Habari za Punde

HOTUBA YA MAONI YA KAMATI YA ARDHI NA MAWASILIANO KUHUSU MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA ARDHI, NYUMBA, MAJI NA NISHATI KWA MWAKA WA FEDHA 2020/2021



Mheshimiwa Spika,
Sina budi kumshukuru Allah (S.W) mwingi wa rehma na utukufu, kwa kutujaalia uhai na Afya njema, na kutuwezesha kukutana tena katika Baraza hili la Tisa, kwa dhamira ya kuendelea kuwatumikia wananchi wa Zanzibar ambao ndio sababu ya sisi kusimama katika Baraza hili.
Aidha nakushukuru na kukupongeza wewe Mheshimiwa Spika, kwa jitihada zako na namna unavyoliongoza Baraza hili tukufu kwa ustadi na upeo mkubwa.  Ni imani yangu kwamba, utaendelea kutuongoza kwa uadilifu na ustadi wa hali ya juu kwa lengo la kuimarisha Demokrasia katika chombo hiki muhimu cha kuwatumikia wananchi katika kipindi hiki kigumu cha janga la maradhi ya ‘COVID 19’.
Mheshimiwa Spika,
Pia, naomba kuchukua fursa hii, kumshukuru na kumpongeza kwa dhati Mhe.Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wake wote kwa jitihada kubwa wanazozichukua katika kulipeleka mbele gurudumu la maendeleo ya nchi yetu na Taifa kwa ujumla.
Mheshimiwa Spika,
Lakini pia kwa namna ya pekee, nawashukuru Wajumbe wote wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano kwa kazi zao nzuri wanazozifanya wakati wote wa kazi za Kamati, jambo ambalo limepelekea wepesi kwangu kuweza kuiongoza Kamati hii inayosimamia Wizaramuhimu kabisa.  Wajumbe wa Kamati wameonesha umahiri, weledi na umakini wa hali ya juu na wameweza kuijadili ipasavyo Bajeti hii na kuhoji mambo mengi ya msingi, kwa lengo la kuhakikisha fedha  wanazoidhinisha katika Baraza hili, zinatumika vizuri na kwa lengo lakuwaletea maendeleo wananchi wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Napenda kutumia fursa hii pia, kuwapongeza na kuwashukuru Wawakilishi wote waliomo katika Baraza lako Tukufu, kwa kuendelea kuwawakilisha na kuwatumikia wananchi waliowachagua. Ni wazi kwamba wananchi wamejenga imani kubwa kwetu, nasi hatuna budi kurejesha imani kwao, kwa kuwatumikia kwa dhati na kwa moyo wetu wote, kwa dhamira ya kutetea maslahi yao katika Baraza hili tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Vile vile, Naomba niwakumbushe wajumbe wenzangu kuwa kipindi chetu cha miaka mitano kimefikia ukingoni, hivyo kila mmoja wetu ajitahidi kutekeleza aliyoahidi na kwa pamoja tutakuwa tumemsaidia Mheshimiwa Rais kutekeleza ilani ya Chama cha Mapinduzi na kukamilisha ahadi zake kwa wananchi waliotuchagua kwa wakati.
Mheshimiwa Spika,
Kabla ya kuendelea na hotuba hii, kwa ruhusa yako, na kwa heshima ya kipeee naomba niwatambue Wajumbe wa Kamati ya Ardhi na Mawasiliano kama ifuatavyo:
1.    Mheshimiwa Hamza Hassan Juma                              Mwenyekiti
2.    Mheshimiwa Suleiman Sarhan Said                                        M/Mwenyekiti
3.    Mheshimiwa Hidaya Ali Makame                                Mjumbe
4.    Mheshimiwa Jaku Hashim Ayoub                               Mjumbe
5.    Mheshimiwa Khadija Omar Ali                                  Mjumbe
6.    Mheshimiwa Said Omar Said                                     Mjumbe
7.    Mheshimiwa Ussi Yahaya Haji                                  Mjumbe
Mheshimiwa Spika,
Aidha, Kamati hii inafanyakazikwa kusaidiwa na Makatibu wawili ambao wamekuwa wakitusaidia kwa kiasi kikubwa na kwa uweledi wa hali ya juu katika kutekeleza majukumu yetu, msaada wa makatibu hao umekuwa chachu ya mafanikio makubwaya Kamati hii. Makatibu hao ni:
1.    Ndg. Fatma Omar Ali                                                Katibu
2.    Ndg. Mwaka Mwinyi Waziri                                       Katibu
Mheshimiwa Spika,
