Habari za Punde

Ziara ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Kutembelea Mradi wa Huduma za Jamii Mijini ZUSP.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akiwa katika ziara yake kutembelea Mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) kuangalia utendaji wa Mradi huo wa ujenzi wa mitaro ya kupitishia maji machafu na (kulia kwa Rais) Mke wa Rais wa Zanzibar Mama Maryam Mwinyi na Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mhe. Zuberi Ali Maulid na (kushoto kwa Rais) Mkuu wa Mkoa wa Mjini Magharibi Unguja Mhe. Idrisa Kitwana Mustafa na Waziri wa Ujenzi Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar Mhe. Rahma Kassim Ali.
 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la MapinduziDk. Hussein amefanya ziara ya kuutembelea baadhi ya maeneo yaliyomo kwenye mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) na kueleza kwamba hajaridhika na hali ya usafi katika maeneo yote ya Mji wa Zanzibar.

Rais Dk. Hussein aliyasema hayo leo wakati wa ziara yake hiyo ambayo alipata fursa ya kutembelea maeneo mbali mbali yaliyomo kwenye mradi wa ZUSP pamoja na maeneo yanayotupwa taka katika makaazi ya watu ndani ya mji wa Zanzibar bila kufuata taratibu pamoja na kulitmbelea jaa la Kibele.

Akikamilisha ziara yake hiyo huko Kwarara, Wilaya ya Magharibi B, alieleza kwamba mji wa Zanzibar bado hauko safi na kueleza kwamba hajaridhika na hali hiyo na wala kuridhika na utendaji wa mradi wa ZUSP ambao Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imekopa fedha nyingi kutoka Benki ya Dunia zipatazo Dola milioni 55 katika awamu ya pili ya mradi huo.

Alisema kuwa mahitaji yaliyokusudiwa katika mradi huo hayajafikiwa na Wilaya hazifanyi wajibu wao ipasavyo katika suala la usafi kutokana na kutokuwepo mipango madhubuti ya mradi.

Alisema kuwa katika vituo vya taka kumekuwa na ucheleweshaji mkubwa wa taka ambazo hukaa kwa muda mrefu hali ambayo inahatarisha afya za wananchi.

Alisisitiza kwamba hakuna sehemu maalum ya kuhidhadhi taka hali inayopelekea mji uendelee kuwa mchafu, hivyo alisisitiza haja ya kurekebishwa kwa hali hiyo na kuwataka watendaji wote husika kufanya kazi.

Alieleza kuwa vifaa vingi vilivyonunuliwa katika mradi huo havikidhi haja ya mradi na kusisitiza kwamba jambo hilo atachukua hatua kwani fedha iliyotumika ni kodi ya wananchi.

Rais Dk. Mwinyi alisikitishwa na hali ya kuwa hadi hivi leo ambapo mradi huo unatakiwa kumalizika mwishoni mwa mwezi huu wa Disemba lakini kuna fedha hazijatumika nabado mahitaji mengi yanahitajika yakiwemo vifaa kwa ajili ya usafi wa mji.

Aliongeza kuwa katika mradi huo kuna wataalamu wengi lakini hawafanyi kazi zao ipasavyo katika kuusimamia mradi huo hali inayopelekea kutumia fedha kinyume na matakwa ya mradi.

Kwa upande mwengine Rais Dk. Hussein Mwinyi alizitaka Manispaa za Wilaya zote za Mjini kuwajibika na kufanya kazi zao kwani hali ya mji wa Zanzibar bado ni mchafu na kumtaka Mkuu wa Mkoa kukaa na Manispaa zote tatu kwa lengo la kutafuta suluhisho.

Baada ya kupata malalamiko ya wakaazi wa Kwarara juu ya uchimbaji wa mchanga kiholela, Rais Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa ni marufuku kwa mtu yoyote kuchimba mchanga katika maeneo hayo bila ya kibali cha Serikali na kuwataka kutoa taarifa kwa wananchi pale wanapowabaini wananchi wanaofanya uhalifu huo.

Aidha, alimtaka RPC wa Mkoa wa Mjini kutafuta ufumbuzi wa haraka katika kuweka hali ya usalama kwenye eneo hilo la Kwarara kufuatia malalamiko kutoka kwa wananchi juu ya hali ya usalama wao.

Mapema akiwa katika eneo la  Jaa la Kibele, Wilaya ya Kati Mkoa wa Kusini Unguja, Rais Dk. Hussein Mwinyi alisisitiza haja ya kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa malengo yaliyokusudiwa.

Aidha, alimuagiza Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja Rashid Hadidu Rashid kuyafanyia kazi malalamiko ya wananchi waliyomueleza Rais yakiwemo kuhusu uhaba wa fedha walizolipwa fidia, kubomolewa nyumba zao pamoja na kutopata maslahi kwa wale wafanyakazi wa Mradi huo kutoka kampuni iliyojenga mradi huo.

