STATE HOUSE ZANZIBAR
OFFICE
OF THE PRESS SECRETARY
PRESS
RELEASE
Zanzibar Disemba 28, 2020
RAIS
wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi ameahidi
kuunda Tume maalum ya Uchunguzi ili kubaini sababu zilizosababisha kuporomoka kwa sehemu ya Jengo la Beit el Ajaib mwishoni
mwa wiki iliyopita.
Dk. Mwinyi ameeleza hayo leo katika
Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul-wakil Kikwajuni Jijini Zanzibar, wakati
alipokutana na wadau mbali mbali wa Mji
mkongwe.
Alisema iko haja ya kuunda Tume ya
Uchunguzi ili kubaini chanzo cha ajali
iliotokea pamoja na kutafuta njia
zitakazowezesha kuepuka majanga, sambamba na kuwepo uhifadhi bora wa mji huo.
Alisema ni jukumu la taasisi zilioko
Mji Mkongwe, ikiwemo Mamlaka ya Mji Mkongwe, Wakfu na mali ya Amana pamoja na
Shirika la nyumba kushirikiana ikiwa ni hatua ya kuyatafutia ufumbuzi matatizo mbali mbali yanayokabili
mji huo.
Alisema Tume itakayoundwa itakuwa na
jukumu la kuangalia sababu zilizosababisha kuporomoka kwa sehemu ya jengo hilo na nini kinahitaji kufanyika ili kuwepo
uhifadhi bora wa Mji huo, ukihusisha majengo yake.
Aidha, alisema Tume hiyo itaangalia
changamozo zinazokabili Taasisi zilizopewa mamlaka, akibainisha baadhi ya changamoto
hizo hutokana na urasimu wa kiutendaji.
Alisema maeneo mengine yatakayopaswa
kuangaliwa na Tume hiyo ni kuhusiana na weledi wa watendaji pamoja na muundo wa
Bodi, huku akibainisha Tume hiyo itafanyakazi kuambatana na hadidu rejea.
“Lengo ni kutunza Mji na kuepusha
maafa………..mapendekezo yanapawa kuwa ya muda mrefu, kati na mrefu ikizingatiwa gharama nyingi zinazohitajika”,
alisema.
Dk. Mwinyi alisema taarifa ya
uchunguzi inapaswa kuainisha juu ya majengo yatakayohitaji kufungwa na wakaazi
wake kuondolewa mara moja
Alieleza kuwa Zanzibar imepoteza nembo
muhimu ya Taifa na kusema wakati umefika wa kutizama ustawi wa mji mkongwe
katika jicho la aina yake.
Alisema uchunguzi utakaofanywa
haulengi kumtuhumu au kumuonea mtu, bali utazingatia haki na hivyo hatua zitachukuliwa pale itakapobainika kufanyika uzembe.
Rais Dk.Mwinyi, akitoa ufafanuazi wa
baadhi ya mapendekezo, alisema katika
mwelekeo wa kuwa na Mji Mkongwe uliohifadhika vyema, ni lazima kuwepo mfuko
maalum wa Uhifadhi wa mji huo na kusema serikali itakuwa ya kwanza katika
kuchangia, sambamba na kuwashajiisha wadau kufanya hivyo.
“Serikali itaweka ‘seriousness’ katika
uhifadhi wa mji mkongwe kwa kuwa na bajeti na wafanyakazi wenye taaluma pamoja
na mfuko maalum, lakini pia naunga mkono suala la kuwa na ‘stone town day’”,
alisema.
Aidha, alisema ni wakati muafaka wa
kuangalia kwa makini utaratibu wa vyombo vya moto kuingia na kutoka katika eno la Mji Mkongwe.
Alitumia fursa hiyo kuishukuru
Serikali ya Oman kwa utayari wake katika kusaidia uhifadhi wa mji Mkongwe a Zanzibar.
