Habari za Punde

Hali ya Umaskini Nchini Imekuwa Ikipungua Kutoka Asilimia 39% Mwaka 1991 hadi Asilimia 26.4% Mwaka 2017/2018

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akitoa Taarifa fupi ya Tasaf Zanzibar kwa Niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein kwenye Uzinduzi huo.
Umati wa Viongozi, Wawakilishi wa Kimataifa, Taasisi za Umma na Wanau wa Tasaf uliohudhuria kwenye  Uzinduzi wa Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Tasaf  kwenye Ukumbi wa J.K. Nyerere Mjini Dar es salaam ambapo Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Jamuhuri Dr. John Pombe Magufuli.
Na.Othman Khamis.OMPR.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. John Pombe Joseph Magufuli alisema hali ya umaskini Nchini imekuwa ikipoungua kutoka asilimia 39% Mwaka 1991 hadi asilimia 26.4% Mwaka 2017/2018 hali inayoleta matumaini makubwa wa Jamii hasa lile kundi lenye kipato duni.
Alisema Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania hivi sasa  inaongoza miongoni mwa Mataifa yaliyomo ndani ya  Bara la  Afrika kwa kuwa Nchi iliyojizatiti kupambana kikamilifu na Umaskini kwa mujibu wa Takwimu za Kimataifa zinazosimamiwa na Benki ya Dunia {WB}.
Dr. John Pombe Magufuliu alisema hayo wakati akizindua rasmi  Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} sherehe iliyofanyika katika  Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Jijijini Dar es salaam.
Alieleza kwamba tatizo la Umaskini ni moja ya changamoto linalozikabili Nchi Nyingi Duniani zikiwemo zile za Bara la Afrika ambapo zaidi ya asilimia 55% ya Watu Maskini wanaishi ndani ya Bara hilo ikijidhihirisha wazi kuwa kila Watu Watatu Mmoja ni Maskini.
Alisema Serikali Kuu imekuwa ikibuni  Sera, Mikakati pamoja na Mipango mbali mbali inayoratibu na kusimamia kasi ya kupunguza au ikiwezekana kuondoa kabisa Umaskini ili Taifa linapoingia Uchumi wa Kati ifikapo Mwaka 2025 liwe na uwezo kamili wa kujitegema.
“ Yapo mafanikio makubwa yaliyopatikana tokea kuanza kwa Mpango wa kupunguza Umaskini ndani ya Mdari wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF}”. Alisema Dr. John Pombe Joseph Magufuli.
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania lieleza kwamba aliwapongeza aais Wastaafu wa Tanzania kwa uamuzi wao wa kubuni na kusimamia Mipango ya Maendeleo ndani ya Mfuko wa Jamii Tasaf .
Dr. Magufuli aliwahimiza Viongozi wa Mikoa na Wilaya Nchini Bara na Zanzibar  kufuatilia Mpango huo uliokuwa Mkombozi wa Wananchi wengi, vyenginevyo ni kipimo tosha cha kushindwa kusimamia majukumu yao.
Alifahamisha kwamba ni aibu kwa Viongozi waliopewa jukumu la kusimamia Mpango huo na kuibuka Kaya Hewa katika Awamu za Awali za Mfuko wa Maendeleo katika Mpango wa kupunguza Kaya Umaskini Nchini.
Alifahamisha kuwa zipo changamoto zilizojitokeza na kuibuliwa na Watendaji wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii  za uwepo na Wana kaya Hewa katika maeneo mengi Nchini.
“ Kaya zipatazo elfu 73,561 ziligundulika Nchini kote, Kaya 18,261 wahusika walifariki, Kaya 18,700 hazipo, Kaya 9,903 walihama na Kaya 10 katika Halmashauri”. Alisema Dr. Magufuli.
Alionya kwamba Serikalki haitakuwa na huruma kwa Mtu au Kiongozi ye yote atakayetaka kujinufaisha kibinafsi kupitia Kipindi cha Pili cha Awamu ya Tatu kupitia Mpango huo wa kupunguza Kaya Maskini Tanzania.
