Habari za Punde

Rais Dk Hussein Ali Mwinyi: Uchumi Utaendeshwa na Sekta Binafsi

 

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi akisisitiza jambo wakati akizungumza Wafanyabiashara wa Sekta mbalimbali Zanzibar uliofanyika katika Ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdulwakil Kikwajuni Jijini Zanzibar.

RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyiamesema kuwa Serikali anayoiongoza itatoa msukumo mpya katika kutatua changamoto zinazokabili biashara hapa Zanzibar.

Rais Dk. Hussein Mwinyi aliyasema hayo leo katika hotuba yake aliyoitoa katika mazungumzo kati yake na wafanyabiashara wa Zanzibar, hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Sheikh Idriss Abdulwakil, Kikwajuni Jijini Zanzibar.

Katika hotuba yake Rais Dk. Hussein Mwinyi alisema kuwa anataka kuweka mashirikiano na sekta binafsi pamoja na kuongeza na kuwepo mijadala ya wazi na yenye tija kwa lengo la kuweka mazingira mazuri kwa wafanyabiashara.

Rais Dk. Hussein alisema kuwa Serikali haifanyi biashara bali kazi yake ni kutengeneza Sera nzuri, sheria, kanuni, na kuweka mifumo ya udhibiti wa biashara lakini uchumi utaendeshwa na sekta binafsi.

Aliongeza kuwa Serikali itaweka mfumo rafiki, kuondoa urasimu, rushwa na vikwazo vyote vinavyotakana na utendaji mbovu.

Rais Dk. Hussein alieleza maono yake ni kuifanya Zanzibar kuwa ni kituo cha biashara katika Afrika Mashariki hasa kutokana na mazingira yake kijiografia kwani Zanzibar inaweza ikawa kituo cha biashara, utalii, viwanda, bandari huru hiyo ni kutokana na jinsi ilivyo.

Rais Dk. Hussein alirejea kauli yake ya kuwataka viongozi wa Mawizara kutengeneza mipango yenye bajeti huku akisema kuwa kila sekta ina utaratibu wake na kwa upande wa ujenzi wa barabara Serikali itafanya na kuchukua jukumu lake hilo la kujenga barabara na sio sekta binafsi.

Alisema kuwa madhumuni ya mkutano huo ni kutimiza ahadi yake aliyoahidi wakati wa Kampeni ya kukutana na wafanyabiasharana kutaka kujua changamoto zao na kuahidi pale atakapaingia madarakani watakaa pamoja huku akieleza kwamba changamoto zote amezisikia na zitafanyiwa kazi hasa ikizingatiwa viongozi wa Serikali walikuwepo katika mazungumzo hayon wakiwemo Mawaziri na Makatibu Wakuu.

Katika maelezo yake alisema kwambazipo tabia ya kufanya mikutano mingi bila ya ufumbuzi ambapo katika utawala wake tabia hiyo hatoitaka na kusisitiza kwamba kuchukuliwa changamoto na kutofanyiwa kazi ni kupoteza muda hivyo ni lazima mikutano iwe na tija.

Hivyo, aliwaeleza watendaji wote Serikalini kwamba ana miadi na wananchi katika miaka mitano hivyo ni lazima kufanya kazi kwa haraka ili kutatua changamoto zilizopo na kama zikitokezea kuwashinda apalekewe.

Alisema kuwa kwa upande wa bandari, katika mradi huo kuna uwezekano mkubwa wa kushirikiana na sekta binafsi.

Aidha, alieleza uwezekano wa kuwa na bandari hapa Zanzibar itakayotoa huduma za utalii, bandari za uvuvi na bandari za mafuta na bandari za kila kitu  kwa ajili ya kuchukua meli kubwa ambapo kwa upande wa meli ndogo zinaweza kufanya kazi za kusambaza katika maeneo mengine kutoka Zanzibar.

Aliwaahaidi kwamba  Serikali iko tayari  kushirikiana na sekta binafsi ili kuweza kuyatimiza hayo kwa mustakbali wa Zanzibar.

