Habari za Punde

Wanaokaidi Agizo la Serikali kuzuia Mikusanyiko kuchukuliwa hatua za Kisheria

Na Takdir Suweid,  Zanzibar 29-03-2020. 
Waziri wa Katiba na Sheria Zanzibar Khamis Juma Maalim amesema Serikali haitowafumbia Macho Wananchi wanaokaidi agizo lililotolewa na Serikali la kuzuia Mikusanyiko katika maeneo yao. 

Akizungumza na Vijana wa Timu ya Mpira Nyarugusu amesema Serikali imepiga marufuku mikusanyiko,hivyo Vijana hao kuendela kucheza Mpira wa Miguu katika Kiwanja hicho ni kosa kisheria. 

Amesema Serikali imetoa agizo hilo si kwa ajili ya kuwakomoa Wananchi bali waweze kujikinga na kupunguza janga la Corona linaloiathiri Dunia kwa sasa, hivyo si vyema kufanya Ukaidi. 

Hata hivyo amewasihi Wananchi kuendelea kutii Sheria bila ya Shuruti ili kujinusuru na athari zinazoweza kujitokeza dhidi yao. 

Mbali na hayo amewaagiza Viongozi wa Shehia, Halmashauri na Mabaraza ya Manispaa kusimamia Agizo la Serikali na kuwafikisha katika sehemu husika wakati watakapowabaini wanakwenda kinyume na maelekezo hayo ili wachukuliwe hatua za kisheria. 

Kwa upande wake Sheha wa Shehia ya Pangawe Abdallah Juma Mtumweni amesema tokea kutangazwa kwa Katazo hilo amezungumza mara kwa mara na Vijana hao lakini wamekuwa wakikaidi na kulazimika kufikisha Malalamiko hayo Viongozi wengine ili kupatiwa Ufumbuzi wa haraka.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.