Habari za Punde

Hafla ya Kuapishwa Kwa Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt. John Pombe Magufuli Jijini Dodoma Jana 5/11/2020.

 


Dk. John Pombe Joseph Magufuli ameapishwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kipindi cha pili katika Awamu ya Tano ya uongozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi Mkuu uliofanyika hivi karibuni nchini Tanzania.

Rais Magufuli ameapishwa katika Sherehe zilizofanyika kwa mara ya kwanza Jijini Dodoma katika uwanja wa Jamhuri ilihudhuriwa na viongozi mbali mbali wa Kitaifa na Kimataifa pamoja na Maelfu ya wananchi kutoka sehemu mbali mbali ndani ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sherehe hizo zimehudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi pamoja na baadhi ya Marais wa nchi za Afrika akiwemo Rais Yoweri Mussein Rais wa Uganda, Azali Ossoumani Boinakheir  Rais wa Muungano wa Visiwa vya Comoro, Rais wa Zimbabwe Emmerson Mnangagwa pamoja na viongozi wengine waliowawakilisha Marais wao, Mabalozi na wakuu wa Taasisi za Kimataifa.

Katika hotuba yake ya salamu alisema kuwa uchaguzi sasa umekwisha na jukumu kubwa na muhimu lililopo mbele ni kuendeleza jitihada za kuijenga na  kuleta maendeleo kwa Taifa la Tanzania na kueleza kuwa kiapo alichoapa yeye pamoja na Makamo wake wa Rais Mama Samia Suluhu Hassan watahakikisha wanakienzi kwa nguvu zote

Alieleza kuwa bila ya kujali tofauti za kiitikadi, dini, kabila ama rangi atashirikiana na watu wote katika kuhakikisha yale yote aliyoyaahidi katika Kampeni yanatekelezwa ikiwa ni pamoja  kuilinda na kudumisha amani na usalama wa nchi, uhuru wa nchi na mipaka yake pamoja na Muungano na Mapinduzi matukufu ya Zanzibar ya Januari 12, 1964.

Aliongeza kuwa jitihada za kujikomboa na kujenga Taifa linalojitegemea na kulenga kukamilisha miradi mikubwa iliyoanzishwa na ile mipya pamoja na kuimarisha usimamizi wa maliasili zikiwemo rasilimali kama bahari, madini mifugo na kadhalika pamoja na kukuza uchumi na kushuhulikia changamoto za umasikini pamoja na kero zinazowakabili wananchi. Pia mapambano dhidi ya rushwa nayo yataendelea na yale wizi na ubadhirifu wa mali ya uma.

Rais Magufuli alikishukuru chama chake cha CCM, wanachama wake na viongozi wake wote kaunzia Shina hadi Taifa, aliwashukuru wasanii kwa kuiombe kura CCM nchi nzima na kupelekea chama hicho kupata ushindi wa kiishindo.

Aliwashukuru wagombea wenzake wote wa Urais na wale wagombea wenza kwa kushiriki vizuri wagombea, aliishukurukamatiya maandalizi kutokana na watu kujaa ndani na nje ya uwanja na kusema kuwa hali hiyo inampa chamgamoto katika Serikali yake mpya na kitu cha kwanza ni kuanza kujenga uwanja mkubwa sana hapo Dodoma ili sherehe nyengine zitakapokuja watu wote waingie kwenye uwanja huo mpya.

Pia, alitumia fursa hiyo kutoa shukurani na kuvipongezwa vyombo vya habari kwa kufanya kazi kwa uweledi na uzalendo mkubwa tangu kuanza kwa kampeni hadi hivi leo zinapokamilika shughuli za uchaguzi pamoja na kuwapongeza Wabunge na Madiwani wote hasa kutokana na mwaka huu wengi wao kutoka CCM

Rais Magufuli alitoa pongezi za pekee kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi kwa kupata kura nyingi na kuzisha uchaguzi wa Zanzibar pamoja na kuwapongeza Wawakilishi.

Pia, aliwaahidi wananchi wa Dodoma kuzifanyia kazi ahadi zote alizozitoa wakati wa Kampeni katika mkoa huo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa barabara za kulizunguka Jiji hilo.

Katika hotuba yake hiyo Rais Magufuli aliwapongeza wananchi wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kusema kuwa ushindi aliopata ni ushindi wa wananchi wote na si wa wanaCCM peke yao.

Alisema kuwa tarehe 5 Nombemba mwaka 2015 aliapishwa na leo tarehe 5 Novemba ameapishwa tena kwa miaka mitano mengine jambo ambalo ni tofauti na 2015 ambapo aliapishwa Jijini Dar es Salaam lakini mara hii ameapishwa Dodoma na kuwa Rais wa kwanza kuapishwa katika jiji hilo.

