Habari za Punde

NGOs ZATAKIWA KUENDESHA MIRADI YENYE TIJA

Wanufaika wa miradi ya kilimo na mifugo katika vijiji vya Kipanga na Ilogombe wakimsikiliza Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Dkt. Faustine Sambaiga katika kikao cha pamoja alipotembelea vijiji hivyo kukagua miradi inayotekelezwa na shirika la PELUM Tanzania.
 Picha zote Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

Na Mwandishi wetu Mufindi
Mwenyekiti wa Bodi ya Uratibu wa Mashirika yasiyo ya Kiserikali Dkt. Richard Sambaiga ameyataka Mashirika Yasiyo ya Kisrikali kuhakikisha miradi wanayoifanya inawaongezea tija wananchi badala na kufadhili miradi isiyoweza kusababisha maendeleo bayana kwa walengwa.

Dkt. Sambaiga ameyasema hayo Wilayani Mufindi, Iringa wakati akikagua utekelezaji wa miradi ya kilimo, ufugaji na mpango wa matumizi bora ya  ardhi inayofanywa na Shirika la PELUM Tanzania katika vijiji vya Kipanga na Lilongole.

"Kuna umuhimu kwa hawa wananchi wanaofanya kilimo au ufugaji  wafanye kwa namna ambayo itawaongezea tija, kuliko kuona wanatumia nguvu nyingi lakini tija kidogo" alisema Dkt. Sambaiga.

Amesisitiza mwenendo wa mashirika kuripoti kazi walizofanya na kufanikiwa, ziendane na kuongeza ufanisi katika utendaji kazi ili miradi hiyo iwe mfano na kuhamasisha wengine kujiunga.

"Tuongeze vipengele vya kuwezesha utaalamu wa kilimo na ufugaji uwe wa kisasa ili kuongeza tija na miradi hiyo iwe ni mfano"

Naye Msajili wa Mashirika yasiyo Ya Kiserikali,  Vickness Mayao ameyataka mashirika hayo kutoa taarifa mara kwa mara kwa wananchi kuhusu kazi zao na kuboresha majukumu wanayoyafanya.

"Bado tunahimiza mashirika kutekeleza majukumu yao kwenye eneo walilosajili, wanaweza kuongeza thamani ya miradi yao bila kuathiri lengo lao" amesema Mayao.

Akiwasilisha taarifa ya mradi huo, Mratibu wa shirika hilo Donati Senzia amesema, shirika kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi, inatarajia kupima mashamba zaidi ya 500 ili wananchi hao wapewe hati na ardhi ili kuwanufaisha kiuchumi.

"Tuliona kwenye mradi huu tusiishie tu kupima bali tuangalie ardhi itawanufaishaje wananchi kiuchumi hasa kwa akina mama" amesema Senzia.

Naye Afisa Ardhi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mufindi Simon Mbago amesema wanashirikiana na mashirika mbalimbali kuhakikisha wananchi wananufaika na ardhi kwa kuwapimia na kubainisha matumizi ya ardhi.

Baadhi ya wanufaika wa vijiji hivyo wameelezea kufurahishwa kwao na PELUM hususani kupata elimu ya kumiliki na kuitumia ardhi kwa manufaa na kupunguza migogoro ya ardhi kwa kiwango kikubwa.

Hata hivyo, wananchi wengi waliomba Serikali kwa kushirikiana na NGOs kuwasaidia kutatua kero ya Barabara na maji ili kuwawezesha kujikita katika Kilimo.

"Kipaumbele kwetu ni barabara kwani hata haya mazao hatuwezi kuyafikisha kwenye masoko barabara yetu inapitika katika msimu mmoja tu, wakati wa mvua hatuwezi kufika mjini", alisema mmoja wa wanakijiji.

Ziara ya ukaguzi wa kazi za Mashirika Yasiyo ya Kiserikali inakusudia katika kujirishisha dhidi ya taarifa za Mashirika zinazowasilishwa katika Ofisi ya Msajili, taarifa za wafadhili pamoja na kujiridhisha na thamani halisi ya fedha zilizotumika katika maeneo ya mradi.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.