Moja kati ya jukumu la msingi la Kamati yetu ni kuchambua mapendekezo ya Serikali, kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya kila mwaka, hivyo katikakutekeleza jukumu hilo lililoelezwa katika Kanuni ya 96(1)ya Kanuni za Kudumu za Baraza la Wawakilishi (Toleo la 2016), Kamati yangu ilikaa na kuijadili na hatimaye kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati, sasa kwa ruhusa yako na kwa niaba ya Kamati, napenda kuwasilisha maoni ya Kamati kuhusiana na Bajeti hiyo kwa mwaka wa fedha 2020/2021.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya utangulizi huo sasa, naomba nitekeleze jukumu nililopewa na Kamati la kuwasilisha maoni ya Kamati, mbele ya Baraza lako tukufu.
Mheshimiwa Spika,
Kwa mwaka huu wa fedha Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati imepangiwa kutekeleza Programu Kuu Tatu (3) ambapo utekelezaji wake unasimamiwa na Programu Ndogo Saba (6).
PROGRAMU KUU YA USIMAMIZI WA ARDHI NA MAKAAZI
Mheshimiwa Spika,
Programu Kuu hii ina jukumu la kuhakikisha usalama wa matumizi ya ardhi na huduma za makaazi bora kwa wananchi. Aidha Programu Kuu hii inatekelezwa kupitia programu ndogo mbili ambazo ni Programu ndogo ya Utawala wa Ardhi, Nyumba na Makaazi na Programu ndogo ya Utatuzi wa Migogoro ya Ardhi.
PROGRAMU NDOGO YA UTAWALA WA ARDHI, NYUMBA NA MAKAAZI
Mheshimiwa Spika,
Dhumuni la programu ndogo hii ni kuhakikisha usalama wa umiliki wa ardhi na upatikanaji wa makaazi bora kwa wananchi wa Zanzibar.
Mheshimiwa Spika,
Programu ndogo hii inajumuisha Kamisheni ya Ardhi, Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali, Shirika la Nyumba, Wakala wa Majengo, Mamlaka ya Uhifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe, Bodi ya Usajili wa Wakandarasi, Bodi ya Usajili wa Wasanifu, Wahandisi na Wakadiriaji wa Majengo, Bodi ya Condominium pamoja na Bodi ya Kudhibiti Kodi za Nyumba.
KAMISHENI YA ARDHI
Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa Kamisheni ya Ardhi bado wanafanya kazi katika jengo bovu ambalo haliridhishi hata kidogo kwa wafanyakazi wa taasisi hii, Jengo ambalo linavuja kwa kiwango kikubwa hali inayopelekea usumbufu kwa watendaji wa Ofisi hii hasa kwa kipindi kama hiki cha mvua.
Mheshimiwa Spika,
Kamati pia inaiomba Serikali kuwapatia Kamisheni ya Ardhi jengo jipya litakaloendana na hadhi ya utendaji wa taasisi hii na umuhimu wake.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na kazi nzuri inayofanywa na Kamisheni ya Ardhi bado kuna tatizo la ucheleweshaji wa utoaji wa hati za haki ya matumizi ya ardhi kwa wananchi, jambo linalosababisha ongezeko la migogoro ya ardhi katika kisiwa cha Zanzibar. Hivyo, Kamati yangu inaitaka Kamisheni ya Ardhi kuongeza kasi ya utoaji wa hati ya matumizi ya ardhi kwa wananchi na wawekezaji ili waweze kutimiza malengo yao kwa wakati.
Mheshimiwa Spika,
Kamati inaiomba Serikali kupitia Wizara ya Ardhi, Nyumba, Maji na Nishati kuifanyia mapitio ya haraka Sheria ya Ardhi hususan katika kifungu kinachohusiana na utoaji wa “lease” za maeneo ya uwekezaji. Kuchelewa kuifanyia mapitio Sheria hiyo ni kuikosesha Serikali mapato yatokanayo na maeneo ya uwekezaji.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu imegundua miaka ya nyuma kuna watu walipatiwa “Right of Occupance” ambayo maeneo hayo yalipaswa kupatiwa “lease” ambapo Serikali ingeliweza kupata Mapato katika maeneo hayo ya uwekezaji, na hili ndilo jambo linalowafanya watu kuyadhibiti maeneo ya uwekezaji bila ya kuyaendeleza kwa sababu wanajua kuwa hawana jukumu la kulipia wakati wanakuja wawekezaji makini na kutaka kuwekeza katika maeneo hayo ila hawayapati jambo ambalo hukosesha mapato Serikali na ajira kwa vijana wetu.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inamuomba Mhe.Waziri kubadilisha umiliki wa watu hao kutoka “Right of Occupance” kuzibadili ziwe “lease” ili kuongeza thamani ya ardhi lakini pia kupata mapato makubwa ili kuweza kusaidi kunyanyuka kwa uchumi.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaipongeza Serikali kwa kusaidia kutatua migogoro ya Ardhi ambayo imedumu kwa muda mrefu, migogoro mingi iliyokuwepo tangu miaka ya 1995 lakini kwa jitihada zako Mhe. Waziri umekuwa muwazi katika kuwasaidia wanyonge hasa wananchi wa vijijini ambao wamenyang’anywa maeneo na wajanja mbali mbali hasa kutoka mjini.