Alisema kuwa kwa pamoja inawezekana kufanyika hayo kwani uwezo upo, mtaji na upo , uzoefu upo, masoko na utayari wa Serikali upo na rasilimali ipo na kwa vile Zanzibar inajitangaza vyema nje ya nchi hatua hiyo itasaidia.

Alisema kuwa mabenki kadhaa hapa nchini yameonesha nia ya kushirikana na Serikali katika kuijenga Zanzibar kwa masharti nafuu hivyo, uwezo wa kifedha upo na hayo yanawezekana na yanatekelezeka katika azma ile ile ya kuijenga Zanzibar kiuchumi.

Alirejea kutoa ahadi yake kwa wafanyabiashara ya kuondosha changamoto zote zinazokwamisha biashara hapa Zanzibar.

Akieleza changamoto ya kodi alisema kuwa yeye si muumini wa kodi kubwa kwani wapo watu wanaodhani kwamba kodi kubwa ndio pato kubwa kwa Serikali lakinhi ni kinyume chake na badala yake kodi kubwa ndio inayopunguza wafanyabiashara.

Aliongeza kwamba watakaofanya biashara kwa kodi kubwa ni wachache lakini ikipunguzwa kodi watakaofanya biashara ni wengi, lakini serikali haiishi kwa kodi pekee bali  mzunguko wa biashara ndio unaoongeza fedha na kukuza uchumi.

Kwa upande wa suala la udhitibi,alisema kuwa kuna mamlaka za udhibiti zipo nyingi ambazo zote zinataka kutoza bidhaa moja bila ya kutokuwepo sababu na kutolea mfano wa badari ya Malindi, Zanzibar ambapo mamlaka zinazotoza kodi zipo karibu nne.

Alisema kuwa wakati umefika wa kuziunganisha baadhi ya mamlaka ili kuweza kupata ufanisi jambo ambalo linawezekana na litafanyika kwani Zanzibar ni ndogo na haiitaji kuwepo mamlaka nyingi.

Alieleza matatizo ya miundombinu ya usafiri ikiwemo bandari, ambapo hivi sasa watu wameigeuza bandari ni sehemu ya kuweka makontena yao.

Anataka kuweka utamaduni wa kufanyakazi kwa pamoja kati ya sekta binafsi na sekta ya umma katika serikali na kusisistiza kwamba sekta binafsi inaweza kushirikiana na serikali katika masuala mengi lakini wanaohitajika ni wale ambao wanaelewa.

Alisisistiza kuwa watu watakaoendesha mashirikia ya baishara ni lazia wawe wanajua biashara na haiwezekani kuona mtu anaongoza shrika halafu anapata hasara  na kueleza tataizo la badanri na uwanja wa ndege yatakwisha.

Aliongeza kuwa hakuna Mamlaka ya Vitega Uchumi Zanzibar (ZIPA) itakuwa onestope center kwa kujumuisha masuala yote muhimu kwa muwekezaji na wahusika wote ni lazima wawepo ZIPA ili kikitoka kibali kitoke kwa pamoja.

Alisema kuwa utaondoshwa urasimu, rushwa, watu kutowajibika katika taasisi hiyo na kueleza sababu ya kuiweka Wizara husika inayoshughulikia uwekezaji kuwa chini yake iili iwe chini ya macho yake na hilo ni kwa kila Wizara.

Aliwataka kila kiongozi ayachukue yale yaliyozungumzwa na wafanyabiashara ili wakikutana tena wazungumzie mafanikio na sio changamoto.

Kwa upande wa ajira alisisitiza haja ya kuekekeza katika kupata ajira 300,000,alizoziahidi wakati wa Kampeni kwa mashirikiano na sekta binafsi  na kusisitiza haja ya kupatikana ajira zaidi ya hizo iwapo sekta ya viwanda itaimarishwa.

