Habari za Punde

Balozi Seif aipongeza kamati ya michezo ya ZBC kwa kusimamia mashindano ya Yamle Yamle Cup

 Mwanamichezo Maarufu Nchini Mohamed Raza  Kushoto akimkabidhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi na na baadae Mkurugenzi Mkuu wa ZBC Chande Omar Omar seti ya Jezi kwa Vijana wadogo wanaohudumia mashindano ya Yamle Yamle Cup hapo Vuga Mjini Zanzibar.
 Mkurugenzi wa Shirika la Utangazaji Zanzibar Chane Omar Omar akipokea moja ya seti ya Jezi zilizotolewa na Mfanyabiashara Mohamed Raza kwa washindi wa mashindano ya Yamle Yamle Cup.
 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Iddi kati kati akimkabidhi Kikombe  Mkurugenzi wa ZBC Chande Omar kitakachokuwa cha Mshindi wa kwanza wa fainali ya Mashindano ya Yamle Yamle Cup.
Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano ya Yamle Yamle Cup  Sadiq Ali Hamad {DJ Flash} akitoa shukrani kwa uongozi wa Serikali na Mwanamichezo Mohamed Raza kwa ushirikiano uliopelekea Yamle Yamle Cup kuzindi kuchanja mbuga.
Picha na – OMPR – ZNZ.

Na Othman Khamis, OMPR
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ameipongeza Kamati ya Michezo ya Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} inayosimamia Mashindano ya Yamle Yamle Cup kwa ufanisi mkubwa iliyopata katika kuendesha Mashindano hayo ndani ya Kipindi cha Miaka Miwili.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa pongezi hizo wakati wa hafla fupi ya kukabidhi Vifaa vya Michezo, Vikombe pamoja na nishani kwa Washindi wa Mashindano hayo vilivyotolewa na Mwanamichezo Maarufu akiwa pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya ZAT Mohamed Raza Hassanali hapo Aisini kwake Vuga Mjini Zanzibar.
Alisema wanamichezo na Wananchi wengi Nchini wameshuhudia jinsi mashindano hayo yalivyofanya vizuri chini ya Kamati ya mashindano hayo ikielewa kwamba Michezo hivi sasa ni ajira na sio burdani pekee.
Balozi Seif alieleza kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iliamua kuziboresha Studio za Redio na Tv za Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} baada ya kuelewa kazi kubwa inayofanywa na Watendaji wa Taasisi hiyo ya Habari ya kutoa Elimu, Burdani pamoja na Michezo.
Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa pongezi maalum kwa Mwanamichezo Maarufu Nchini Mohamed Raza kutokana na jitihada zake za kuunga mkono sekta ya Michezo Nchini iliyopata mafanikio makubwa.
Alisema Taifa linathamini mchango mkubwa wa Mwanamichezo huyo uliomuwezesha kupewa heshima ya kuwa Mshauri wa Rais aliyewahi kusimamia masuala ya Michezo Nchini.
Akitoa taarifa ya Mashindano hayo Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar Chande Omar Omar alisema mashindano ya Yamle Yamle yamebuniwa kutoa fursa kwa Wanamichezo Mitaani kuungana na kushiriki mashindano ili kuhamasisha Jamii kupenda kushiriki Michezo.
Chande alisema ZBC hivi sasa inaongoza katika kurusha vipindi kupitia Mitandao ya Kijamii katika urushaji wa vipindi na imepata nafasi ya Nne katika fani ya Habari kwa mujibu wa Utafiti uliofanywa na Wataalamu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam.
Alisema kutokana na kazi kubwa inayofanywa kupitia mashindano hayo  Yamle Yamle imepata umaarufu mkubwa kwenye sekta ya michezo ambayo Taifa linaweza kuitumia fursa hiyo kuwasilisha Ujumbe wake kwa Umma.
Mapema Mwanamichezo Maarufu Nchini Mohamed Raza Hassanali alisema ubunifu ulioonyeshwa na Watendaji wa ZBC kupitia Kamati iliyoundwa umeleta muamko na hatimae kuungwa mkono na wadau wa Michezo ndani nan je ya Nchi.
Raza alisema kwa vile michezo imo ndani ya damu yake amejitolea wakati wowote kuongeza nguvu zake katika kuona changamoto zinazojichomoza ndani ya maandalizi au mashindao hayo zinapatiwa ufumguzi mara moja.
Mwanamichezo huyo Nchini aliahidi kwamba kamwe hatovunjika moyo katika kusaidia harakati za Maendeleo ikiwemo Sekta ya Michezo ambayo amekuwa akiishabikia kila siku.
Katika hafla hiyo Mwanamichezo Mohamed Raza Hassanali amekabidhi Seti za Jezi kwa Vijana wadogo 17 wanaohudumia mashindano ya yamle yamle, Vikombe kwa Mshindi wa Kwanza na wapili vikiwa mali yao, zawadi kwa Mfungaji na Kipa bora,Mwanamichezo mwenye nidhamu pamoja naMedani za dhahabu na Shaba kwa washindi wa kwanza na Pili.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.