Mheshimiwa Spika,
Kwa wale wananchi wenye asili ya maeneo hayo ambao wamerithi au ya ukoo wao wasilazimike kupewa “Lease” kwasababu wapo katika ardhi yao lakini kwa wale ambao wamenunua ni lazima wapewe lease ili Serikali ikusanye mapato.
Mheshimiwa Spika,
Pia, Kamati yangu inaiomba Serikali kupitia kwako Mhe. Waziri kulipatia ufumbuzi eneo la Fungu refu Mkokotoni ambalo wananchi wa huko pia wanahitaji ufumbuzi ili nao waweze kulitumia kwa ajili ya shughuli zao za kimaisha na Maendeleo ili kupambana na hali ya umaskini.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu kwa mara nyengine inaipongeza Wizara kwa kuwashajiisha wananchi kusajili na kuigawa mirathi yao kwani kuna familia nyingi zinatumia mali za Mirathi ikiwemo nyumba na Mashamba wakati bado havijarithishwa hili ni jambo baya sana linaweza kwenda kutupatia adhabu kubwa huko tuendako, na wengine mali hizi za mirathi ambazo hazijarithishwa pia huzitumia mapato yake kwa ajili ya kwenda kwenye ibada ya Hijja jambo ambalo ni haramu, kwa hiyo Kamati inaungana na Wizara katika kuwaelimisha wananchi kusajili  mali zao za Mirathi pamoja na kufuata utaratibu wa kuzirithisha ili kila mtu apatewe haki yake na aitumie kwa mipango yake ya Maisha.
Mheshimiwa Spika,
Vile vile, Kamati pia inapongeza Wizara kwa kuendelea kuzitambua Eka tatu tatu na kuzipatia hati lakini ushauri wa Kamati kwa zile Eka ambazo zimeshajengwa nyumba za makaazi sana kwa asilimia kubwa basi ni vyema zikabadilishwa matumizi yake ili ziendane na dhamira ya wananchi kupewa Ekari  tatu kwa ajili ya Kilimo.
Mheshimiwa Spika,
Sambamba na hilo, Kamati yangu inaitaka Idara ya Mipango Miji na Vijiji kuharakisha Upangaji na Upimaji wa Miji na Vijiji na kuweka miundombinu yote muhimu ikiwemo Makaazi, Maofisi, Viwanja vya Michezo, Maeneo ya kufanyia Ibada, Maeneo ya Kilimo, Maeneo ya wazi kwa shughuli za kijamii pamoja na maeneo ya uwekezaji.
Mheshimiwa Spika,
Katika Idara hii bado kuna mambo Kamati yangu inashauri kwamba ni vyema yakatofautishwa maeneo ya Makaazi pamoja na yale ya uwekezaji hasa katika ujenzi wa Mahoteli ya Kitalii kwani kuchanganyika maeneo ya Mahoteli ya kitalii pamoja na Makaazi ya wananchi inachangia kuharibu silka na utamaduni wa uzanzibari, lakini pia unawakosesha utulivu Watalii wanaokuja kutembelea nchi yetu.
Mheshimiwa Spika,
Pia, Kamati yangu inaishauri Idara ya Mipango Miji na Vijiji kushirikiana na Wizara ya Ujenzi na Mawasiliano katika kupanga “Road Master Plan” pamoja na miundombinu ya Maji Machafu kwani tumeona katika miaka ya hivi karibuni Mafuriko yamekuja makubwa na kuathiri maisha na shughuli za kiuchumi.
OFISI YA MTHAMINI MKUU WA SERIKALI
Mheshimiwa Spika,
Hadi hivi sasa Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali bado inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa Kanuni itakayomuongoza Mthamini katika utekelezaji wa kazi zake za uthamini hususan katika masuala ya viwango vya tathmini ya makaazi na vipando hali inayompelekea kushindwa kutekeleza majukumu yake kama Sheria inavyomtaka.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na Kadhia hiyo, Kamati yangu inaiomba Serikali pamoja na Wizara kuharakisha ukamilishaji na upatikanaji wa Kanuni hii ili kuweza kuwaondolewa wananchi usumbufu katika maeneo yote yaliokusudiwa kutekelezwa miradi ya maendeleo. Pia, Kamati yangu inaitaka Afisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali kuweka viwango vya tozo na ada ili ziwasaidie katika kutekeleza Majukumu yao ya kimaisha
Mheshimiwa Spika,
Kuchelewa kwa Kanuni hii inapelekea kuwakosesha wananchi wetu malipo yao kwa wakati hasa katika suala ucheleweshwaji wa ulipaji wa fidia kwa wananchi na pia wakati mwengine hupelekea kucheleweshwa kwa baadhi ya miradi.
Mheshimiwa Spika,
Ufinyu wa Bajeti kwa Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali bado ni changamoto inayokwamisha utekelezaji wa majukumu yao ya kila siku. Ofisi hadi sasa haiwezi kujikimu katika suala zima la ufuatiliaji wa masuala ya uthamini wa mali na vipando kwa taasisi za Umma na za Binafsi.
Mheshimiwa Spika,
