Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Ali Mohamed Shein Ahutubia Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akihutubia katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Sheria Zanzibar yaliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakiul Kikwajuni Jijini Zanzibar.leo 11,Febuary 2020.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein amewataka wananchi kuheshimu kazi, majukumu na maamuzi ya Tume za Uchaguzi nchini, kwa kuzingatia kuwa taasisi hizo zimeundwa kwa mujibu sheria na Katiba za nchi.

Dk. Shein amesema hayo katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul wakil Kikwajuni mjini hapa katika kilele cha maadhimisho ya siku ya sheria Zanzibar.

Alisema kila mwananchi ana wajibu wa kuhakikisha anaheshimu kazi za vyombo hivyo katika  uendeshaji na utoaji wa maamuzi katika masuala yote yanayohusu uchaguzi wa Zanzibar na ule wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alisema wananchi wana wajibu wakuejiepusha na vitendo vyote vinavyokwenda kinyume na sheria na kanuni zilizowekwa na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC) pamoja na ile ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania (NEC).

Alisema ni vyema kuhakikisha kwamba kila mwenye sifa na haki ya kushiriki katika uchaguzi huo, anafanya hivyo kwa kuelewa kuwa huo ni msingi muhimu wa kudumisha utawala bora na Demokrasia.

Aidha, alizitaka taasisi zinazoshughulikia masuala ya uchaguzi pamoja na usalama wa wananchi kufahamu wajibu walionao na kutekeleza majukumu yao ipasavyo, akibainisha umuhimu wausalama wanchi  kuwa ndio lengo la Serikali.

“Ni vyema ikafahamika kuwa suala la kuendeleza demokrasia na kudumisha hali ya usalama na amani wakati wote ni wajibu wetu wa kikatiba”, alisema.

Alisema Zanzibar ina nafasi ya kujifunza njia bora katika kuendesha kampeni za uchaguzi kwa kuzingatia hoja, ajenda na mambo muhimu ya maendeleo ya jamii na nchi, kama ilivyobainishwa katika Ilani za Uchaguzi badala ya kutumia mwanya huo kufanya kampeni zenye kuleta mifarakano, chuki na uhasama.

Rais Dk. Shein alisema kuna umuhimu wakuhakikisha kampeni za uchaguzi haziwagawi watu kutokana na rangi zao, makabila yao, dini au miji na vijiji walivyotoka.

Akigusi kauli mbiu ya maadhimisho hayo isemayo “Dumisha utawala wa sheria na Demokrasia katika uchaguzi mkuu 2020”, Dk. Shein alisema  suala la kuendeleza Demokrasia na kudumisha hali ya usalama na amani wakati wote ni wajibu wa kikatiba.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imetunga sheria ya uchaguzi namba 4 ya 2018, ikiwa ni juhudi za kukuza na kudunisha demokrasia na utawala bora pamoja na kuhakikisha uchaguzi unakuwa huru na wa haki.

Alisema sheria zimebainisha taratibu zinazopaswa kuchukuliwa pale wananchi wasiporidhika na hatua zilizochukuliwa na moja ya taasisi zinazoshughulikia mchakato wauchaguzi.

“Iwapo mtu hukuridhikana uamuzi wa Tume ya Uchaguzi anaweza kupeleka shauri lake mahakamani kwauamuzi”, alisema.

Alieleza kuwa uamuzi wowote utakaokwendakinyume na taratibu zilizowekwa na sheria, zitasababisha zogo na kuanzisha fujo na hivyo kuwa chanzo cha watu kugombana na hatimae kuingiana maungoni.

Alisema Serikali haitasita kuchukulia hatua za kisheria   dhidi ya watu wote watakaobainika kuhusika na matukio ya aina hiyo.

Alisema kila nchi Duniani ina mfumo wake wa utawala na demokrasia, sambamba na taratibu zakuendesha uchaguzi, ikiwemo namna ya kuwapata viongozi wakushika  nyadhifa tofauti Serikalini.

“Watanzania tuna mfumo wa Demokrasia unaokidhi hali ya usalama na mazingira yetu na ndio maana sio sahihi na sio halali, si haki na haifai kwa Taifa jengine kuingilia mfumo na taratibu halali za uchaguzi wanchi yetu zilizowekwa na Tume ya Uchaguzi”, alisema.

Aidha aliwataka viongozi wavyama vya siasa kuzingatia jukumu kubwa la kuwatumikia na kuwasimamia wanachama  na wafuasi wao kwa kuzingatia misingi ya demokrasia na utawala bora.

“Si vyema chama cha siasa kushutumu kukosekana kwamisingi ya demokrasia katika chama kingine na taasisi nyengine wakati hali hiyo ni mbaya zaidi ndani ya chama kinacholalamika”, alisema.

