Habari za Punde

HUDUMA ZA USTAWI WA JAMII NCHINI KUIMARISHWA

Katibu Mkuu Wizara ya Afya – Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu (wa tatu kutoka kulia) akikata utepe katika moja ya miongozo saba kuashiria kuzindua miongozo hiyo yenye lengo la kuimarisha huduma za Ustawi wa Jamii nchini.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya – Idara kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akionesha moja ya miongozo saba iliyozinduliwa yenye lengo la kuimarisha huduma za ustawi wa Jamii nchini. Kulia ni mwakilishi wa shirika la IOM Dkt. Qasim Sufi, Kushoto ni Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ngóndi.
Picha zote na kitengo cha mawasiliano serikalini WAMJW

Na.Magie Nkulu  

Serikali kupitia Wizara ya Afya – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii imezindua miongozo saba yenye lengo la kuimarisha huduma za Ustawi wa Jamii nchini.
Akizindua miongozo hiyo jijini Dodoma Katibu Mkuu Wizara ya Afya – Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amesema moja ya jitihada za kuimarisha Huduma za Ustawi wa Jamii ni kutengeneza miongozo hiyo ikiwa ni sehemu ya kuboresha huduma za ustawi nchini.
“Lengo letu kubwa ni huduma za Ustawi wa Jamii ziendelee kuimarika siku hadi siku, utengenezaji wa miongozo hii ni moja ya jitihada” amesema Jingu.
Ameongeza pia kuwa, Serikali imefanya mambo mengi  katika kuimarisha huduma za Ustawi hususani kwa watoto, wazee, akina mama na wahanga wa ukatili hivyo miongozo hiyo inaboresha zaidi huduma hizo kufanyika ikiwemo mwongozo wa kuwaelekeza wanaotaka kuanzisha makazi salama, mwongozo wawakilishi wa watoto mahakamani Pamoja na program za kijamii za marekebisho ya tabia kwa Watoto wanaokinzana na sheria.
Miongozo mingine ni wa kuwaunganisha Watoto na familia zao, mwongozo wa utambuzi wa huduma kwa Watoto walio katika mazingira hatarishi, mwongozo wa uanzishaji wa makazi ya wazee na wasiojiweza Pamoja na mwongozo wa majukumu ya Maafisa Ustawi wa Jamii katika Mamlaka za Serikali za Mitaa.
Awali akimkaribisha Katibu Mkuu kuzindua miongozo hiyo, Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Naftali Ng’óndi amesema kwa ujumla miongozo hiyo inalenga kuboresha, kuweka taratibu na vigezo vya kutoa huduma za Ustawi kisayansi kwani katika utengenezaji wake umefanyika utafiti mkubwa wa ndani na nje ya nchi.
Naye Mkurugenzi wa Idara ya Afya, Ustawi wa Jamii na Lishe kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI Dkt. Rasheed Maftaha amesema Halmashauri zinahitaji miongozo ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi kwa kuzingatia viwango.
“Tunaahidi miongozo hii tutaisimamia ipasavyo inatekelezwa kama ilivyokusudiwa.” Alisema Maftaha.
Mwakilishi wa shirika la IOM linalojihusisha na kuhifadhi wahanga wa ukatili na usafirishaji haramu Dkt. Qasim Sufi amesema miongozo hii ya Taifa inakwenda sambamba na mpango wa Taifa wa kutokomeza ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Pamoja na mpango wa kupambana na usafirishaji haramu wa binadamu.
Inakusudia pia kusaidia jitihada za Serikali katika kukuza uwezo wa kupanga, kutekeleza na kusimamia mikakati na huduma katika kupambana na unyanyasaji wa wanawake na Watoto.
Wakati huo huo, Dkt. Jingu amezindua muundo wa Utumishi wa kada ya Maafisa Ustawi wa Jamii wenye lengo la kubainisha majukumu ya Maafisa Ustawi wa Jamii ili kuondoa mkanganyiko na kada nyingine.
Muundo huo pia unalenga kusaidia vyuo vinavyotoa taaluma ambazo ni muhimu katika fani za Ustawi wa Jamii kuweza kuimarisha Mitaala yao ili kutambua ni watu gani wanahitajika katika kada ya ustawi wa jamii, ikiwemo kuongeza sifa za watu wanaostahili kuajiriwa kama Maafisa Ustawi wa Jamii.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.