Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Amemuapisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif Sharif Hamad.

 

RAIS wa zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akimuapisha Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Mhe. Maalim Seif  Sharif Hamad, hafla hiyo ya kuapishwa imefanyika katika ukumbi wa Ikulu Jijini Zanzibar leo 8/12/2020.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein Ali Mwinyi amemuapisha Maalim Seif Sharif Hamad kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar na kueleza kwa upande wake kuwa atajitahidi kuyadumisha maridhiano kwa maslahi mapana ya nchi.

Rais Dk. Hussein aliyasema hayo leo mara baada ya kumuapisha Makamo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad, hafla iliyofanyika Ikulu Jijini Zanzibar.

Katika hotuba yake Rais Dk. Hussein Mwinyi alisisitiza kwamba yale yaliyo ndani ya mamlaka na uwezo wake atayatekeleza bila kigugumizi wala ajizi.

Alisema kuwa kwa kuanzia ametekeleza maelekezo ya Kikatiba kwa kuwafikia ACT Wazalendo na kuwakaribisha kuunda Serikali.

Aliongeza kuwa kwa mamlaka aliyonayo kwenye Kifungu cha 66 cha Katiba ya Zanzibar, jana Disemba 7,2020 amewateua Nassor Ahmed Mazrui na Omar Said Shaaban kuwa Wawakilishi kutoka miongoni mwa nafasi 10 alizopewa za kuteua Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi.

Aidha, Rais Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa atashauriana na Makamo wa Kwanza wa Rais juu ya kujaza nafasi zilizobakia katika Baraza la Mawaziri na namna bora ya kuendesha Serikali ya Umoja wa Kitaifa.

Rais Dk. Hussein Mwinyi  alisema kuwa yeye ni muumini wa umoja wa kitaifa, mshikamano, udugu na maridhiano na anaamini kwamba maridhiano ni njia nzuri ya kujenga umoja wa kijamii na ustawi wa nchi na wananchi wake.

Katika hotuba yake hiyo Rais Dk. Hussein Mwinyi alimshukuru Makamo wa Kwanza wa Rais Maalim Seif Sharif Hamad kwa kukubali uteuzi wake na kueleza kwamba ridhaa ya Maalim Seif imemuwezesha kutimiza matakwa ya Katiba ya Zanzibar ya mwaka 1984 katika Ibara ya 39-(1), na kunukuu  “Kutakuwa na Makamu Wawili wa Rais ambao watajulikana kama Makamu wa Kwanza wa rais na Makamu wa Pili wa Rais’.

Rais Dk. Hussein alisema kwamba maridhiano ya kweli yanajengwa kwa mambo matatu likiwemo dhamira, na kusisitiza kwamba maridhiano ya kweli hayawezi kupatikana na kuwa endelevu iwapo wahusika na wadau wote hawana dhamira ya kweli ya kufikia, kufanikisha na kuendeleza maridhiano hayo.

Alieleza jambo la pili ni kuvumiliana na kusahau yaliyopita kwani ujasiri wa maridhiano ni kusahau yaliyopita na kutotonesha vidonda kwani vidonda vikitoneshwa kila mara haviwezi kupona.

Alimalizia jambo la tatu kuwa ni kujenga utamaduni wa kuaminiana kwani maridhiano yoyote hayawezi kudumu iwapo pande mbili zitakuwa haziaminiani na  kila wakati kutafuta sababu ya kutupiana lawama na kutoana kasoro.

Rais Dk. Hussein alitoa shukurani kwa viongozi na wafuasi wa Chama cha ACT Wazalendo kwa mchango wao katika kufikia kufanyika maridhiano na wakaweza kushirikiana na Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kuunda Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Awamu ya Nane.

Alisema kuwa maamuzi hayo pia, yamefikiwa kwa kuzingatia mawazo maelekezo na busara kutoka viongozi wa chama chake cha CCM na siyo maamuzi yake pekee na kutoa shukurani kwa viongozi wenzake wa CCM kwa mawazo yao na maelekezo yao hadi kuweza kufikia katika hatua hiyo iliyoshuhudiwa hivi leo.

“Sisi viongozi kila wakati hatuna budi kuzingatia na tufahamu kwamba maslahi ya wananchi ndio jambo la msingi. Tofauti zetu kama ndogo au kubwa zisiwe kikwazo cha maendeleo ya wananchi na nchi yetu kwa jumla”alisisitiza Dk. Hussein Mwinyi.

