Habari za Punde

Rais Dk Hussein Ali Mwinyi ampongeza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi akisalimiana na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe.Elias Kuandikwa wakati alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na kumpa pongezi kwa Ushindi alioupata katika Uchaguzi Mkuu uliopita mwaka huu.[Picha na Ikulu] 15/12/2020.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsikilza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe.Elias Kuandikwa wakati walipokuwa na mazungumzo alipofika Ikulu Jijini Zanzibar leo kwa ajili ya kujitambulisha pamoja na kumpa pongezi kwa Ushindi alioupata katika Uchaguzi Mkuu uliopita mwaka huu.[Picha na Ikulu] 15/12/2020.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Ali Mwinyi (kulia) akimsikilza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Mhe.Elias Kuandikwa (katikati) katika mazungumzo yaliyofanyika Ikulu Jijini Zanzibar leo alipofika  kujitambulisha na kumpa pongezi kwa Ushindi alioupata katika Uchaguzi Mkuu uliopita  (kushoto) Katibu Mkuu Wizara hiyo Nd,Faraji Mnyepe.[Picha na Ikulu] 15/12/2020.


RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Hussein Ali Mwinyi amempongeza Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Elias Kuandikwa kwa uteuzi alioupata na kuahidi kuendelea kushirikiana nae.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo Ikulu Jijini  Zanzibar  wakati alipofanya mazungumzo na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Elias John Kuandikwa aliyefika Ikulu kwa ajili ya kujitambulisha na kumsalimia Rais ambapo pia, Waziri huyo alifuatana na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Faraji Mnyepe.

Katika mazungumzo hayo, Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza jinsi alivyofarajika na uteuzi wa Waziri huyo kutokana na uwezo wake mkubwa wa uongozi na kuahidi kumpa mashirkiano makubwa ili iwe ni chachu katika utekelezaji wa kazi zake ndani ya Wizara hiyo.

Rais Dk. Hussein alisema kuwa kwa vile Wizara hiyo ni ya Muungano ana matumaini makubwa kwamba ataendelea kuwa karibu na Waziri huyo katika kuhakikisha anatekeleza vyema majukumu yake sambamba na kuhakikisha Brigedi za Zanzibar zinaendelea kuimarika zaidi.

Nae Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Elias John Kuandikwa alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa kuchaguliwa kwa kishindo na wananchi wa Zanzibar katika uchaguzi Mkuu uliofanyika Oktoba mwaka huu 2020.

Waziri Kuandikwa alieleza matumaini yake pamoja na yale ya wananchi wa Zanzibar na Watanzania wote kwa jumla kwamba Rais Dk. Hussein Mwinyi atawaletea maendeleo makubwa Wazanzibari hasa kutokana na kasi yake kubwa aliyoanza nayo ya utendaji wake wa kazi kwa azma ya kuwaletea wananchi maendeleo.

Aidha, Waziri Kuandikwa alimpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa kazi nzuri aliyoifanya wakati akiwa Waziri katika Wizara hiyo jambo ambalo limempa wepesi na faraja katika uongozi wake na kuahidi kufuata nyayo zake ili kufikia malengo yaliokusudiwa.

Pamoja na hayo, Waziri Kuandikwa alimuahidi Rais Dk. Hussein Mwinyi kwamba atahakikisha anatumia nafasi yake kuja mara kwa mara Zanzibar katika kutekeleza majukumu yake ya kikazi hasa ikizingatiwa kwamba Wizara yake ni ya Muungano.

Sambamba na hayo, Waziri Kuandikwa ameahidi kuendelea kujifunza kutoka kwa Rais Dk. Mwinyi kutokana na mafanikio makubwa yaliopatikana kutokana na uongozi wake akiwa katika Wizara hiyo huku akiahidi kufanya kazi zake kwa ustadi mkubwa zaidi.

Rais Dk. Hussein Mwinyi kabla ya kuchaguliwa kuwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alikuwa Waziri  wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kwa muda wa kipindi cha miaka kumi na moja (11).

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.