Alisema kuwa changamoto za watu kuekeza kwenye sekta ya viwanda zitaondoshwa na kusisistiza kwamba Serikali inataka kuekeza viwanda vyenye kuajiri watu wengikwani  viwanda vingi vinaweza kupatikana hapa Zanzibar ilimradi tu mazingira yawe mazuri huku akieleza haja ya kuvilinda viwanda vya ndani kwa lengo ni kumnufaisha Mzanzibari.

Rais Dk. Hussein alisema kuwa lazima kuwepo sera za kuwasaidia watu wa ndani na kutaka kuewa upendeleo kwa wazawa kwani hivyo ndivyo nchi nyengine zinazoyajenga makampuni yao.

Aliwasisitiza wafanyabiashara kulipa kodi huku akisema kuwa kodi maalum zimewekwa Zanzibar ili kuwasaidia Wazanzibari kupata unafuukatika bidhaa zao licha ya kuwa bado wananchi wa kawaida hawanufaiki.

Alisema kuwa wapo wafanyabiashara ambao hawalipi kodi “sina nia ya kufufua makaburi na kumtafuta mchawi lakini nataka kusema kuanzia sasa kila mtu alipe kodi”, alisema Dk. Hussein.

Alisema kuanzia sasa kwenda mbele kila mtu alipe kodi ikiwa ni pamoja na kulipa kodi inayolipwa kutoka kwa wafanyakazi kutoka nje, na kusisitiza kwamba kodi ndogo zilipwe na kutaka kulipwa jinsi inavyotakiwa kulipwa na kutaka kuwekwa mifumo mizuri ya kodi.

Alisema kuwa hapo zamani watu walikuwa wanakuja kununua bidhaa Zanzibar kwa sababu kodi ilikuwa ndogo na bei afadhali lakini hivi sasa wengi wao wanaelekea Kariakoo Dar-es-Salaam kwa sababu bei ya mwisho haimsaidii mwananchi.

Rais Dk. Hussein alisema kuwa ni vyema mfanyabiashara akapata faida, Serikali ikapata na mwananchi nae apate na isiwe upande mmoja tu wa wafanyabiashara pekee yao wakapata.

Alisema kuwa bado utamaduni wa kufanya kazi kwa mazoea utachukua muda lakini jitihada zitafanyika katika kuuondoa haraka na kusema kuwa hatowaachia Mawaziri pekee yao na kuahidi kuunda Kitengo kitakachokuwa chini ya Ofisi yake kitakachokuwa na kazi ya  Ufuatiliaji wa Utekelezaji wa Miradi katika sekta mbali mbali “President’s Delivery Bureau” (PDB).

Alieleza kuwa kazi ya taasisi hiyo itakuwa ni kuuangalia uchumi wa Zanzibar unakwenda vile anavyotaka, itakuwa na wataalamu wa uchumi, wa fedha na maeneo mengine mbali mbali ambacho kitasaidia pia, kuwasukuma Mawaziri katika kutekeleza majukumu yao ambapo pia, wataalamu wa taasisi hiyo watakuwa wafuatiliaji wa maazimio yote yanayoazimiwa kufanywa.

Alisema kuwa miradi ya Serikali iko mingi na wote wanaweza kunufaika na kuwataka kuwa wawe tayari kushirikiana na kuwahakikishia wafanyabiashara hao kwua maoni yote waliyoyatoa yatafanyiwa kazi na kuwataka kwenda kukaa na Mawaziri ili kuyatekeleza yote hayo.

Sambamba na hayo, aliahidi kukutana na wafanyabiashara wa kila sekta, huku akisema kwua mazingira ya kufanya biashara Zanzibar yatakaa sawa na kusisitiza kwamba Mawaziri wote watafanya kazi na wafanyabiashara hao kwa karibu.

Mapema akitoa salamu kutoka sekta binafsi Ali Amour alisema kuwa ipo haja ya kuweka vivutio maalum kwa ajili ya uwekezaji katika maeneo maalum yatayofanyiwa utafiti maalum ikiwemo ya kisiwa cha Pemba na kuahidi mchango wake wa kuchukua jukumu la kushajihisha matumizi sahihi ya maeneo hayo.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.