Habari za Punde

NARCO yamsimamisha kazi Meneja West Kilimanjaro


Na Mwandishi Wetu,
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Ranchi ya Taifa (NARCO), Masele Mipawa amemsimamisha kazi Meneja wa Ranchi ya West Kilimanjaro iliyopo Arusha, Hezron Kyaruzi kwa tuhuma za kukosa uadilifu kwa mali za Umma na kusababisha upotevu wa Ng’ombe takriban 32.

Akiwa katika ziara ya kutembelea Ranchi hiyo ya West Kilimanjaro mwishoni mwa wiki (Julai 18, 2020), Mipawa alisema kuwa waliamua kufanya maamuzi hayo kufuatia changamoto nyingi zinazoikumba shamba hilo ambazo kwa kiasi kikubwa zimechangiwa na uongozi mbovu wa meneja huyo.

“Kutokana na upotevu wa Ng’ombe, uzembe na ukosefu wa maadili tumeamua kumsimamisha kazi  Meneja wa Ranchi na Msaidizi wake na  hatua nyingine za kisheria na kinidhamu zitafuata,”alisema Mipawa

Mipawa alisema ziara hiyo aliyoifanya katika Ranchi hiyo ni kufanya ukaguzi kutokana na taarifa walizokuwa wakizipata ambazo zilionesha kuwa katika shamba hilo kumetokea upotevu  wa Ng’ombe ambao Kampuni ya NARCO haina taarifa nao.

“Ziara hii imetusaidia kubaini kuwa kuna wizi uliokithiri katika shamba hili ambao umechangiwa na mahusiano mabovu kati ya Meneja na jamii inayozunguka shamba hili, ukosefu wa maadili na uadilifu wa Meneja ambao umepelekea  Ng’ombe 32 kupotea,”alisema

“Kati ya ng’ombe hao 32 waliopotea 15 wameshapatikana na wengine 17 hawajapatikana mpaka sasa huku ng’ombe wengine 27 walichinjwa bila kibali cha makao makuu,”alifafanua Mipawa

Kufuatia hali hiyo, Mipawa alisema wameamua pia kumsimamisha kazi Msaidizi wake kwa kuwa alishindwa kumshauri vizuri meneja huyo huku ikidaiwa alikuwa akishirikiana na meneja huyo kwenda kuazima ng’ombe kwa watu binafsi ili Ranchi hiyo ionekane ina idadi kubwa ya ng’ombe.

Aidha, Mipawa aliwataka wafanyakazi wengine waliobaki katika shamba hilo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, wazingatie nidhamu na uzalendo huku akiwaonya kuwa Serikali ya Awamu ya Tano haitavumilia mtu yeyote anayehujumu rasilimali za Taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.