Akitoa maelezo mafupi kwenye hafla hiyo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein alisema Utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania ni kielelezo cha jinsi Serikali zote mbili zinavyothamini Wananchi wake.
Dr. Shein katika maelezo hayo mafupi yaliyotolewa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema thamani hiyo ya Serikali kwa Umma wake imezingatia wale wenye mazingira magumu na hivyo kufanya juhudi za kuwaondolea kero zao na kuwajengea maisha bora.
Alisema siri kubwa ya mafanikio katika Utekelezaji wa Miradi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} ni Uratibu na ushirikishwaji wa moja kwa moja wa Wananchi pamoja na usimamizi mzuri wa Fedha zinazotolewa katika kutekeleza Miradi hiyo.
Dr. Shein alibainisha wazi kwamba Wananchi wa Zanzibar, pale inapotajwa Tasaf  maana yake ni kuzungumzia chombo muhimu sana kinachomkomboa Mwananchi Maskini na kumletea Maendeleo kutonana na mabadiliko makubwa katika Kaya zao na Miundombinu inayojengwa kwa njia ya kutoa ajira za muda kwa walengwa.
“ Wananchi wa Zanzibar wamenufaika sana na Utekelezaji wa Awamu ya kwanza ya Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini Tanzania. Najua tumekuwa na TASAF Awamu ya kwanza hadi ya Tatu ambazo zimesaidia kuweka mazingira mazuri kwa Wananchi kujiletea Maendeleo” Alisisitiza Dr. Shein.
Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Walengwa wa Mradi huu wameweza kuongeza idadi ya Milo yao kutoka Mmoja hadi miwili au Mitatu kwa Siku iliyokwenda sambamba na kuimarika kwa mahudhurio ya Watoto wao katika Skuli mbali mbali kutokana na uwezo wa Wazazi kuwahudumia kwa Vifaa, sare na chakula kufuatia ruzuku iliyokuwa ikitolewa.
“ Kaya zimeweza kuanzisha Miradi midogo midogo ya kujiongezea kipato. Ushuhuda wa haya yote umeonekana kutoka kwa walengwa wenyewe katika maeneo mbali mbali ya Utekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini ”. Alisisitiza Dr. Shein.
Akigusia Sekta ya Kilimo Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dr. Ali Mohamed Shein alieleza kwamba Mpango huo umeongeza uzalishaji wa mazao mchanganyiko kutokana na Wana Kaya kuhamasika na sekta hiyo iliyopiga hatua kubwa katika uzalishaji wa mazao mbali mbali.
Alisema ongezeko hilo la uzalishaji  wa mazao tofauti hasa Mpunga limekuja baada ya ujenzi wa Matuta ya kuzuia Maji ya Bahari kuingia katika Mabonde ya Mpunga na hatimae eneo lenye ukubwa wa zaidi ya Ekari 400 limeweza kuokolewa na kuendelea kutumika kwa ajili ya kilimo.
Dr. Shein alifahamisha kwamba hali hii imepelekea maeneo yaliyokuwa yamehamwa na Wakulima kwa muda mrefu sasa yanatumika kwa shughuli za kilimo kinachoonekana kuhamasisha Wananchi waliowengi na hata kujishughulisha pia na ukulima wa Mazao ambayo zamani hayakuwa yakilimwa katika maeneo ya Visiwa vya Unguja na Pemba.
“ Tumekuwa mashahidi wa kuona mfano hai wa mazao mapya yaliyoibuliwa kulimwa kupitia mpango wa kunusuru Kaya Maskini ndani ya Visiwa vya Zanzibar kama vile Vutunguu Maji, Nyanya, Alizeti na Carrot”. Alionyesha faraja yake Dr. Shein.
Alifahamisha kwamba inapendeza kuona kuwa Mpango huu wa Kunusuru Kaya Maskini umekuwa ukiongeza ushiriki wa Wanawake Mjini na Vijijini katika kujihusisha ya shughuli za Kiuchumi kupitia Miradi yao waliyoianzisha.
