Habari za Punde

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed ayafunga Maonyesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania Jijini Dar es salaam

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla akipokewa na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania {TANTRADE} Nd. Edwin  Rutageuka alipofika kufunga Maonyesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania Jijini Dar es salaam.
Mh. Hemed Suleiman akiridhika na kiwango cha Mpira kilichotengenezwa Nchini Tanzania baada ya kupata maelezo ya kina kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania {TANTRADE} Nd. Edwin  Rutageuka.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar MheshimiwA Hemed Suleiman Abdulla akiyafunga Rasmi Maonyesho ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania kwenye Ukumbi wa Mikutano ndani ya eneo hilo la Maonyesho jijini Dar es salaam.
Mjasiri amali mwenye ulemavu wa Macho Bwana Nyangalio Abdulla Nyangalio akimkaribisha Mh. Hemed Suleiman kwenye banda la Taasisi yake inayotoa mafunzo ya Ufundi Charahani .

 Kamanda wa Kitengo ya Ufundi cha Suma JKT Meja Peter Sebyiga akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman juu ya harakati zao za uzalishaji wa bidhaa mbali mbali zinazouzwa katika Vikosi tofauti vya Ulinzi Nchini.

Picha na – OMPR – ZNZ.


Na Othman Khamis, OMPR

Watanzania wanapaswa kujenga Utamaduni wa kununua Bidhaa zinazozalishwa na Viwanda vilivyopo Nchini ili kukuza Mapato ya Taifa, kuongeza ajira hasa kwa Vijana  kupitia Sekta mbali mbali  za uzalishaji ambazo ni kiungo muhimu katika maendeleo ya Viwanda.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Hemed Suleiman Abdulla alitoa kauli hiyo wakati akiyafunga Maonyesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yaliyokuwa yakifanyika katika Uwanja wa Maonyesho wa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere Jijijini Dar es salaam.

Alisema mwenendo wa Biashara Nchini Tanzania ulipata mtetereka kidogo kutokana na utegemezi wa baadhi ya bidhaa kutoka  Mataifa ya Viwanda kusita kuingizwa Nchini kwa sababu ya Mataifa hayo kuwekewa Karantini baada ya kuibuka kwa maradhi yanayosababishwa na virusi vya Corona { Cavid – 19 }.

Mh. Hemed aliwashauri Watanzania hasa Wahandisi na Wataalamu wa Sekta ya Viwanda kulichukulia suala hili ya Mripuko wa Virusi vya Corona  kama ni fundisho kwa kuzidisha kasi ya Uzalishaji wa bidhaa  ambazo zitapaswa soko lake Kuu na muhimu litumike hapa Nchini.

Alisema wazalishaji lazima waanze kutengeneza na kuimarisha mifumo ya ndani kwanza ikiwemo ya uzalishaji na usambazaji bidhaa zinazozalishwa na Viwanda vyote na ziada itakayopatikana ndio inaweza kuuzwa nje.

“ Soko imara la ndani litaweza kujenga misingi imara ya ushindani katika masoko ya Kikanda na Kimataifa”. Alisisitiza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar.

Mheshimiwa Hemed alieleza kwamba ni jambo la kutia moyo kuona takriban Viwanda elfu 8,477 vilivyoanzishwa ndani ya kipindi cha Miaka Mitano iliyopita tokea 2015 vinatumia Mali ghafi za ndani.

Alisema uzoefu unaonyesha  kuwa Nchi nyingi zilizoendelea Duniani katika Sekta ya Viwanda  mfano China zilianza kutengeneza mazingira ya ndani kwanza ambapo asilimia 80% ya bidhaa zinazozalishwa hutumika ndani na ile iliyobakia ya asilimia 20%  ndio inayosafirishwa nje ya Nchi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa wito kwa Wananchi na wadau wote  kuunga mkono jitihada kubwa zilizochukuliwa na Serikali zote mbili Nchini Tanzania Bara na Zanzibar katika kujiimarisha kwenye kukuza Uchumi wa Viwanda.

Alisema jitihada hizo zilizofanywa na Serikali ndani ya kipindi kifupi  ndizo zilizoipaisha Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania kuingia katika Uchumi wa Kati na hatimae kutangazwa rasmi na Benki ya Dunia mnamo Mwezi Julai Mwaka 2020.

Akizungumzia viwanda vodogo vidogo na Biashara ndogo ndogo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mheshimiwa Hemed Suleiman alisema Sekta hiyo inaendelea kutoa mchango mkubwa katika pato la Taifa kwa wastani wa asilimia 35% kila Mwaka.

Alisema hayo ni mafanikio makubwa yaliyopatikana na Serikali kupitia Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015/2020 katika kuinua kipato cha Wananchi wanyonge  sambamba na kupunguza tatizo la ukosefu wa fursa za ajira.

Mheshimiwa Hemed alibainisha kwamba  Serikali itaendelea kuenzi na kukuza juhudi hizo ili kuviwezesha  Viwanda vidogo vidogo  na vya Kati kukua na kufanya Kazi kwa tija zaidi kasi itakayoendelezwa ndani ya miaka Mitano ijayo kwa kuimarishwa vipaumbele  vyengine katika Sekta Binafsi itakayoleta ushindani wa soko.