Mfano mzuri Ofisi ya Mthamini ilitakiwa kufanya uthamini wa mali na vipando katika mradi wa utanuzi wa Kiwanja cha Ndege Pemba. Kamati inasikitishwa kuona hadi leo Ofisi ya Mthamini imeshindwa kutekeleza suala hilo na kupelekea wananchi kuilalamikia Serikali na kushindwa kujua hatma yao na sababu kubwa ni kuchelewa kwa kupitishwa viwango vya thamani ya mazao na vipando ambavyo vilihitaji vipate baraka ya Bodi ambayo uzinduzi wake ulichelewa.
Mheshimiwa Spika,
Vile vile, Kamati inaipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kwa kuona umuhimu wa kuwaongezea fungu la fedha kwa Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali kutoka katika mfumo wa ‘OC’ na kwenda katika mfumo wa Ruzuku.
Mheshimiwa Spika,
Pamoja na pongezi hizo, Kamati inaiona fedha ya Ruzuku uliopangiwa Ofisi hii ni ndogo sana ambapo ni  Milioni 132, 000,000 tu kwa mwaka mzima wa fedha 2020/2021 hasa ukizingatia Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali ana majukumu mengi ambayo ni ya kiutendaji na kiufuatiliaji zaidi ukilinganisha na Ofisi nyengine.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaiomba Serikali kuiongezea Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikali fedha za Ruzuku kwa lengo la kuisaidia Ofisi hii kuweza kufanya kazi zake kwa ufanisi na kwa wakati uliopangwa.
Mheshimiwa Spika,
Ofisi hii pia ina changamoto ya ukosefu wa Ofisi Pemba hali inayopelekea uzoroteshaji wa utekelezaji wa majukumu yao kwa upande wa Pemba ambapo wafanyakazi waliopo Ofisi ya Unguja hulazimika kufanya kazi pia katika maeneo ya Pemba pale inapohitajika jambo linalowaletea usumbufu mkubwa haswa ukizingatia Ofisi yenyewe ina upungufu wa wafanyakazi.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaiomba Serikali kuharakisha ukamilishaji wa muundo wa Utumishi kwa Ofisi ya Mthamini Mkuu wa Serikaliambao utawapa mamlaka ya kuanzisha Ofisi ya Mthamini kwa upande wa Pemba, lengo ni kuleta ufanisi katika utekelezaji wa majukumu ya kila siku.
MAMLAKA YA HIFADHI NA UENDELEZAJI WA MJI MKONGWE
Mheshimiwa Spika,
Kamati haridhishwi na ukusanyaji wa mapato wa Mamlaka ya Hifadhi na Uendelezaji wa Mji Mkongwe. Kamati inatambua kwamba Mamlaka hii ina uwezo wa kutosha wa kukusanya mapato kama ilivyopangiwa na Serikali kwani ina vyanzo vingi ambavyo vipo hai kiutendaji. Kinachotakiwa ni usimamizi na ufuatiliaji kupitia vyanzo hivyo.
Mheshimiwa Spika,
Kamati inaona wazi kwamba Mamlaka hii haisimamii wala haifuatilii ipasavyo vyanzo vyake vya mapato ya ndani jambo ambalo linalowapelekea wao kushindwa kufikia malengo ya mapato wanaokadiriwa kuyakusanya kwa mwaka wa fedha husika.
Mheshimiwa Spika,
Mfano halisi wa hilo, mnamo mwaka 2019/2020 Mamlaka hii ilipangiwa kukusanya katika kianzio chake cha utoaji wa vibali vya ujenzi ilipangiwa kukusanya Milioni 150,000,000 ambapo hadi kumalizika kwa mwaka huo wa fedha imefanikiwa kukusanya Milioni 22,640,000 tu ambapo sawa na asilimia 15.1 na kwa upande wa kianzio cha mapato ya kazi za biashara ilipangiwa kukusanya Milioni 55,000,000 ambapo hadi kumalizika kwa mwaka huo wa fedha imefanikiwa kukusanya Milioni 3,450,000 tu sawa na asilimia 6.3kwa kweli hii haileti picha nzuri katika ukusanyaji wa mapato Kamati inaomba Serikali kuweka umakini mkubwa katika usimamizi na ukusanyaji wa mapato kwa Bajeti ijayo .
Mheshimiwa Spika,
Hali hii hairidhishi hata kidogo, Kamati yangu inaiomba Serikali kwa kushirikiana na Wizara ya Fedha na Mipango kufanya ufuatiliaji wa karibu na wa mara kwa mara kwa taasisi zetu zote kwa lengo la kubaini changamoto zinazowakabili katika zoezi zima la ukusanyaji wa mapato kupitia vianzio wanavyopangiwa.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaona wazi kwamba kuna uvunjaji wa mapato ya Serikali ndani ya Taasisi zetu. Kwa jicho la karibu tunaona wazi kwamba Mamlaka hii kuna tatizo linalopelekea kutofikia malengo ya fedha waliopangiwa kuyakusanya.
Mheshimiwa Spika,
Pia, Mamlaka hii ina tatizo la kuchelewesha majibu ya maombi ya vibali vya ujenzi kwa waombaji husika katika maeneo ya Mji Mkongwe ambayo yana azma njema ya kuwekeza katika Hifadhi ya Mji wetu wa Kihistoria.


