Na Immaculate Makilika- MAELEZO
Serikali kupitia Balozi
wa Tanzania nchini Ubeligiji na Mwakilishi wa Tanzania katika Umoja wa Ulaya imesema
kuwa Bunge la Umoja wa Ulaya halijatoa azimio lolote kuhusu Tanzania kupitia
kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Bunge hilo.
Akizungumza mapema leo kupitia
televisheni ya Taifa (TBC), Balozi wa Tanzania nchini Ubeligiji na Mwakilishi wa Tanzania katika
Umoja wa Ulaya Jestus Nyamanga alisema kuwa kuna taarifa za upotoshaji na
zisizo na ukweli wowote zinazosambazwa
kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii
zikidai kuwa Bunge la Umoja wa Ulaya jana Novemba 19 limeazimia kusitisha
misaada na mikopo kutoka umoja huo na mashirika yake, kwa nchi ya Tanzania
sambamba na kuiwekea vikwazo.
Halikadhalika taarifa hizo
za upotoshaji zinadai kwamba Bunge hilo la Umoja wa Ulaya limeazimia kuiwekeza
vikwazo Tanzania na kuzuia kuuza bidhaa zake katika nchi za Umoja wa Ulaya.
“Novemba 19 asubuhi hapa
Ubeligiji, Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje ya Umoja wa Ulaya ilikutana katika
kikao chake cha kawaida, moja ya masuala yaliyojadiliwa ilihusu Tanzania na
hali ilivyo baada ya Uchaguzi Mkuu kukamilika, huu ni utaratibu wa kawaida kabisa wa Kamati hiyo kuijadili
nchi ambayo ni mdau wao mkubwa wa maendeleo mara tu baada ya Uchaguzi Mkuu
kukamilika”, alisema Balozi Nyamanga
Balozi Nyamanga
alifafanua kuwa kikao hicho ni kikao cha Kamati ya Bunge ya Mambo ya Nje na si
Bunge lote na hata hivyo kikao hicho kilitoa nafasi kwa wabunge kutoa mawazo
yao na kujadili kuhusu hali ya Tanzania baada ya Uchaguzi Mkuu ambapo ni wabunge watano tu
ndio walitoa mawazo yao kati ya wabunge 71 wa Kamati hiyo. Ambapo hilo lina
idadi ya wabunge 705 na hivyo halijatoa azimio lolote kuhusu
Tanzania.
Alibainisha kuwa pia kuna taarifa ambazo si za kweli zinazoenezwa
na watu wenye nia mbaya na Tanzania
zikidai kwamba Bunge hilo la Umoja wa Ulaya limeazimia kuifutia Tanzania msaada wa euro milioni 626 ambazo Tanzania
inapewa na Umoja wa Ulaya kila mwaka, si kweli kwamba Umoja huo unaipa Tanzania
fedha hizo kwa ajili ya utekelezaji wa miradi. Aidha Serikali inaendelea
kutekeleza miradi yake mbalimbali.
“Hakuna mjadala wala
majadiliano yanayoendelea katika Umoja wa Ulaya wala hakuna azimio lililowekwa na Kamati hiyo ya Bunge,
wala kuizuia Tanzania kuuza bidhaa zake katika nchi hizo za Umoja wa Ulaya, hata
hivyo naomba niwahakikishie watanzania wenzangu kwamba uhusiano wa Tanzania na
Umoja wa Ulaya ni mzuri sana kwa zaidi ya miaka 45 sasa na tunaendelea
kushirikiana katika masula mbalimbali
yanayohusu maendeleo kwa pande zote mbili”, alisema Balozi Nyamanga.
No comments:
Post a Comment