Habari za Punde

Tamko la vyama vya siasa Zanzibar

 KATIBU mkuu wa Chama cha Demokrasia Makini Ameir Hassan Ameir akitoa tamko kwa niaba ya viongozi wa vyama vya siasa kuhusiana na mambo yanayoendelea nchini katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo (kushoto) makamu Mwenyekiti wa DP-Zanzibar Peter A. Magura na (kulia) ni Makamu Mwenyekiti wa NLD Mfaume Khamis.
 BAADHI ya viongozi wa vyama vya siasa walioshiriki katika tamko, wakisikiliza mwakilishi wao Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia makini (Hayupo pichani) katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo.
 BAADHI ya waandishi wa Habari wakifuatilia Tamko la viongozi wa Vyama vya Siasa Zanzibar katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo

BAADHI ya waandishi wa Habari wakifuatilia Tamko la viongozi wa Vyama vya Siasa Zanzibar katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo
Picha na Ramadhani Ali

Na Ramadhani Ali – Maelezo                         04.04.2020
VIONGOZI wa Vyama Zanzibar wameishauri Msajili wa vyama vya siasa nchini kutathimini kauli za baadhi ya viongozi wa vyama vya siasa hasa wakati huu taifa linaeleka katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Akitoa tamko la Umoja wa vyama vya siasa Zanzibar, Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia Makini, Ameir Hassan Ameir, katika ukumbi wa Sanaa Rahaleo, alisema kauli hizo zinaashiria kuleta uvunjifu wa amani nchini.
Alisema,umoja wao unaridhishwa na utendaji wa serikali iliyopo madarakani kwa kuwafikishia wananchi wake maendeleo na kudumisha amani, mshikamno na ustawi wa jamii kwa ujumla.
Aidha, aliishauri Ofisi ya Msajili wa vyama vya siasa nchini, kuvifuta vyama vya siasa vinavyokwenda kinyume na havitakii mema nchi.
Akizungumzia Tume huru ya Uchaguzi iliyoundwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein,Katibu Ameir alisema, vyama vya siasa vyote vilishauri katika mchakato mzima wa kuundwa tume hiyo.
“Sisi viongozi wa vyama vya siasa kwa upande wa Zanzibar tumeridhishwa na uteuzi wa Tume uliofanywa na Rais ambao umekusanya wataalamu kutoka vyama mbalimbali vya siasa” alisema.
Hata hivyo, viongozi hao, walishauri serikali kuangalia upya muundo wa serikali ya Umoja wa kitaifa ili kuweza kushirikisha vyama vyote vya siasa katika kuunda serikali.
Sambamba na hayo, alisema vyama hivyo vimeridhishwa na utendaji wa mwenendo wa utekelezaji wa ilani ya CCM ya mwaka 2015-2020 inayosimamiwa na Rais wa Jamuhuri ya Muungamo wa Tanzania Dk. Jouhn Pombe Magufuli na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein.
Pamoja na hayo, waliwashauri watendaji wanasimamia maeneo ambayo ilani hiyo inatekelezwa kuhakikisha hawamuangushi Rais ambaye amekuwa mstari wa mbele katika kuboresha sekta ya Afya, Elimu, Ustawi wa Jamii, na Miundombinu mengine Mijini na Vijijini na kuhakikisha inakamilika kwa wakati.
Akizungumzia Ugonjwa wa Corona, walipongeza  juhudi zinazochukuliwa na serikali katika kupambana na ugonjwa huo, ambao umekuwa tishio na kuuwa watu wengi duniani.
Hivyo, aliwaomba wananchi kuwa watulivu huku wakifuata maelekezo yanayotolewa na viongozi wakuu pamoja na wataalamu wa afya katika kujikinga na janga la Corona kwa kujiepusha kukaa vikundi na safari zisizozalazima kwani hadi sasa hakuna chanjo ya Ugonjwa huo.
Sambamba na hayo, waliwaomba viongozi waandamizi hususani wa kitaifa nao kuchukua tahadhari wanapotoka katika safari za kikazi nje ya nchi kuhakikisha wanafuata maelekezo ya wataalamu yanayoyataka kufuata taratibu zote za kujikinga na Ugonjwa ili usisambae ndani ya nchi.
Vyama vilivyoshiriki katika tamko hilo, ni Demokrasia Makini, SAU, UPDP,NLD,DP,TLP,CCK,CCM,TADEA,AFP, NCCR-Mageuzi na ADC.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.