Mheshimiwa Spika,
Uchelewaji wa majibu hayo kwa baadhi ya wawekezaji wanaotaka kuwekeza katika hifadhi ya Mji Mkongwe hupelekea kuikosesha Mapato makubwa Serikali yetu kwa maslahi ya nchi hii.
Mheshimiwa Spika,
Kutokana na changamoto hii, Kamati inaiomba Mamlaka hii kufanya haraka kuzijibu barua zote zinazofika ofisini kwao kwa ajili ya maombi kwani kufanya hivyo ni kuisaidia Serikali kiingiza mapato yake ya ndani na kinyume chake ni kuikosesha Serikali mapato hali inayopelekea kuathiri uchumi wetu.
WAKALA WA MAJENGO
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inampongeza  Mkurugenzi wa Waakala wa Majengo pamoja na watendaji wake kwa kazi kubwa za kizalendo wanazozifanya za kusimamia ujenzi wa baadhi ya taasisi za Serikali kwa kutumia gharama ndogo kulingana na uzito wa kazi wanazozifanya.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaitaka Waakala kuandaa Kanuni zitakazowaekea makisio ya ujenzi au ukarabati tofauti na hivi sasa Wakala anategemea ruzuku tu kutoka Serikalini kwani Wakala anao uwezo wa kuendesha taasisi kupitia vianzio vyake vya ndani.
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaipongeza Serikali kwa kusikia kilio chetu cha siku nyingi cha kujenga Jengo lao la Ofisi linalolingana na hadhi yao. Kutokana na hali hiyo, Kamati yangu imefarijika kuona kuwa Wakala tayari imeshapata eneo la kujenga Ofisi zao za kudumu.

