Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Aongoza Wananchi wa Zanzibar Katika M,aziko ya Waziri Kiongozi wa wa Kwanza Zanzibar na Brigedia Jeneraliu Marehemu Ramadhani Haji Faki Yaliofanyika Kijiji Kwao Mkwajuni Mkoa wa Kaskazini Unguja leo.29-3-2020.


Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akijumuika na Waumini wa Dini ya Kiislam wakati wa kuusalima Mwili wa Marehemu Waziri Kiongozi Mstaaf na Brigedia Jenerali Mstaaf Ramadhani Haji Faki iliongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh. Saleh Omar Kabi,iliofanyika katika Masjid Mushawar Muembeshauri Wilaya ya Mjini Unguja,(kulia kwa Rais) Naibu Kadhiu Mkuu wa Zanzibar. Sheikh Hassan Othman Ngwali na Jaji Mkuu wa Zanzibar Mhe. Omar Othman Makungu na (kushoto kwa Rais) Katibu wa Mufti Mkuu wa Zanzibar.Sheikh. Khalid Ali Mfaume.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Ali Mohamed Shein  leo ameongoza mazishi ya Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki yaliyofanyika kijijini kwao Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa, dini na serikali pamoja na wananchi, ndugu na jamaa walihudhuria  katika mazishi hayo akiwemo Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa Majaliwa, ambaye amemuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli.

Viongozi wengine waliohudhuria ni Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Brigedia Jenerali wa Brigedi ya Nyuki Zanzibar Fadhil Omar Nondo, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee,  Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Said Hassan Said, Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, Mawaziri na viongozi wengine wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar pamoja na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Mapema Alhaj Dk. Shein aliungana na viongozi wa dini, vyama vya siasa na Serikali, ndugu, jamaa, marafiki na wananchi mbali mbali katika sala ya kumsalia Marehemu Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki katika Msikiti Mushawar, Mwembeshauri, Mjini Unguja sala iliyoongozwa na Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Saleh Omar Kahbi.

Mazishi ya Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki yalifanyika kwa taratibu zote za Kidini na Kijeshi ikiwa ni pamoja na kutolewa salamu za heshima, salamu za Kijeshi pamoja na kupigia mizinga 17 zoezi lililoongozwa na Gwaride chini ya kiongozi wake Himid Alawi Nguzo

Akisoma Wasfu wa Marehemu Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki , Waziri Ofisi ya Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mohammed Aboud Mohammed alisema kuwa Marehemu amezaliwa mwaka 1930 katika Kijiji cha Mkwajuni, Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Alisema kuwa Marehemu amesoma elimu ya Msingi hadi darasa la nane na baada ya kuhitimu masomo yake, alijiunga na Jeshi la Polisi  ambapo pia, alipata mafunzo kwa muda wa miezi minane huko SOTCH LOGOSK, iliyokuwa USSR.

Marehemu Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki kwa maelezo ya Waziri Aboud, alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Watu 14 ya Chama cha Afro Shirazi (ASP) iliyoongoza Mapinduzi Matukufu ya Januari 12 mwaka 1964 chini ya uongozi wa Jemedari Rais wa Kwanza wa Zanzibar Marehemu Mzee Abeid Amani Karume.

Aliongeza kuwa Marehemu alikuwa Mjumbe wa Baraza la Mapinduzi (MBM) Mwaka 1964 hadi mwaka 1984 ambapo pia, Marehemu amefanya kazi katika Jeshi la Polisi kwa muda wa miaka 14 akipitia ngazi mbali mbali kuanzia “Full Inspector, Acting Superintendent” mwaka 1964 hadi mwaka 1966 akawa “Full Superintendent.

Waziri Aboud alieleza kuwa Marehemu Ramadhan Haji Faki mnamo mwaka 1964 hadi mwaka 1966 alikuwa Kiongozi wa Idara ya Uhamiaji Zanzibar,  na mwaka 1964 hadi mwaka 1977 Marehemu alikuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya Umoja wa Vijana wa ASP na akawa mwanzilishi wa Kambi za Vijana Zanzibar.

Alieleza kuwa mnamo mwaka 1968 hadi mwaka 1976 Marehemu alikuwa Mwenyekiti wa ASP wa Uagiziaji wa Bidhaa kutoka Nje na mwaka 1976 hadi 1977 alikuwa Mwenyekiti wa ASP, Bandari, meli na Uvuvi na mnamo mwaka 1976 hadi 1977 Marehemu alikuwa Mwenyekiti wa ASP, Hoteli, Utalii na Nyumba za Starehe.

Aidha, alieleza kuwa Marehemu alikuwa Mwanachama Mtiifu wa Chama Cha ASP hadi mwaka 1977 kilipozaliwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kuwa na kadi nambari 000061 ya CCM.

Kwa maelezo ya Waziri Aboud  mwaka 1980 hadi 1983 Marehemu alikuwa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Baraza la Mapinduzi na mwaka 1983 hadi mwaka 1984 Marehemu alikuwa Waziri Kiongozi wa Zanzibar.

Waziri Aboud aliongeza kuwa wakati wa uhai wake, Marehemu alishiriki katika vita vya Kagera vilivyomng’oa adui, Nduli Iddi Amin Dada wa Uganda  na kutokana na Ushujaa wake katika Jeshi alipewa jina la “One Man One Bomb”.

Sambamba na hayo, Waziri Aboud alieleza kuwa Marehemu Waziri Kiongozi Mstaafu Brigedia Jenerali Mstaafu Ramadhan Haji Faki amefariki dunia Machi 28 mwaka huu wa 2020 huko Jijini Dar es Salaam.

Alieleza kuwa hadi anafariki dunia Marehemu ameacha watoto watatu ambapo katika uhai wake alitoa mchango mkubwa kwa Taifa kwani alikuwa kiongozi mzalendo, Mwanamapinduzi, shujaa na mchapakazi.

Aliongeza kuwa Marehemu Ramadhan Haji Faki ameacha pengo kubwa kwani alikuwa mstari wa mbele katika kutetea haki na maendeleo kwani aliweka mbele maslahi ya Taifa na ndio maana akashiriki katika kumng’oa Nduli Idd Amin huko Uganda.

Hivyo, kwa niaba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wanatoa pole kwa familia pamoja na wananchi wote wa Zanzibar.

Pamoja na hayo, Waziri Aboud alieleza kuwa  Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk. John Pombe Magufuli na yeye kwa upande wake anatoa pole kwa familia pamoja na wananchi wote wa Zanzibar kutokana na msiba wa kiongozi huyo. Mwenyezi Mungu ailaze roho ya Marehemu pahala pema Peponi-Amin.

Rajab Mkasaba, Ikulu
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 
 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.