Rais wa Zanzibar na mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alitoa rai kwa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {TASAF} kuendelea kuwa weledi katika usimamizi wa Mpango huo ili kuyalinda mafanikio yaliyopatikana lakini pia kupata matokeo bora zaidi ilivyokuwa katika Awamu zilizopita.
Dr. Shein alisema kwa upande wa Serikali utaendelea kuwahimiza kutimiza jukumu lake na kuhakikisha kuwa watekelezaji wa Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wanapata fursa ya kuwahudumia Wananchi walengwa ipasavyo.
Mapema akitoa Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango huo wa Kunusuru Kaya Maskini Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania Dr. Ladislaus Mwamanga alisema Kaya maskini katika Awamu iliyomalizika zimewezeshwa kushiriki kazi za uzalishaji Nchini.
Nd. Mwamanga alisema uwezeshwaji huo  ulilenga kwenye Sekta  za Mawasiliano ya Bara bara, Afya, Kilimo, Kazi za ujasiri amali, utunzaji wa Mazingira na Elimu pamoja na kujumuisha Vikundi 22,303 Tanzania Bara na Zanzibar na kuleta mafanikio makubwa.
Mkurugenzi huyo Mtendaji wa Tasaf  Tanzania alifahamisha kwamba kipindi cha Pilicha Awamu ya Tatu ya Tasaf kitazingatia kuondoa changamoto zilizopita ikiwemo uwepo wa Kaya zisizo sifa ambapo Watendaji watakuwa makini kuzifikia Kaya zote Nchini kwa kutumia Teknolojia katika kupata Taarifa sahihi.
Akitoa Takwimu ya Tafas jinsi ilivyosaidia kupunghuza UmaskiniTanzania Mtakwimu Mkuuu  wa Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Dr. Albina Chwaya alisema Watanzania Wanyonge  wamepata fursa zaidi za kuwekeza baada ya kupata ruzuku kutoka Mfuko wa Tasaf.
Dr. Albina alisema Mfuko wa Maendeleo ya Jamii Tanzania {Tasaf} umesaidia kupunguza Ujmaskini kwa asilimia 0.2% hadi Mwaka 2018 hali iliyojionyesha wazi kupiga hatua kubwa kwa upatikanaji wa huduma za Kijamii Nchini.
Alitolea mfano uandikishaji wa Wanafunzi umefikia asilimia 78% kutoka Mwaka 2012 hadi asilimia 83 Mwaka 2018  zoezi lililokwenda sambamba na upatikanaji wa huduma ya Maji safi kwa asilimia 83% na  Makaazi bora kufikia  hadi asilimia 84%.
“ Tanzania sasa imepiga hatua kubwa ya kupunguza kasi ya Umaskini ikilinganishwa na Mataifa ya Rwanda, Kenya, Afrika Kusini, Zambia na Zimbabwe”. Alifafanua Dr. Albina Chwaya.
Akitoa salamu kwa Niaba ya Taasisi na Mashirika  ya Kimataifa Mwakilishi wa Benki ya Dunia Bibi Arora  alisema Programu hiyo imekuja kutokana na matokea mazuri ya Awamu zilizopita  ikizingatiwa lengo Kuu ni kupunguza au kuondosha kabisa Umaskini.
Bibi Arora  alisema kutokana na Tanzania kuonyesha njia bora ya Mikakati yake ya kuondosha Umaskini kwa Wananchi wake Benki ya Dunia imeridhia kutoa Mkopo wa Dola za Kimarekani Milioni 450 sawa na thamani ya Shilingi ya Kitanzania Trilioni  1.04.
Mwakilishi huyo wa Benki ya Dunia ameihakikisha Tanzania kwamba Taasisi yake ya Fedha ya Kimataifa itaendelea kuiunga Mkono katika harakati zake kuondosha au kupunguza Umaskini kwa Wananchi wake na kufikia lengo la Uchumi wa Kati.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.