PROGRAMU NDOGO YA UTATUZI WA MIGOGORO YA ARDHI
MAHAKAMA YA ARDHI
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inampongeza sana Mwenyekiti mpywa wa Mahakama ya Ardhi kwanza kwa mashirikiano yake kwa Kamati lakini pia kwa kuendeleza yale mema yote yalioanzishwa na Mwenyekiti aliyetangulia, akishirikiana na Mahakimu wenzake kwa kuharakisha uendeshaji wa kesi lakini pia uharaka wa kuendesha kesi hizo na wananchi wengi wanaridhika na utendaji wa Mahakama ya Ardhi kwa utendaji wao, isipokuwa tu Kamati imegundua kuna changamoto nyingi katika mahakama hizo kama tulivyoelezea katika kikao kilichopita kwenye ripoti za Kamati, kwa kifupi nizielezee baadhi yao ili iwe dira katika awamu ijayo.
1.    Kwanza uhaba wa wafanyakazi katika Mahakama zote za Unguja na Pemba.

2.    Uhaba wa Mahakimu katika Mahakama zote za Unguja na Pemba jambo ambalo inambidi Mwenyewe Mwenyekiti wa Mahakama ya Ardhi aingie kazini kwendwa kuendesha Kesi wakati alitakiwa asimamie masuala ya kiutawala zaidi.

3.    Karibu Mahakama zetu zote hazina Majengo yao wenyewe na zinafanyakazi katika Majengo ya kuazima jambo ambalo linaleta shida katika utendaji wa kazi zao Kamati yangu inaitaka Kamisheni ya Ardhi kuwapatia maeneo Mahakama ya Ardhi kwa Unguja na Pemba ili kujenga Majengo yanayolingana na kazi zao.

4.    Changamoto nyengine ni ukosefu wa usafiri kwa Mahakimu wote wa Unguja na Pemba jambo hili halileti afya kwenye utoaji wa haki.

5.    Uhaba wa Bajeti ambao umesababisha malimbikizo ya madeni ambayo watendaji ilibidi wakope “Stationaries” pamoja na “Furnitures” ili utendaji wa Mahkama uendelee vizuri lakini madeni hayo bado yapo hadi leo. Kamati yangu inaitaka Serikali kupitia Wizara iwaingizie fedha za kutosha na kwa wakati ili waweze kulipa madeni na kuweza kujikimu katika harakati zao za uendeshaji wa ofisi.

6.    Ukosefu w usafiri kwa Wazee wa Mahakama ambapo siku za mvua wanapata usumbufu wa kufika kazini kwa wakati na hili huleta usumbufu kwa wenye Kesi.

7.    Suala la maslahi ya Mahakimu, Kamati yangu inaitaka Wizara kuharakisha “Scheme of Service” ya Mahakimu ili ilingane na uzito wa kazi zao.

8.     Kamati imeona kuna ukosefu wa mavazi kwa Wazee wa Mahakama kwani kazi zao nyingi huambatana na kutembelea baadhi ya maeneo yenye migogoro na yenye mwitu, miiba na hata Mawe kwa hiyo Kamati inaitaka Mahakama ya Ardhi kuwapatia vifaa ikiwemo makoti ya mvua na viatu ili waweze kufanya kazi muda wote.

