Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akizungumza wakati wa hafla ya maziko ya Rais Mstaaf wa Awamu ya Tatu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Benjamin William Mkapa, yaliofanyika Kijijini kwao Lupaso Mkoani Mtwara.

RAIS wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Ali Mohamed Shein, amesema kuwa Rais
Mstaafu wa Awamu ya Tatu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Bejamin William
Mkapa aliyahifadhi na kuyalida Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar ya mwaka 1964 kwa
vitendo.
Pia, Rais Dk. Shein aliongeza kuwa Marehemu mzee Mkapa aliuhifadhi
na kuulinda Muungano wa Tanganyika na Zanzibar kwa vitendo hivyo, ataendelea
kuheshimiwa kwa ari yake hiyo na uzalendo wake huo aliokuwa nao.
Rais Dk. Shein aliyasema hayo wakati akitoa salamu za wananchi wa
Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kufuatia kifo cha Marehemu Rais Bejamin
William Mkapa katika maziko yaliyofanyika huko kijijini kwake Lupaso, Mkoa wa
Mtwara, Wilaya ya Masasi.
Hivyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa wananchi wataendelea kumuenzi
na kumkumbuka Rais Mkapa katika maisha yao yote sambamba na kumuombea kwa
Mwenyezi Mungu.
“Takribani siku hizi sita zilizopita tulikuwa na majonzi makubwa
lakini hatukusikitika kwani ndio uwezo wa Mwenyezi Mungu, hivyo ni jukumu letu
kumuombea Mzee wetu huyu ili MwenyeziMungu amsamehe makosa yake na amjaalie
amuweke mahala pema”
“Mwenyezi Mungu atupe hatima njema ya maisha yetu hapa duniani
tukitimiza wajibu wetu katika kutekeleza majukumu yetu kama vile alivyofanya
kiongozi wetu huyu Rais Benjamin William Mkapa”, alisema Rais Dk. Shein.
Hivyo, Rais Dk. Shein alisema kuwa kwa majonzi makubwa wananchi wa
Zanzibar wanaungana na ndugu zao wote wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
wananchi wa Mkoa wa Mtwara na hasa Wilaya hiyo ya Masasi katika
maombolezo ya msiba huo mkubwa.
Aidha, Rais Dk. Shein alimtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania Dk. John Pombe Joseph Magufuli kupokea salamu hizo za wananchi wa
Zanzibar huku akisisitza kwamba safari hiyo ya umauti ni ya mwisho ambayo ni muhimu
na ya lazima kwa kila mwanaadamu.
Nao marais wastaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nyakati
tofauti walitoa salamu zao za mwisho kabla ya kuzikwa kwa Rais Mkapa na
walitumia fursa hiyo kumuelezea Rais Mkapa jinsi walivyomfahamu kwa miaka mingi
sambamba na utekelezaji wake wa kazi.
Rais Kikwete kwa upande wake alieleza kuwa Marehemu Mkapa alikuwa
ni kiongozi mtambuzi wa manufaa ya watu wake anaowaongoza ambaye amelifanyia
mengi taifa hili la Tanzania katika uongozi wake.
“Nafsi yangu kama zilivyo nafsi zenu imegubikwa kwa kuondokewa na
ndugu yetu, mwenzetu huyu Rais Mkapa…………sisi Waislamu tunahusia kwa kiongozi
wetu Bwana Muhammad (S.A.W) anasema kuwa
mwanaadamu kwa maumbile yake ni mkosaji na ndugu yetu ni mwanaadamu…”
“..............hivyo, huenda pengine katika umri wake amewahi
kuteleza akafanya kosa asilolitaka au asilolipenda Muumba wetu basi katika hali
kama hii mwenzetu akiondoka duniani basi ni vyema kumuombea msamaha kwa
Mwenyezi Mungu kwani hata baba yetu Adam alikosea”, alisema Rais Mstaafu Ali
Hassan Mwinyi.
Sambamba na hayo, Rais Mwinyi alisema kuwa Rais Mkapa alikuwa ni
mtu mzuri sana, mwema sana na mbaridi sana lakini alikuwa ni mfanya kazi kweli
kweli na alikuwa hana masihara katika kazi mambo ambayo yameleta manufaa kwa
Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliwashukuru viongozi wote
na wananchi pamoja na Kamati ya Kitaifa iliyoshughulikia vyema msiba huo huku
akimuelezea Rais Mkapa kuwa alipenda kwao na kuwataka Watanzania kujifunza jambo
hilo kwani Mzee Mkapa aliusia kuzikwa katika kijiji alichozaliwa cha Lupaso.
Nao
wanafamilia wa Marehemu Mzee Mkapa walitoa shukurani kwa wananchi na viongozi
wote pamoja na Serikali kwa kuujali na kuushughulikia msiba wa Rais Mkapa
ambapo maziko ya kiongozi huyo yalifanyika kwa taratibu zote za Kiserikali na
kidini.
Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment