Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk Hussein Ali Mwinyi Amekutana na Kufanya Mazungumzo na Uongozi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Ikulu leo.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (katikati) alipokuwa akizungumza na Uongozi wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) (kushoto) leo wakati walipofika kumpa pongezi na kuzungumzia masuala mbali mbali ya kiutendaji katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.[Picha na Ikulu] 01/12/2020.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia)akiagana na Gavana wa  Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Prof.Florens D.A.M.Luoga (kati) mara baada ya mazungumzo na Uongozi wa Benki hiyo yaliyofanyika leo  katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mheshimiwa Dk. Hussein Ali Mwinyi ameihakikishia Benki Kuu ya Tanzania (BOT) ushirikiano wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Awamu ya Nane ikiwa ni pamoja na kupokea ushauri kutoka benki hiyo kwa lengo ni kuimarisha uchumi wa Zanzibar.

Rais Dk Hussein Mwinyi ameyasema hayo leo Ikuku Jijini Zanzibar wakati alipofanya mazungumzo na Uongozi wa Benki Kuu ya  Tanzania ukiongozwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Profesa Florencs Luoga pamoja na viongozi wengine wa Benki hiyo kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika maelezo yake Rais Dk. Hussein aliupongeza na kuukaribisha ujumbe huo huku akieleza kwamba ipo haja kwa Benki hiyo kuishauri Zanzibar katika masuala ya kiuchumi katika kufikia malengo yaliyowekwa kutokana na utaalamu mkubwa uliopo katika Benki hiyo.

Rais Dk. Hussein alitumia fursa hiyo pia, kuipongeza Benki hiyo ya (BOT) kwa uwamuzi wake wa kuipa hadhi Ofisi yake ya Zanzibar kwa kuifanya kuwa Ofisi ndogo ya Benki hiyo sambamba na kuahidi kuendelea kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.

Alisema kuwa tayari kwa upande wa Tanzania Bara uwezo mkubwa umejengwa sambamba na kufanya tafiti ambapo matokeo yanaonekana na kueleza kwamba kwa upande wa Zanzibar nayo ina jukumu la kuyachukua na kuweza kuyafanyia kazi ili yaweze kuleta matokea chanya.

Alisema kuwa mifumo iliyojengwa kwa upande wa Tanzania Bara katika upande wa kodi, fedha, matumizi na mapato hivi sasa unakwenda vizuri na uwezo umejengwa kwa kutosha katika kuleta mafanikio hivyo azma ni kuungwa mkono.

Aliongeza kuwa tatizo kubwa ni ukusanyaji wa kodi na kueleza kwamba ugonjwa wa COVID 19, umekuwa ukitumika kama ni sababu ya kila kitu lakini inaonesha wazi kwamba jitihada hazipo.

Alisema kuwa licha ya kuwepo kwa ugonjwa wa COVID 19 lakini mifumo ya kodi nayo ikikaa sawa mafanikio makubwa yanaweza kupatikana na kutekelezeka.

Alisema kuwa uteuzi wa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango anaeshughulikia kodi na fedha utasaidia kwani ni vyema kiongozi huyo akahakikisha katika muda mfupi iwezekanavyo mifumo inakaa sawa na kwa vile anatokea benki ya (BOT) anamatumaini makubwa kwamba atapata msaada wa kutoka kutoka benki hiyo.

Aidha,  alisema kuwa uchumi wa Zanzibar kwa hivi sasa unatilia mkazo sana katika Uchumi wa Buluu sambamba na utalii, uvuvi wa bahari kuu na sekta nyengine hivyo, msaada wa kitaamu wa kiuchumi utahitajika kwa kiasi kikubwa kutoka benki hiyo.

Rais Dk. Hussein alisisitiza haja ya kutafuta njia bora ya kuwasaidia wajasiriamali kwani mikopo inayotolewa hivi sasamasharti yake ni magumu na ndio maana wengi wao wanafeli hivyo, msaada wa (BOT)unahitajika ili kupata njia nzuri zaidi.

Aliongeza kuwa licha ya kuwepo kwa bajeti ya Uwezeshaji wananchi kiuchumi ambayo inaonekana haukufanya vizuri kwa sababu mbali mbali ikiwemo ile zana ya baadhi ya watu katika jamii kudhani kwamba fedha za Serikali hutolewa kama zawadi hivyo mrejesho wake huwa hauendi  vyema.

Sambamba na hayo, alisema kwamba ofisi yake iko wazi katika kushirikiana na benki hiyo ya (BOT) na kusema kuwa lengo ni kutoka katika uchumi wa kawaida na kufikiria uchumi mkubwa zaidi  hasa ikizingatia haja ya kuimarisha uchumi kama zilizovyofanya nchi za visiwa duniani kwa kuyachukua mazuri na kuyaleta.

Hivyo, alieleza kwamba hatua hizo zote zinahitaji mashirikiano na Benki hiyo huku akisisitiza kwamba changamoto ya kuwepo kwa fedha haramu pamoja na changamoto nyenginezo Ofisi yake iko wazi katika kutoa mashirikiano yanayohitajika.

Mapema Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT)  Profesa Florens Luoga alimpongeza Rais Dk. Hussein kwa kuchaguliwa na wananchi kwa kura nyingi na kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi wa Awamu ya Nane.

Gavana huyo wa (BOT), alimueleza Rais Dk. Hussein  mafanikio ya benki hiyo pamoja na changamoto zilizopo na jinsi wanavyochukua juhudi za kuzitafutia ufumbuzi wa haraka.

Kiongozi huyo alimueleza Rais Dk. Hussein azma ya (BOT) ya kushirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kuhakikisha uchumi wa Zanzibar unaimarika zaidi.

Aidha, alisema kuwa uchumi wa Zanzibar umeendelea kukua kwa kiwango cha kuridhisha kwa kiwango cha wastani wa asimilia 6.8 kwa kipindi cha miaka mitano iliyopita ambapo sekta ya huduma ndio imekuwa ikichangia zaidi.

Alisisitiza kwamba mwendo wa kasi ya mfumko wa bei umebakia tulivu ambapo kasi ya mfumuko wa bei ilishukuka kutoka tarakimu mbili mwaka 2011 asilimai 14.7 na kufikia tarakimu moja ikiwa ni wastani wa asilimia 5.4 kwa kipindi cha mwaka 2013-2019.

Pamoja na mafanikio hayo, Profesa Luoga alisema kwamba bado kuna changamoto kadhaa ambazo Benki Kuu inaendelea kuzipatia ufumbuzi wa kudumu kwa kushirikiana na wadau mbali mbali huku akieleza kwamba pamoja na changamoto ya athari za ugonjwa wa Corona, sekta ya kibenki imeendelea kuwa imara.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.