PROGRAMU KUU YA USIMAMIZI WA HUDUMA ZA MAJI NA NISHATI

Mheshimiwa Spika,
Programu Kuu hii  inasimamiwa na Mamlaka ya Maji (ZAWA), Shirika la Umeme (ZECO), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Maji na Nishati (ZURA), Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uendelezaji wa Mafuta na Gesi Asilia (ZPRA), Kampuni ya Maendeleo ya Mafuta na Gesi Asilia(ZPDC) pamoja na Idara ya Nishati na Madini.
IDARA YA NISHATI NA MADINI
Mheshimiwa Spika,
Kwa mara nyengine tena, Kamati yangu imebaini kuwa Idara ya Nishati na Madini haina Sera ya Nishati na Madini ambayo ndio muongozo mkuu wa utekelezaji wa kazi za idara hii.

Mheshimiwa Spika,
Kwa kuchukuwa umuhimu wa Sera hii, Kamati yangu inaiomba Serikali kupitia bajeti hii ya 2020/2021 kutenga fedha maalum za ukamilishaji wa Sera hiyo muhimu kwa maslahi ya Taifa kwani kukosekana kwa Sera hii inapelekea kukwamisha utekelezaji wa baadhi ya miradi ya uwekezaji katika Sekta hii ya Nishati na Madini.

Mheshimiwa Spika,
Kwani nchi yetu hivi sasa imo katika kutafuta wawekezaji kuja kuwekeza katika Sekta ya Nishati ya Umeme Mbadala kama inavyofahamika kuwa sio rahisi kwa muwekezaji yeyote ambaye yuko tayari kuja kuwekeza katika nchi iliyokuwa haina Sera madhubuti itakayomuongoza katika uwekezaji, ndio maana Kamati yangu inaitaka Wizara kukamilisha Sera hiyo ili Wawekezaji makini waje kuwekeza ndani ya Serikali yetu.

SHIRIKA LA UMEME (ZECO)
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu haina budi kuwapongeza Mkurugenzi Mkuu wa Shirika pamoja na watendaji wake kwa kazi kubwa ya kutupatia huduma za nishati ya umeme kwa muda wote wa masaa ishirini na nne.

Mheshimiwa Spika,
Pongezi maalumu ziende kwa Uongozi wa Shirika kwa kutoa na kutekeleza agizo la Mhe. Rais alilolitoa kwa ajili ya kulipa deni lote kutoka Tanesco kutokana na malimbikizo ya muda mrefu tunashukuru deni hilo sasa limemalizika. Pamoja na hayo, Kmati yangu inalitaka Shirika lisibweteka deni hilo lisije kujirudia tena.

MAMLAKA YA UDHIBITI WA HUDUMA ZA MAJI NA NISHATI (ZURA)

Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inaipongeza Mamlaka hii kwa kazi kubwa wanayoifanya ya kuhakikisha wananchi wa Zanzibar wanapata huduma ya Maji na Mafuta iliyo katika kiwango bora lakini pia na bei iliyo sahihi, Kamati yangu inapongeza tena jitihada inayofanywa na Mamlaka hii kwa kuweza kuvikagua Vituo vya Mafuta mara kwa mara ili kuhakikisha mafuta yanayotumika ni yanayokidhi kiwango bora.

Mheshimiwa Spika,
Pongezi maalum ziwaendee Mkurugenzi Mkuu, Naibu Mkurugenzi Mkuu na watendaji wote kwa ubunifu wao wa kujenga jengo bora la kisasa la Makao Makuu ya Mamlaka pamoja na Wizara nzima jambo hili ni la mfano wa kuigwa.

Mheshimiwa Spika,
Kwa upande wa Bandari ya Mafuta, Kamati yangubado inaendelea kutoa masikitiko kwa Serikali kwa kuuhamisha Mradi wa Ujenzi wa Bandari ya Mafuta na Gesi kutokuwepo chini ya usimamizi wa ZURA na kushughulikiwa na taasisi nyengine jambo ambalo wenyewe ZURA ndio wanaojua changamoto zinazowakuta hasa wakati mafuta yanapokosekana nchini na pale meli zinapochelewa kufika za Mafuta hapa Zanzibar ndio maana ya kubuniwa mpango huo wa Bandari ya Mafuta na Gesi katika eneo la Mangapwani.

