|
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA BORA
Kitalu Na. 339, Mtaa wa Nyerere - Kilimani
S.L.P 4019, DODOMA
Simu: +255 734 047 775; 734 119 978
Barua Pepe: info@chragg.go.tz
Tovuti: www.chragg.go.tz
|
Juni
16, 2020
TAARIFA KWA
VYOMBO VYA HABARI
Tamko
la Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) wakati wa Maadhimisho ya
Siku ya Mtoto wa Afrika Juni 16, 2020
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB)
inaungana na wadau wote wa haki za watoto katika kuadhimisha “Siku ya mtoto wa Afrika”. Siku hii
inaikumbusha dunia juu ya mauaji ya watoto wapatao 2,000 wa kitongoji cha
Soweto nchini Afrika Kusini, waliouawa kikatili miaka 44 iliyopita na iliyokuwa
Serikali ya Makaburu.
Siku hii ilizinduliwa rasmi Mwaka 1991 na uliokuwa Umoja
wa Nchi Huru za Afrika (OAU) ili kuwakumbuka watoto hao waliokuwa wakidai haki
ya kutobaguliwa na haki nyingine za binadamu.
Wakati tunaadhimisha siku hii muhimu wadau wote wa haki
za watoto hatuna budi kujitathimini namna tulivyoandaa na kutekeleza mifumo rafiki
na inayofikiwa na wote katika kulinda haki za watoto kwa kuzingatia kauli mbiu
ya mwaka huu inayosema: “Mifumo rafiki
ya upatikanaji wa haki ya mtoto: Ni msingi wa kulinda haki zao.”
THBUB
inapenda kupongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kwa hatua mbalimbali zinazochukua katika kulinda haki na maslahi
ya watoto. Hatua hizo ni pamoja na kuridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa na
kikanda, kutunga sera, sheria, kanuni, miongozo na kuandaa mipango na mikakati
mbalimbali inayolinda, kutetea na kukuza haki za mtoto.
Miongoni
mwa mikataba ambayo Tanzania imeridhia ni Mkataba
wa Kimataifa wa Haki za Mtoto (1989) na
Mkataba wa Afrika wa Haki na Ustawi wa Mtoto (2003).
Kwa upande wa sheria, Tanzania imefanikiwa kutunga sheria
mbali mbali zikiwemo Sheria ya Mtoto Na.21/2009,Sheria ya Mtoto Na. 6/2011, Sheria ya Kanuni za Adhabu na Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai, Tanzania Bara
na Zanzibar. Aidha, kanuni mbalimbali zimetungwa zikiwemo Kanuni za Mahabusu za
Watoto, Kanuni za Ulinzi wa Mtoto, Kanuni za Shule ya Maadilisho, Kanuni za
Mahakama za Watoto na Kanuni za Kamati za Ustawi katika kulinda haki za mtoto.
Sera ya Mtoto (2008) na Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kuzuia
na Kupambana na Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (2017 - 2022) ni miongoni
mwa nyezo nyingine zilizoandaliwa kuhakikisha ustawi wa haki za mtoto hapa
nchini.
THBUB inatambua kupitia Mikataba, Sera, Sheria, Miongozo
na Mipango hio, mifumo rafiki ya kusimamia upatikanaji wa haki kwa watoto imeanzishwa
na kuimarishwa. Mifumo hiyo ni pamoja na mahakama za watoto, madawati ya jinsia
na watoto katika vituo vya polisi, mahabusu za watoto, mabaraza ya watoto na
Shule ya maadilisho. Vile vile, mafunzo ya kuwajengea uwezo watumishi katika
taasisi hizi yamekuwa yakifanyika mara kwa mara ili kuwawezesha watumishi kutekeleza
majukumu yao ya kusimamia utekelezaji wa haki kwa watoto kwa ufanisi mkubwa.
Pamoja na jitihada hizo, bado kuna changamoto mbalimbali
zinazoathiri upatikanaji wa haki za watoto katika jamii. Changamoto hizo ni pamoja na watoto kuwekwa
vizuizini katika magereza ya watu wazima kinyume na sheria ya mtoto, watoto kutopata
msaada wa kisheria wakiwepo katika mkinzano na sheria na uelewa mdogo wa jamii
kuhusu Sheria ya Mtoto na Kanuni zake. Nyingine ni ukeketaji, utumikishaji wa
watoto, unyanyasaji wa kingono, kimwili, kisaikolojia na mimba za utotoni ambazo
zimekuwa na athari kwa mtoto kiafya na kielimu.
Hivyo basi, THBUB inapenda kutoa mapendekezo yafuatao kwa
Serikali, wadau mbali mbali na jamii kwa ujumla:
1.
Mamlaka zinazotoa haki kwa
wahanga wa ukatili, wakiwemo watoto zitoe haki kwa wakati kwa kuzingatia
maslahi mapana ya mtoto.
2.
Wadau wa haki za binadamu
waendelee kutoa elimu ya haki za binadamu kwa jamii ili kubadili mila na
tamaduni potofu pamoja na kukemea vitendo vya ukatili, unyanyasaji na
udhalilishaji wa watoto.
3.
Wazazi wawajibike katika
malezi ya watoto ili kuimarisha familia zao. Aidha, wahakikishe watoto wa
kike na wa kiume wanapatiwa fursa sawa ili ndoto zao katika maisha zifikiwe.
4.
Watoto wapatiwe elimu ya
afya ya uzazi ili waweze kujitambua na kuwa na uelewa juu ya madhara ya mimba
na ndoa za utotoni.
5.
Wadau mbalimbali wa haki za
watoto wahakikishe kuwa ulinzi, usalama na haki za mtoto zinaimarishwa na
kuhakikisha kuwa aina zote za ukatili na ubaguzi dhidi ya watoto zinatokomezwa.
Imetolewa na:
(SIGNED)
Mohamed Khamis Hamad
Makamu Mwenyekiti
TUME YA HAKI ZA BINADAMU NA UTAWALA
BORA
Juni 16, 2020
No comments:
Post a Comment