Alitoa pongezi kwa Tume ya Uchaguzi, viongozi wa dini, vyombo vya Ulinzi na Usalama na kupelekea amani na usalama  kutawala katika kipindi cha uchaguzi na kuwapongeza Wataznania kwa kuonesha utulivu mkubwa katika kipindi chote cha uchaguzi kwani baadhi ya nchi uchaguzi ni chanzo cha migogoro na vita lakini kwa Watanzania wamevuka salama na kuuthibitishia ulimwengu kuwa Watanzania ni wapenda amani na wamekomaa kidemokrasia.

Alisema kuwa hatua hiyo inaonesha wazi kwamba Mwenyezi Mungu anaipenda Tanzania na kueleza kuwa tangu kupatikana uhuru Tanzania imepita katika mitihani mingi lakini imevuka salama ikiwa ni pamoja na kukingwa na janga la Corona.

Aidha, aliwashukuru viongozi wa Mataifa mbalimbali waliokuja kuungana na Watazania katika sherehe hizo wakiwemo Marais, Makamo wa Rais, Mawaziri mablimbali, Mabalozi pamoja na Wawakilishi wa Taasisi za Kimataifa wakiwemo EAC, SADC na Umoja wa Afrika pamoja na wale waliotuma salamu za pongezi kutoka Mataifa mbalimbali.

Alisema kuwa salamu hizo zinatoa nguvu ya kuwatumikia wananchi vizuri pamoja na kukuza ushinrikiano wa nchi hizo pamoja na Taasisi wanazoziwakilisha.

Alipokea salamu za heshima  na kupigwa wimbo wa Taifa, Wimbo wa Afrika Mashariki pamoja na mizinga 21 ilipigwa  ambapo Rais pia alipata fursa ya kukagua gwaaride  likiwa katika umbo la kawaida.

Akitoa salamu kwa niaba ya wananchi wa Uganda, Rais wa Uganda, Yoweri Kaguta Museven alitoa pongezi kwa Rais Magufuli pamoja na CCM na Watazania wote kwa ushindi ambao ni wa amani huku akiipongeza Tanzania kwa kuingia katika uchumi wa Kati.

Aidha, Rais Museven alisisitiza haja ya kufuatwa nyayo za waasisi wa Mataifa ya Afrika waliopigania uhuru na kuupongeza mwelekeo wa CCM kisiasa.

Kiongozi huyo wa Uganda alipongeza juhudi zilizochukuliwa na Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na  viongozi wenziwe waasisi wa Afrika kwa kujenga umoja na mshikamano na uongozi thabiti ambao uliwapelekea kufauli na kuondokana na ukoloni.

Aliipongeza CCM kwa kupata kura za juu ambapo aliweza kushuhudia ushindi huo kupitia televisheni ya TBC na kuonesha ushindi hasa katika Jimbo la Hai, Newala na mengineyo.

Aliwataka vijana kufuata msimamo wa Waasisi Wazalendo walioongozwa na Mwalimu Nyerere ambapo yeye amekuwa mfuasi wa Mwalimu Nyerere kwa muda wa miaka 57 hivi sasa  na kuyataja mabo yaliyopewa kipaumbele ikiwa ni pamoja na ukombozi wa Afrika yote, ustawi kwa kuzalisha mali sambamba na kuimarisha huduma,usalama na udugu.

Nao Marais wa Comoro, Zimbabwe na viongozi wengine walitoa pongezi wka Rais Magufuli kwa ushindi alioupata pamoja na kuwashukuru wananchi wa Tanzania kwa kuendeleza amani na utulivu hasa ikizingatiwa kwaba nchi zote hizo Jamhuriya Muungano wa Tanzania imechangia kwa kiasi kikubwa katika kupata uhuru wao.  

Mapema bendera ya Rais iliteremshwa  huku Rais akiangalia na wimbo wa “Retreat” kupigwa na baadae alikula kiapo na kusaini hati ya uapisho yeye pamoja na Makamo wake Mama Samia Suluhu Hassan  na baadae Rais alikabidhiwa ngao na mkuki.

Dua na sala zilizomwa na viongozi wa dini  na baadae Rais alielekea kwenye jukwa maalum na kupokea saluti pamoja na salamu ya heshima , salamu za rais, wimbo wa taifa, wimbo wa Afrika Mashariki na mizinga 21 ilipigwa, bendera ya Rais ilipandishwa  na gwaride liliunda umbo la “Alpha” na baadae Rais alilikagua  gwaride ambapo pia, gwaride la nje lilipita mbele ya Rais na kutoa heshima.

Katika sherehe hizo vikundi mbali mbali vya sanaa viliburudisha kikiwemo kikundi cha utamaduni kutoka Zanzibar pamoja na burudani za wasanii maarufu wa nyimbo za Bongoflava na kwaya kutoka Chuo cha Utumishi wa Umma.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.