Habari za Punde

Taarifa Ya Mheshimiwa Simai Mohammed Said Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.leo Ijumaa 15 Januari 2021.


Mhe.Simai Mohammed Said Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar.

Ndugu Wananchi
Wazazi na Walezi
Walimu na Wanafunzi
Assalamu Alaykum;
Ifuatayo ni Taarifa Maalum kuhusu uratibu na uendeshaji wa Masomo kwa mwaka 2021. Kama mjuavyo kuwa skuli zote za Serikali na Binafsi zitafunguliwa rasmi Siku ya Jumatatu ya Tarehe 18 Januari 2021 na kumaliza Muhula wa masomo tarehe 10 Disemba 2021.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar imepanga Kalenda ya Masomo mwaka 2021 kuwa na Mihula miwili ambayo itakuwa na shughuli zifuatazo:
 Jumla ya Wiki za Masomo 43
 Jumla ya Wiki za Mapumziko 07
 Jumla ya Siku za Masomo 213
 Jumla ya Siku za Mapumziko 42
 Jumla ya Siku za Maadhimisho ya Kitaifa 13
INDHARI/ZINGATIA

 Siku za Mwezi Mtukufu wa Ramadhan Masomo yataanza Saa 1:30 Asubuhi hadi Saa 4:30 Asubuhi kwa Mkondo wa Asubuhi na kwa Mkondo wa Mchana Masomo yataanza Saa 5:00 Asubuhi hadi Saa 8:00 Mchana na Skuli zenye Mkondo Mmoja Masomo yataanza Saa 2:00 hadi Saa 7:00 Mchana.
Ndugu Wananchi, Wazazi na Walezi, Walimu na Wanafunzi

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali inawaomba kuzingatia mambo yafuatayo ili kufikia lengo lililokusudiwa la kutoa Elimu Bora kwa Jamii.

i. Skuli zote za Serikali na Binafsi kuhakikisha kuwa zinafuata Mitaala na Mihutasari rasmi iliyoidhinishwa na Serikali na kukamilishwa kwa wakati uliowekwa ili wanafunzi wamalize masomo yao kwa muda uliopangwa.
ii. Tunawaomba Wazazi, Walezi, Walimu na Wadau wengine wa elimu washirikiane kwa pamoja katika malezi ya watoto wetu ili kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora itakayowajengea ufahamu na kuwawezesha wanafunzi kuikabili vyema mitihani yao ya mwisho wa mwaka na kupata maarifa ya ziada kutokana na elimu hiyo.
iii. Skuli binafsi zinashauriwa kuzingatia ada zao za masomo kulingana na hali ya maisha iliyopo kwani Skuli zetu zipo kwa lengo la kutoa huduma kwa jamii na kuendelea kuisaidia Serikali katika lengo lake la kutoa elimu bora kwa watu wote.
iv. Ninazishauri Skuli za Serikali na za Binafsi ambazo wanafunzi wake wanatarajiwa kufanya mitihani ya Taifa ya Kidato cha Sita mwezi wa Mei 2021 kuhakikisha kuwa wanafunzi wote waliosajiliwa wanaruhusiwa kufanya mitihani yao bila ya kikwazo chochote.

v. Wizara inatoa agizo kwa uongozi wa skuli zote za Binafsi zinazotumia usafiri wa mabasi kwa wanafunzi kuhakikisha kuwa wanapakia wanafunzi kwa idadi husika kama inavyotakiwa na Idara inayohusika na usalama barabarani. Skuli yoyote ambayo itapakia wanafunzi zaidi ya uwezo wa basi husika taratibu za kisheria zitachukuliwa dhidi ya skuli hiyo.

Aidha, tunazitaka skuli zote zinazotumia usafiri wa mabasi kuweka alama ya utambulisho wakati wanapowapakia wanafunzi.
vi. Wizara inawashauri Wazazi na Walezi kutowapa vyombo vya moto wanafunzi ambao hawajafikia umri wa miaka 18 ili kuepusha madhara yatakayojitokeza. Wizara pia inazishauri Mamlaka zinazosimamia suala la usalama barabarani zichukue hatua zinazostahiki kwa mujibu wa sheria zilizopo.
vii. Ninaagiza kuwa kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi kufanyike usafi wa nguvu katika maeneo yote ya majengo ya Taasisi zinazotoa Elimu kuanzia Maandalizi hadi Vyuo vikuu kwa Unguja na Pemba.

Pia natoa agizo la kila Jumamosi ya wiki katika maeneo ya dakhalia zote kufanya usafi maalum kutokana na kuonekana kuwa katika hali mbaya. Mwisho nawaagiza walimu wakuu wa skuli zote za Serikali na za Binafsi zipange ratiba zao na pia nawataka Maafisa Elimu kusimamia zoezi hili.
Nawashukuru wananchi wote na wadau wa elimu kwa mashirikiano wanayoyatoa katika kuendeleza juhudi za elimu nchini.
‘Elimu Bora kwa Maendeleo ya Taifa’
Naomba kuwasilisha.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.