Aidha, Dk. Hussein Mwinyi alitoa nasaha zake kwa wananchi na kuwataka wote wawe kitu kimoja na kuunga mkono juhudi hizo zenye lengo la kudumisha umoja na mshikamano.

Alimshukuru Makamu wa Kwanza wa Rais kwa kuheshimu na kutimiza matakwa ya Kikatiba na kwa moyo wake wa maridhiano.

Aidha, alikishukuru chama chake cha CCM kwa ushirikiano ambao kimempa na kumshukuru Mwenyekiti wa CCM Taifa Dk. John Pombe Magufuli na Makamu Mwenyekiti wa CCM na Rais Mstaafu wa Zanzibar, Dk. Ali Mohamed Shein kwa baraka zao na kuunga mkono hatua hiyo.

Sambamba na hayo, alieleza kwamba kizazi cha leo cha Wazanzibari ambao asilimia 93 wamezaliwa baada ya Mapinduzi na Muungano, kinayo dhima ya kipekee ya kufunga ukurasa wa uhasama na chuki na kufungua ukurasa mpya wa upendo na maridhiano.

Mapema Makamo wa Kwaza wa Rais wa Zanzibar Maalim Seif Sharif Hamad katika hotuba yake alimshukuru na kumpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa nia yake thabiti aliyoonoesha ya kujenga maridhiano na kukubali pendekezo la chama cha ACT Wazalendo na kumteua yeye kuwa Makamo wa Kwanza wa Rais.

Alieleza kuwa chama chake kimeona Rais Dk. Hussein ni mtu wanaeweza kufanya nae kazi, anaeweza kusikilizana na wanaeweza kumpa nafasi ya kuthibitisha nia yake njema.

Aliongeza kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa iliyoasisiwa na Katiba ya Zanzibar kupitia marekebisho ya Kumi ya Katiba ya mwaka 2010 ilikusudiwa kuwa chombo cha kusimamia, kuratibu na kuongoza juhudi za Wazanzibari kufikia Maridhiano na Umoja wa Kitaifa.

Alisema kuwa haikuwa na bado sio lengo la Serikali ya Umoja wa Kitaifa kuwa chombo cha kugawana vyeo kwa kambi za kisiasa.

Maalim Seif alisema kuwa chama chake kuingia Serikalini na kuingia Barazani ni ishara ya nia njema ya kutaka kushirikiana na Rais Dk. Hussein Mwinyi na kuongeza kuwa maridhiano, amani na utulivu ndio jawabu la kuivusha Zanzibar kutoka ilipo sasa kwenda kuwa Zanzibar iliyopiga hatua kubwa kimaendeleo.

“Kwa sababu ya mwelekeo huo ndio maana chama changu cha ACT Wazalendo na mimi mwenyewe binafsi tumekubali kuingia kwenye Serikali ya Umoja wa Kitaifa ili kusaidia na kuijenga Zanzibar mpya”,alisema Maalim Seif.

Pamoja na hayo, Maalim Seif alitoa wito kwa Wazanzibari wote waliopo ndani na nje ya nchi wakubali kunyoosha na kupokea mkono wa maridhiano.

Sambamba na hayo, Maalim Seif alitumia fursa hiyo kumpongeza Rais Dk. Hussein Mwinyi kwa kuanza kazi vizuri, alimpongeza Makamo wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla kwa kuteuliwa, aliwapongeza Mawaziri wote walioteulwia, Wakuu wa Mikoa na kuwapongeza Wawakilishi Nassor Ahmed Mazrui na Omar Said Shaaban.

Katika hafla hiyo, viongozi mbali mbali walihudhuria akiwemo Makamo wa Pili wa Rais Hemed Suleiman Abdulla, Spika wa Baraza la Wawakilishi Zubeir Ali Maulid, Jaji Mkuu wa Zanzibar Omar Othman Makungu, Katibu wa Baraza la Mapinduzi na Katibu Mkuu Kiongozi Dk. Abdulhamid Yahya Mzee.

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mwinyi Talib Haji, Mawaziri, Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Idirisa Kitwana Mustafa, Naibu katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Abdalla Juma Mabodi, Wakuu wa vikosi vya ulinzi na usalama, viongozi wa vyama vya siasa, Mufti Mkuu wa Zanzibar Sheikh Omar Salh Kabih na viongozi wengine wa dini, viongozi wa Serikali na wanafamilia.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.