na lengo la kujadiliana namna ya kufanya kazi kwa ushirikiano katika masuala ya utawala bora.
Baadhi ya Makamishna na Viongozi wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala bora wakimsikiliza Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) wakati wa kikao kilichofanyika ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma leo kuzungumzia namna ya kufanya kazi kwa ushirikiano katika masuala ya utawala bora.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) (wa tatu kutoka kushoto mstari wa mbele) akiwa katika picha ya pamoja na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na baadhi ya watendaji wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala Bora mara baada ya kikao kilichofanyika ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma leo kilichokuwa na lengo la kujadiliana namna ya kufanya kazi kwa ushirikiano katika masuala ya utawala bora.
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapt. (Mst), Mhe. George H. Mkuchika (Mb) akiagana na Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Mohamed Hamad baada ya kikao na Makamishna wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora kilichofanyika ofisini kwake Mtumba, jijini Dodoma leo. Kikao hicho kilikuwa na lengo la kujadiliana namna ya kufanya kazi kwa ushirikiano katika masuala ya utawala bora.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.