Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein Ameweka Jiwe la Msingi Eneo la Ujenzi wa Viwanda na Kiwanda Cha Mwani Chamanangwe Pemba.

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Ali Mohamed Shein, akipata maelezo ya ramani ya eneo ambalo linatarajiwa kujengwa Viwanda mbalimbali katika eneo la Chamangwana Pemba wakati wa hafla ya uwekaji wa Jiwe la Msingi (kushoto kwa Rais)  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Balozi Seif Ali Iddi na (kulia kwa Rais) Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar Mhe.Balozi Amina Salum Ali, wakimsiliza Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Viwanda Zanzibar Dkt.Abdalla Rashid. akitoma maelezo ya eneo ambalo litajengwa viwanda


SERIKALI ya Awamu ya Saba na ile ijayo imedhamiria kwa makusudi kuimarisha uchumi wa viwanda hapa nchini kwa kutenga eneo la viwanda pamoja na kuanzisha kiwanda cha Mwani huko Chamanangwe Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein aliyasema hayo katika hotuba yake aliyoitoa mara baada ya kuweka jiwe la Msingi la uzinduzi wa eneo la Viwanda pamoja na kuweka jiwe la Msingi la Kiwanda cha Mwani huko Chamanangwe Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Katika hotuba yake hiyo, Dk. Shein alisema kuwa katika mikutano ya Kampeni za Chama Cha Mapinduzi (CCM) zinazoendelea mgombea nafasi ya Urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho Dk. Hussein Ali Mwinyi amekuwa akieleza azma ya Serikali ya Awamu ya Nane ya kuimarisha uchumi wa bluu ikiwemo kuimarisha viwanda.

Rais Dk. Shein alieleza kuwa hatua hiyo inaonesha wazi juhudi za Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuanza kutekeleza kwa vitendo katika kupunguza tatizo la ajira kwa kuendeleza viwanda.

Aliongeza kuwa eneo la Chamanangwe limeteuliwa kuwa eneo maalum kwa ajili ya ujenzi wa viwanda ili kuchochea ukuaji wa uchumi hapa nchini na kueleza kuwa kiwanda kitakachojengwa mwanzo ambacho kimezinduliwa ni kiwanda cha kusarifu zao la mwani.

Alisema kuwa malengo la kuendeleza viwanda yanaendana na malengo ya Mapinduzi Matukufu ya Januari 12,1964 ya kujenga uchumi endelevu kwa kuanzisha viwanda na kukuza sekta ya kilimo hapa nchini.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kutoa historia ya viwanda hapa Zanzibar na kusema kuwa suala la viwanda hapa nchini ni suala la zamani kabla na baada ya Mapinduzi ya Januari 12, 1964 ambapo alisema kuwa Zanzibar ilikuwa na viwanda vingi vidogo vidogo Unguja na Pemba.

Alisema kuwa kabla ya Mapinduzi viwanda vilikuwepo lakini hapakuwa na kiwanda hata kimoja kilichomilikiwa na Mzawa hali ambayo ilikuja kubadilika mara baada ya Mapinduzi  hayo kwa kutoa fursa ya kuanzishwa viwanda katika maeneo kadhaa likiwemo eneo la vidogo vidogo Amani, kiwanda cha matrekta Mbweni na vyenginevyo.

Pia, aliongeza kuwa hivi sasa kumekuwepo viwanda kadhaa vinavyomilikiwa na wazalendo na kila mwenye uwezo amekuwa akianzisha kiwanda akitakacho hapa Zanzibar.

Rais Dk. Shein alitumia fursa hiyo kulibariki kwa kulipa jina eneo hilo na kulitaja kuwa eneo la Chamanangwe ya Kilimo itakuwa ni Chamangwe moja na eneo la viwanda litakuwa ni eneo la Pili huku akisisitiza kuwa Chamanangwe itabadilika na itavutia.