“Gharama za uhifadhi lazima
zichukuliwe na Serikali kabla ya msaada, hivyo Serikali itakuwa mstari wa mbele
katika kufanikisha jambo hilo, nawaomba wadau kufanya kila linalowezekana kutunza mji mkongwe, kwa kuwa ni chanzo kikuu
cha mapato pale utakapohifadhiwa vyema”, alisema.
Mapema, Waziri wa Utalii na Mmabo ya
Kale, Lela Mohamed Mussa pamoja na mambo mengine alisema katika tukio la
kuporomoka kwa sehemu ya Jengo la Beit el Ajaib, mwishoni mw awiki iliyopita
mafundi wanne walijeruhiwa na wengine wawili kufariki dunia.
Aidha, Mkurugenzi, Mamlaka ya Mji
Mkongwe Issa Sarboko Makarani, alisema miongoni mwa faida kubwa zinazotokana na
Mji Mkongwe wa Zanzibar kuwepo katika Urithi wa Kimataifa ni kupata msaada Wa matengenezo
pale yanapotokezea maafa, ikiwemo kuporomoka kwa majengo yake.
Alisema Mamlaka ya Mji Mkongwe katika
nyakatri zote imekuwa ikipata msaada mdogo wa kifedha kwa ajili ya kuyashughulikia
majengo yake na ndio sababu ya kuporomoka kwa sehemu ya jingo la Beit al Ajaib
na mengineyo, sambamba nakusema ukosefu
mkubwa wa wafanyakazi wenye taaluma ya Uhifadhi wa Mji Mkongwe kuwa ni
changamoto kubwa inayoikabili mamlaka hiyo.
Nao, wadau mbali mbali wa Mji Mkongwe
wakichangia katika mkutano huo; waliishauri Bodi inayosimamia uhifadhi wa Mji
Mkongwe kuwa na mainjinia wa kutosha ili
kufanyakazi ya kuyakagua majengo mbali mbali yaliomo katika eneo hilo.
Walisema taarifa za uchakavu wa
majengo ni vyema zikawa zinatumwa UNESCO
kabla ili kuepuka majanga mbali mbali ikiwemo vifo.
“Wizara inapaswa kuwa makini wakati wa
kutafuta wajumbe wa Bodi ya Mamlaka ya Mji Mkongwe, ili kuwa na watu wanaoendana
na sifa na mahitaji halisi”, alisema Siti Abasi Ali.
Aidha, walisema Serikali inapaswa
kusaidia katika usimamizi wa upigaji marufuku wa vyombo vya moto, (ikiwemo
Bodaboda) kuingia katika eneo la Mji Mkongwe , ikiwa ni hatua ya kuimarisha
usalama.
Vile vile waliiomba serikali kuanzisha
mfuko maalum (utakaoendeshwa kwa uwazi) katika dhana ya kuuendeleza uhifadhi pamoja na kutoza ada
maalum kwa ajili ya kuchangia uhifadhi
wa mji huo.
Wadau hao wamevitaka vyombo vya
habari, hususan Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kuwa na vipindi maalum vya
kuutangaza Mji Mkongwe wa Zanzibar, wakati ambapo wameibua hoja kuwa wananchi
wengi hawaelewi thamani ya Mji huo na utajiri mkubwa ulionao.
Mkutano huo uliwashirikisha viongozi
wa Kitaifa na wadau mbali mbali, akiwemo Mwakilishi Wa Balozi wa Oman, Mawaziri
wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Mwanasheria Mkuu wa Zanzibar Dk. Mwinyi
Talib haji, Mufti Mkuu wa Zanzibar
Sheikh Saleh Omar Kaab, Mstahiki meya wa Jiji la Zanzibar Saleh Kinana,
Viongozi wa Vikosi maalum vya Serikali ya Zanzibar, Wawekezaji wa sekta ya
Ualii pamoja an wadau mbali mbali wa Mji
Mkongwe.
Abdi
Shamna, Ikulu Zanzibar
Postal Address: 2422
Tel.:0777476982. Fax: 024 2231822
E-mail: abdya062@gmail.com
No comments:
Post a Comment