RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la
Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein amewataka baadhi ya watu wakiwemo
vijana kutojiingiza katika vitendo vinavyoweza kuvunja amani na utulivu nchini
kwa kisingizio cha demokrasia na uchaguzi.
Dk. Shein aliyasema hayo katika ufunguzi wa Maonyesho
ya Nane Nane yaliyofanyika huko Chamanangwe, Wilaya ya Wete Mkoa wa Kaskazini
Pemba ambayo yalihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa vyama vya siasa na
Serikali akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd pamoja
na wananchi wengine.
Rais Dk. Shein alisema kuwa uzoefu unaonesha
kwamba baadhi ya watu na hasa vijana
hushawishiwa na watu wasio na nia njema na nchi yao, wajiingize katika vitendo
vinavyoweza kuvunja amani iliyopo.
Kwa kutilia mkazo jambo hilo la kuvunja amani kwa
kisingizio cha demokrasia Rais Dk. Shein alisisitiza kwamba taasisi ya haki ni
Mahakama Kuu pekee hivyo, mtu anapokosa
haki yake anatakiwa kufungua kesi kwa lengo la kudai haki yake
hiyo na sio kutoa kauli za uvunjifu wa amani.
Katika hotuba yake hiyo, Rais Dk. Shein alitumia
fursa hiyo kuwaasa vijana kama na kuwataka kuepuka kuingia katika mtego huo
kwani hali hiyo inaweza kuhatarisha amani pamoja na maisha yao.
“Nawambia vijana mti na macho, kwamza wafahamu
kwamba Zanzibar ni ya watu wote”alisisitiza Rais Dk. Shein.
Aidha, alieleza kuwa vyombo vya ulinzi vipo imara
katika kukabiliana na mtu yoyote mwenye lengo la kutaka kuvunja amani kabla ya
uchaguzi, wakati wa uchaguzi na baada ya uchaguzi.
“Hakuna mtu anaeweza kuja kuwatisha watu wa
Zanzibar, watu wa Zanzibar wako huru katika nchi yao wamekombolewa na Mapinduzi
ya Januari 12, mwaka 1964, wasitikishe kibiriti, hii serikali kama zilivyo
serikali nyengine………..nawataka wananchi wajue kwamba kuna maisha baada ya
uchaguzi”,alisisitiza Dk. Shein.
Rais Dk. Shein alieleza kwamba siasa ya mfumo wa
vyama vingi haikuja kwa lengo la watu
kugombana kwa sababu ya siasa hivyo, aliwasisitiza vijana wanaoshawishiwa
sambamba na kutengenezewa mazingira ya kuvunja amani wajue kwamba Zanzibar ni ya watu wote na wote
wanailinda.
Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kwamba
wananchi wanahitaji kuendelea na maisha yao na kuzidi kupiga hatua za maendeleo
kwa kuleta ustawi wa maisha katika jamii.
Hivyo, alisisitiza kwamba msingi muhimu wa
kuiendeleza dhamira hio ni kudumisha amani, utulivu, umoja, mapenzi na
mshikamano uliopo hapa nchini.
Rais Dk. Shein alieleza kuwa ni rahisi sana
kuivunja amani lakini si rahisi kuirejesha amani huku akieleza kuwa Zanzibar na
Tanzania nzima kwa jumla ziko salama na
katika kipindi chote hichi kila mmoja anafanya kazi zake, anatembea usiku na
mchana na analala vizuri bila ya hofu wala woga.
Rais Dk. Shein
alisema kuwa mafanikio yanayoendelea kupatikana katika utekelezaji wa
mipango ya mandeleo yakiwemo ya sekta ya kilimo, yanatokana na kuendelea kuwepo
kwa hali ya amani na utulivu.
Alieleza kuwa katika hotuba zake mbali mbali
amekuwa akisisitiza umuhimu wa kuitunza, kuilinda na kuiendeleza amani iliyopo
pamoja na kuwataka wananchi kujiepusha na vitendo vyote vinavyoweza kusababisha
kuvunjika kwa amani iliyopo.
Aliipongeza Wizara ya Kilimo, Maliasili, Mifugo na
Uvuvi kwa ubunifu wa kaulimbiu ya maonyesho ya mwaka huu isemayo “Tudumishe
amani na utulivu kwa maendeleo ya sekta ya kilimo nchini” huku akiendelea
kusisitiza uimarishaji amani na utulivu nchini.
Aliongeza kuwa kauli mbiu hiyo ni muhimu wakati
huu ambapo nchi inaelekea katika kufanya uchaguzi mkuu katika mwezi wa Oktoba
mwaka huu.
Rajab Mkasaba, Ikulu
Zanzibar
Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax:
024 2231822
E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk
No comments:
Post a Comment