Aliongeza kuwa ujenzi katika eneo hilo utaendelea hadi miaka ijayo na kueleza kuwa kiasi cha TZS Bilioni 7.5 zimetolewa na Mashirika ya Serikali ya Zanzibar likiwemo ZSTC, Benki ya (PBZ), ZSSF, BIMA pamoja na Shirika la Bandari kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda hicho cha mwani ambacho ujenzi wake unatarajiwa kuanza hivi karibuni.

Alisema kuwa sekta binafsi zitazidi kuhamasishwa ili kuunga mkono juhudi za Serikali za kuanzisha viwanda katika eneo hilo na maeneo mengine hapa nchini.

Kadhalika, Rais Dk. Shein alisema kuwa Shirika la Biashara la Taifa (ZSTC) hivi sasa limekuwa likinunua mwani kwa wananchi  kwa lengo  ya kuepuka hilba wanayofanyiwa wananchi kutoka kwa baadhi ya Kampuni zinazonunua mwani kwa kuwapa wakulima pesa ndogo.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Shein alieleza kuwa mafanikio hayo yanatokana na ziara yake aliyoifanya nchini Indonesia akiwa ameambatana na viongozi kadhaa akiwemo Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali na kumpongeza kwa hatua hio.

Nae Waziri wa Biashara na Viwanda Balozi Amina Salum Ali alisema kuwa eneo hilo la Chamanangwe ambalo lilitengwa maalum kwa ujenzi wa viwanda lina ukubwa wa hekta 55.37.

Alisema kuwa eneo hilo limetengwa kwa ajili ya viwanda, hifadhi, maduka makubwa, eneo la kilimo cha mbogamboga na matunda, eneo la vyuo vya amali, huduma za jamii kama vile kituo cha afya, msikiti, michezo, migahawa, eneo la ghala, makaazi ya watu pamoja na huduma za zimamoto, ulinzi, taasisi za kusimamia ubora wa bidha ana nyenginezo.

Alieleza kwua hafa ya uwekaji wa jiwe la msingi la kiwanda cha mwani inadhihirisha azma ya Serikali ya kuelekea kwenye uchumi wa buluu na kusisitiza kuwa Chamanangwe itakuwa ni kituo kikubwa hapa Zanzibar kwa kusindika matunda, mbongamboga na viungo ambazo zina soko kubwa sana katika nchi za SADC, Asia na Marekani.

Alisema kuwa ujenzi huo utakapokamilika sekta ya mwanin pekee itazalisha zaidi ya ajira 100,000 katika mnyororo mzima wa kuongeza thamani kutokana na mahitaji makubwa ya karagina katika soko la ndani na masoko ya nje kwa sababu ya umuhimu wake katika viwanda vya vyakula vya binaadamu na wanyama, viwanda vya dawa na vipodozi pamoja na kutengeneza rangi za kupaka katika majengo.

Mapema Katibu Mkuu wa Wizara ya Biashara na Viwanda Juma Hassan Reli alisema kuwa eneo la Chamanangwe linahusisha shehia ya Mchangamdogo, Kiuyu Minungwini pamoja na Kambini ambapo jumla ya TZS Milioni 332,346,630 zimelipwa kwa wakaazi wa Shehia ya Mchanga Mdogo na Kiuyu Minungwini kati ya pesa hizo TZS 251,000,000 zimetolewa kwa wenye mashamba na TZS 81,346,630 zimetolewa kwa wenye mabomba ambayo yalikuwa katika hatua mbali mbali za ujenzi.

Katibu Mkuu huyo aliipongeza Kampuni ya Ujenzi ya Serikali iliyofanya kazi kwa kasi, bidii na gharama nafuu hasa ikifikiriwa kuwa Kampuni hiyo imeanzishwa hivi karibuni.

Viongozi mbali mbali wa siasa na Serikali pamoja na wananchi wa Mkoa wa Kaskazini na Kusini Pemba  walihudhuria katika hafla hiyo akiwemo Makamo wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Idd.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.