Alifahamisha kwamba ili kuimarisha Sekta hiyo katika kutoa mchango wa Maendeleo kwenye Sekta ya Viwanda, ameziomba Benki pamoja na Taasisi za Kifedha Nchini ziangalie jinsi ya kutoa huduma za mikopo Rafiki ili kuwezesha ukuaji wa Viwanda hivyo.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alieleza kwamba Benki na Taasisi hizo za Kifedha ni vyema zikafikiria pia kuwa na huduma maalum ya kuendeleza viwanda Vidogo vidogo  na vya Kati vitakavyoweza kuratibiwa katika Maeneo mbali mbali Nchini.

Alisema Serikali zote tayari zimejiwekea malengo ya kuondoa usumbufu na urasimu katika ngazi zote ili kuweka mazingira itakayovutia uzalishaji na Uwekezaji kutoka ndani na nje waliowekewa milango wazi.

Halkadhalika Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla aliwashauri na kuwaomba Wadau wa Sekta ya Viwanda Wazalendo Nchini  kuitumia fursa ya Uwekezaji wa Miradi ya Kiuchumi na Biashara iliyowekwa na kutangazwa Visiwani Zanzibar.

Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu na Nane imeshajiweka tayari kushirikiana kwa karibu na Wafanyabiashara na Wawekezaji watakaoonyesha nia ya kutaka kuitumia fursa hiyo muhimu katika kuendeleza Sekta ya Viwanda Zanzibar.

Mapema Mkurugenzi Mkuu Wa Mamlaka ya Maendeleo ya Baishara Tanzania Nd. Edwin Rutageuka  alisema Maonyesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania yanaendelea kupata umaarufu  na mafanikio makubwa yaliyopelekea ongezeko la washiriki 595 Tanzania Bara na Zanzibar kwa Mwaka 2020 ikilinganishwa na washiriki 472 pale yalipoanzishwa mnamo mwaka 2016.

Nd. Edwin Rutageuka alisema huu ni ushahidi tosha unaothibtisha kwamba Tanzania inazidi kujiimarisha katika kukuza Uchumi unaotegemea Sekta ya Viwanda.

Mkurugenzi Mkuu huyo wa Tantrade aliihakikishia Zanzibar kwamba Taasisi hiyo imejitolea kuendelea kushirikiana na Wizara ya Biashara na Viwanda ya Zanzibar katika kuona ule mpango wa SMZ wa kutaka kuwa na Kituo cha Maonyesho ya Biashara Nyamanzi kinajengwa.

Akitoa salamu za Wizara ya Biashara na Viwanda Zanzibar Katibu Mkuu wa EWizara hiyo Nd. Juma Hassan Reli alisema Taasisi zote zinazosimammia masuala ya Baishara na Viwanda Bara na Zanzibar zimekuwa zikishirikiana kwa ukaribu zaidi.

Ndugu Juma Reli alisema ushahidi huo umejidhihirisha pale yanapotandaliwa Maonyuesho mbali mbali kati ya pande hizo akitolea mfano yale yanayoandaliwa wakati wa Maadhimisho ya Sherehe za Mapinduzi Matukuru ya Zanzibar zinazosherehekewa kila mwaka kila ifikapo Tarehe 12 Januari.

Akimkaribisha mgeni rasmi kuyafunga Maonyesho hayo ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara wa Mkono Serikali katika Mpango wake wa kuwa na Taifa la Viwanda.

Nd. Ludovic alisema Maonyesho hayo yana lengo la kuwahamasisha Watanzania kuelewa umuhimu wa kupenda kutumia Bidhaa zianzozalishwa na Viwanda vya Tanzania.

Alisisitiza Umuhimu wa Wizara hiyo kwa kushirikiana na ile ya Zanzibar kuendelea kutafuta mbinu za kutatua changamoto zinazowakabidhi  Wajasiria amali wanaoendesha Maisha yao kwa kutegemea Sekta ya Viwanda ikiwemo tozo mbali mbali.

Katika hafla hiyo ya ufungaji wa Maonyesho ya Tano ya Bidhaa za Viwanda vya Tanzania Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alitoa Tuzo na zawadi mbali mbali kwa washiriki wa Maonyesho hayo waliofanya vyema katika utengenezaji wa Bidhaa zao.

Mapema Mheshimiwa Hemed Suleiman Abdulla alipata wasaa wa kutembelea Mabanda mbali mbali ya Maonyesho kutoka Mikoa tofauti Bara na Zanzibar na kuonyesha kuvutiwa na bidhaa zinazozalishwa na Wadau hao wa Sekta ya Viwanda Tanzania.

Ujumbe wa Mwaka huu wa Maonyesho ya Tano ya Biadhaa za Viwanda vya Tanzania unasema:- “ TUMIA BIDHAA ZA TANZANIA, JENGA TANZANIA”.

 

 

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.