MAMLAKAYA UDHIBITI WA UTAFUTAJI NA UENDELEZAJI WA MAFUTA NA GESI ASILIA (ZPRA).
Mheshimiwa Spika,
Kamati yangu inapenda kutoa mkono wa pole kwa wafanyakazi wote wa taasisi hii kwa kuondokewa na kiongozi wao shupavu, mahiri na mtaalamu kwa masuala ya utafutaji na uendelezaji wa taaluma ya mafuta na gesi asilia nchini Ndg. Omar Zubeir Ismail Mwenyezi Mungu ailaze roho ya marehemu huyu peponi Amin.

Mheshimiwa Spika,
Mamlaka hii kwa upande wake imekabiliwa na changamoto yaushirikishwaji mdogo wa wananchi wakati wa zoezi la Uchimbaji na Utafutaji wa Mafuta na Gesi Asilia unapoendelea.

Mheshimiwa Spika,
Kutokana hali hii, Kamati yangu inaiomba Mamlaka hii kuwashirikisha wananchi kikamilifu katika zoezi zima la Utafutaji na Uchimbaji wa Rasilimali ya Mafuta na Gesi Asilia kwa yale maeneo yote yanayopitiwa na mradi huo.

Mheshimiwa Spika,
Kufanya hivyo ni kuondoa malalamiko kwa wananchi dhidi ya Serikali yao na pia itasaidia kuondoa changamoto ndogo ndogo zinazoweza kujitokeza wakati zoezi la Mradi litakapokuwa linaendelea.

Mheshimiwa Spika,
Vile vile, Kamati yangu inaikumbusha ZPRA kwamba bado wananchi waliyoathirika na zoezi la Mitetemo bado hawajalipwa fidia jambo ambalo wanachi wetu wamekuwa wakililalamikia suala hilo, ingawa kwa taarifa tulizonazo kuwa fedha za kulipa wananchi fidia zipo ila ilikuwa inasubiriwa Bodi ya Mtathmini Mkuu wa Serikali ipitishe viwango vya malipo ili fedha hizo ziweze kulipwa kwa Wananchi husika.

Mheshimiwa Spika,
Kutokana na muda nitashindwa kuzijadili baadhi ya taasisi zilizomo katika Wizara hii nitaomba wayazingatie maoni yetu tuliowasilisha wakati wa Ripoti za Kamati. Tunaamini zitaweza kuwasaidia katika kufanikisha majukumu yao ya kila siku.

Mheshimiwa Spika,
Baada ya maoni hayo ambayo yamejikita katika Programu Kuu na Ndogo zilizo na umuhimu zaidi kwa Kamati yangu, ili kuhakikisha Wizara hii inatekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa. Kamati yangu inazipongeza taasisi zote kama vile Bodi ya Wakadiriaji wa Majengo, Bodi ya Wakandarasi, Bodi ya Uhaulishaji Ardhi, Bodi ya Ukondoshaji (Condominium).

Mheshimiwa Spika,
Baada ya hotuba nzuri iliyosomwa na mheshimiwa Waziri pamoja na Maoni haya ya Kamati ya Ardhi na Mawasiliano nawaomba wajumbe wengine wa Baraza lako Tukufu waichaingie vyema bajeti hi na hatimaye kuipitisha kwa lengo la kupata utekelezaji bora kwa maslahi ya wananchi wetu.
Mheshimiwa Spika,
Mimi mwenyewe binafsi na kwa niaba ya Kamati ninayoiongoza ya Ardhi na Mawasiliano, naiunga mkono hoja hii kwa asilimia 100%.
Mheshimiwa Spika,
Baada ya Maelezo hayo, naomba kuwasilisha.
Ahsante,
Mhe. Hamza Hassan Juma
Mwenyekiti,Kamati ya Ardhi na Mawasiliano,
Baraza la Wawakilishi,
Zanzibar.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.