Pia, Rais Dk. Hussein alimtaka Mkuu wa Mkoa huyo kwa yale ambayo yatamshinda ampelekee yeye ili akayatafutie ufumbuzi huku akiagiza kutafutwa eneo maalum kwa ajili ya taka zote za hospitali.

Aliagiza kurejeshwa kwa gari katika mradi huo na kukabidhiwa Meneja wa Mradi huo sambamba na kuhakikisha vifaa vyote husika vinapatikana.

Naye Mshauri Elekezi wa ujenzi wa Mradi Jaa la Kibele David Masawe kutoka Kampuni ya HYDEA, akitoa maelekezo kwa Rais Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa mradi huoalisema tayari umeshakamilika na hivi sasa mradi huo umo katika kwenye uangalizi.

Wakati huo huo, Rais Dk. Hussein Mwinyi ameutaka uongozi unaosimamia utekelezaji wa mradi wa Huduma za Jamii Mijini (ZUSP) kuhakikisha kazi zilizobaki katika maeneo mbali mbali zinakamilishwa katika kipindi cha miezi mitatu.

Dk. Mwinyi ametoa agizo huko Kilimani Jijini Zanzibar, kufuatia ziara aliyofanya ya kutembelea utekelezaji wa mradi huo kutoka Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Amani Karume hadi Kilimani, ambapo alipata fursa ya kuangalia Taa, bustani pamoja na mtaro wa maji uliopembezoni mwa bara bara hiyo.

Rais Dk. Mwinyi ambaye alitembelea kwa miguu kutoka Uwanja wa ndege wa Zanzibar hadi Kimalini akiwa anaangalia hali ya uendelezaji wa Mradi huo wa ZUSP akiwa amefuatana na viongozi mbali mbali akiwemo Spika wa Baraza la Wawakilishi Mhe.Zubeir Ali Maulid, baadhi ya Mawaziri, Mama Mariam Mwinyi na viongozi wengine pamoja na watendaji wa Serikali.

Katika maelezo yake Rais Dk. Mwinyi alisema kuwa utekelezaji wa mradi huo umekuwa na mapungufu makubwa na kusema haitoi taswira njema ya kuifanya barabara hiyo kuwa kioo cha mji wa Zanzibar mbali na mradi huo kuidhinisha fedha nyingi.

Aliwataka viongozi wanaosimamia mradi huo kuhakikisha mradi unakamilika ifikapo mwishoni mwa mwezi wa Februari pamoja na barabara hiyo kuwa safi muda wote, huku akibainisha umuhimu wa miradi yote mikubwa kuwa na kipengele cha kuifanyia matengenezo (maintanance contract).

Rais Dk. Mwinyi aliagiza miti yote iliyopandwa kati kati ya barabara hiyo kumwagiliwa maji ili iweze kustawi vyema, akieleza kutorishwa kwake na hali ilivyo kwani baadhi yake tayari imeanza kukauka kutokana na ukosefu wa maji.

Aliutaka uongozi wa Manispaa za Magharibi A na B kuhakikisha Mtaro unaoendelea kujengwa pembezoni mwa barabara hiyo inakuwa safi, sambamba na kuziweka katika mazingira mazuri bustani zilizopo.

Aidha, alisisitiza umuhimu wa kuajiri wafanyakazi kwa kuzingatia mahitaji yaliopo, akibainisha kuwepo kwa kundi kubwa la wafanyakazi wakati ambapo kazi inayofanywa ni ndogo.

Katika hatua nyengine Dk. Mwinyi alitembelea Kituo cha Mradi wa taka kiliopo eneo la Maruhubi na kuutaka uongozi unaosimamia mradi huo kukaa pamoja na wadau ili kuwaelewesha juu ya utekelezaji sahihi wa mradi huo.

Alisema kuna umuhimu wa wasimamizi wa mradi huo kuzingatia muda wa mradi uliobainishwa katika mkataba ili uweze kukamilika kwa wakati sahihi.

Alisema hoja kubwa ya Serikali na wananchi wa Zanzibar ni kwa mradi huo kuwa ufumbuzi wa kuwaondolea kero ya taka ilioshamiri katika maeneo yote ya Miji na sio katika Manispaa ya Mjini pekee kama uongozi wa ZUSP ulivyojikita.

Dk. Mwinyi aliukumbusha uongozi wa Wizara ya Nchi (OR) Fedha na Mipango wajibu walionao katika kufanikisha mchakato wa upatikanaji wa mikopo ya miradi badala ya kujikita katika usimamizi wake kama inavyofanyika hivi sasa.

Aidha, aliwataka watendaji hao kuwa na hesabu kamili na kufahamu muda utakaotumika kujaza taka makontena yaliopo pamoja safari zitakazofanyika kupeleka taka hizo Kibele, hatua itakayowawezesha kubaini mapungufu katika utekelezaji wake.

Nae, Mratibu wa Mradi wa ZUSP Makame Ali Haji alisema pale mradi huo utakapokamilika utaongeza kasi ya ukusanyaji wa taka  katika maeneo yote ya Mjini kutoka asilimia hamsini (50%) hivi sasa hadi kufikia asilimia 75%. 

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.