Na.Mwashungi Tahir -Maelezo 22/o6/2020.
Kamati tekelezaji ya Umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Amani wametakiwa kujitokeza kuchukuwa fomu za uongozi katika nafasi mbali mbali katika uchaguzi utakaofanyika Oktoba mwaka huu.
Hayo ameyasema Mwenyekiti wa umoja wa Wanawake Tanzania (UWT) Fatma Hamrani huko ofisini kwake wilaya ya Amani wakati alipokuwa akizungumza na kamati tekelezaji kuhusiana na uchukuaji wa fomu kwa nafasi mbali mbali za uongozi .
Amesema wanawake wasijiweke nyuma wasimame kidete katika kuchukua nafasi mbali mbali ikiwemo ubunge, uwakilishi na udiwani kwani hii ni demokrasia na kila mtu anayo haki ya kuchukuwa nafasi na kugombea wakati ukifika.
“Kinamama wenzangu tujitokezeni kwa wingi kuchukua fomu za nafasi mbali mbali kwani hii ni fursa adhimu na tusiiwachie”alisema Mwenyekiti huyo.
Pia aliwaasa akinamama kuhamasishana na kupeyana nguvu kwa kuweka mashirikiano pindi pale wanawake wanapojitokeza kutaka kuomba nafasi za uongozi katika ngazi mbali za chama na serekali.
Nae Kaimu Katibu wa Umoja wa wanawake Tanzania (UWT) Wilaya ya Amani Mwanamvua Mussa Chambo amewataka wanawake kuwa na hamasa kwa kuchukuwa fomu za uongozi katika majimbo pindi zitakapotoka ili waweze kuingia katika vyombo vya kutunga sheria .
“ Iwapo tutapata kushika nafasi za uongozi tutaweza kutoa maamuzi katika vyombo hivyo katika kujikwamua kwa kupambana na mfumo dume wa kiutawala na kupata maendeleo katika jamii”,alisema kaimu huyo.
Kwa upande wanawake hao wamesema wako tayari kuchukuwa fomu za nafasi za uongozi katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwezi wa Oktoba mwaka huu kwa ngazi mbali mbali pale muda utakapofika kwani kinamama wana mchango mkubwa katika kuleta maendeleo katika nchi.
No comments:
Post a Comment