Dk. Shein alibainisha kuwa demokrasia ya kweli inahitajika ndani ya uongozi wa vyama vya siasa kwakuweka misingi bora ya kuendesha chaguzi za viongozi, kutoa fursa za uongozi kwa watu wenye uwezo pamoja na kujiepusha na hatua za kung’ang’ania madaraka.

Alisema wakati Taifa likijiandaa na uchaguzi mkuu ujao, ana imani kubwa na vyombo vya sherina kusisitiza umuhimu wa kutekeleza vyema majukumu yao kwa uadilifu na haki.

Alisema Serikali itaendelea kuhakikisha hali ya amani na utulivu nchini inaendelea kudumu, na kuwakumbusha wananchi jukumu la kuimarisha utawala wa sheria pamoja na kulinda usalama.

Akigusia juu ya uhuru wa mahakama, Dk. Shein alisema katika kipindi chote akiwa madarakani hajawahi wala kuweka azma ya kuingilia uhuru wa chombo hicho, kwakutambua kuwa ndio nguzo na mhimili wa utawala usiopaswa kuingiliwa.

Alitoa shukurani kwa watendaji wote wa Mahakama pamoja na wale waliochangia na kushiriki katika utayarishaji wa toleo la nane la Kitabu cha “Zanzibar Yearbook of Law”, akibainisha matumaini yake kuwa kitabu hicho kimetayarishwa baada ya kufanyika utafiti wa kutosha.

Aidha, aliwapongeza watendaji hao kwa ubunifu wao wakuanzisha programu maalum ya kwenda kwa wananchi, hususan walioko vijijini kwa ajili ya kuwapatia elimu ya kufahamu haki zao zakikatiba na kisheria.

Mapema, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu alisema  sherehe hizo, alisema kwa vipindi tofauti nUchaguzi wa Zanzibar umekuwa na ushindani mkubwa wakisiasa, hivyo akasisistiza umuhimu wa jamii kuendelea kulinda amani iliopo.

Alisema mfumo wa Demokrasia ya vyma vingi kamwe haupaswi kuwa sababu za kuvuruga amani iliopo, akibainisha matukio kadhaa yaliojitokeza katika chaguzi zilizopita kutokana na wananchi kutotii sheria.

Makungu alitoa ushauri kwa kuwataka wanasheria na mawakili wa kujitegemea kupelekea mapendekezo yao Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ili kusikilizwa kwakuzingatia kuwa Serikali hii ni sikivu, kabla ya kuwasilisha mahakamani.

Alisema Idara ya Mahakama imejipanga kuleta mabadiliko makubwaya kiutendaji katika miaka mitano ijayo katika suala zima la utoaji wahuduma

Nae, Waziri wa Katiba na sheria khamis Juma Mwalimu, alitowa wito kwa wananchi kuendelea kuheshimu na kutii sheria za nchi, kwa kuzingatia kuwa hakuna mtu yeyote alie juu ya sheria.

Alisema Wizara hiyo itaendelea na jukumu la kusimamia Utawala wa sheria na upatikanaji wa haki kwawananchi wote.

Aidha, Mwanasheria Mkuu wa serikali ya Zanzibar Said Hassan Said, alisema wakati wakushereherekea siku ya sheria Zanzibar, kuwa hiyo ni fursa ya kuwakumbusha wananchi juu ya haki waliyonayo  ya kupiga kura kwakuzingatia misingi ya utawala bora na utawala wa sheria.

Alisema dhana ya Utawala bora na utawala wa sheria ni nguzo muhimu ya kuifanya Demokrasia ishamiri na kuleta ustawi wajamii pamoja na  maendeleo yao.

Alisema kila Mzanaibari anayo haki na uhuru wa kushiriki katika mchakato wauchaguzi ili kufikia maamuzi yatakayoleta hatma njema ya  maisha yake na Taifa na kusisitiza wajibu wa kila mwananchi mwenye sifa kujiandikisha. .

Alitoa wito kwa wanancho wote kutumia fursaya kuchagua viongozi kwa kuelewa kuwa fursa hiyo hupatikana kila baada ya miaka mitano.

Vile vile, Mkurugenzi wa Mashtaka Ibrahim Mzee Ibrahim, alisema Ofisi hiyo ina wajibu wa kuwachukulia hatua zakisheria watu wote na taasisi zitakazotenda makosa ya uchaguzi, hivyo akasisitiza haja ya taasisi zinazoshughulikia mchakato wauchaguzi kusimamia vyema majukumu yao.

Katika hafla hiyo iliyohudhuria na Viongozi mbali mbali wa Serikali na wadau wa sekta ya Sheria, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Moahmed Shein, alizindua kitabu cha ‘Zanzibar YearBook of Law’ pamoja na kupokea zawadi maalum iliyoandaliwa na Uongozi wa Idara ya Mahakama Zanzibar.

Abdi Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822 
 E-mail: abdya062@gmail.com

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.