Habari za Punde

Mufti: Hakutokuwa na Sala na Baraza la Eid mwaka huu, waislamu watakiwa kusali Misikitinii

Na Ramadhani Ali                                       20.05.2020
Ofisi ya Mufti Zanzibar imetangaza hakutakuwa na swala na Baraza la Eid –el- Fitri Kitaifa mwaka huu kama iliyvyozoeleka na waislamu wametakiwa kuswali katika misikiti yao.

Akizungumza na Waandishi wa Habari Ofisini kwake Mazizini, Katibu wa Mufti Sheikh Khalidi Ali Mfaume amewataka waumini watakaoshiriki swala ya Eid kufuata maelekezo yote yaliyotolewa na Ofisi hiyo ili kujikinga na maradhi ya Corona.

Alikumbusha baadhi ya maelekezo hayo kuwa ni pamoja na kuacha nafasi baina ya mtu na mtu, kutia udhu majumbani, kuchukua mswala, kuvaa maski, kufupisha kisomo na hotuba kwa lengo la kulinda afya za wananchi.

Alisema Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhajj Dkt. Ali Muhamed Shein atatoa salamu za Eid el Fitri kupitia vyombo vya habari siku ya sikukuu kuanzia saa 4.30 na amewataka wananchi kufuatilia salamu hizo.

Sheikh Khalid alieleza kuwa ni marufuku kuswali Eid el Fitri maeneo ya wazi na amewataka Maimamu na Kamati za misikiti kuhakikisha ibada hiyo inafanyika ndani ya misikiti.

Katibu wa Mufti alisema lengo la Ofisi yake kuchukua tahadhari hizo ni kutokana na hali ya maradhi ilivyo hadi hivi sasa.

IMETOLEWA NA HABARI MAELEZO

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.