Habari za Punde

Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania Yatoa Taarifa Kwa Vyombo Vya Habari Tume Yakutana na Wadau wa Uchaguzi wa Mikoa ya Dar es Salaam na Pwani

Mwenyekiti wa  Tume ya Taifa ya Uchaguzi, Jaji Rufaa (Mst.) Semistocles Kaijage akisoma hotuba ya ufunguzi wa Mkutano wa Wadau, Jijini Dar es Salaam

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) leo imefanya vikao na wadau wa Uchaguzi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani ikiwa ni maandalizi ya Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. Uboreshaji wa Daftari kwenye mikoa hiyo utafanyika kwa siku saba (7) kuanzia tarehe 14 hadi 20 Februari 2020.

Mikutano hiyo ilifunguliwa na kuongozwa na Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji Rufaa (Mst.) Semistocles Kaijage kwa Dar es Salaam na Makamu Mwenyekiti wa Tume, Mhe. Jaji Rufaa (Mst.) Mbarouk Salim Mbarouk kwa mkoa wa Pwani. 

Mikutano hiyo imewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo Viongozi wa Vyama vya Siasa,Viongozi wa Dini, Wawakilishi wa Asasi za Kiraia, Wawakilishi wa makundi maalum ya Watu wenye Ulemavu, Vijana na Wanawake, Wanahabari na Wazee wa Kimila. 

Viongozi hao wa Tume wamewaasa wadau hao kushirikiana na Tume kuwahamasisha wananchi kujitokeza kwa wingi kujiandikisha na kuboresha taarifa zao kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura.

Kwa upande wake Mhe. Jaji Rufaa (Mst.) Mbarouk Salim Mbarouk ametoa rai kwa wananchi wa Kata ya Kibuta wilayani Kisarawe ambao walishiriki kwenye zoezi la uboreshaji wa majaribio kujitokeza kwa wingi ili taarifa zao ziweze kuingizwa rasmi kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura. 2 Uboreshaji huu unawahusu Raia wa Tanzania ambao wametimiza umri wa miaka 18 na wale ambao watatimiza umri wa miaka 18 siku ya Uchaguzi Mkuu mwezi Oktoba (2020). Pia, unawahusu wale ambao wamehama kutoka maeneo yao ya awali na kuhamia maeneo mengine ya Uchaguzi na wale ambao Kadi zao zimeharibika au kupotea.

Zoezi la uboreshaji litahusisha kuondolewa kwenye Daftari la Kudumu la Wapiga Kura wale waliofariki na wengine waliopoteza sifa. Kwa mujibu wa Kifungu cha 15(5) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 na kifungu cha 21(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa Sura ya 292, Tume inapaswa kuboresha Daftari la Kudumu la Wapiga Kura mara mbili kati ya Uchaguzi Mkuu mmoja na Uchaguzi Mkuu unaofuatia.

“Kadi yako, Kura yako. Nenda Kajiandikishe” Imetolewa na: Idara ya Habari na Elimu ya Mpiga Kura 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.