Habari za Punde

CCM kesho kuzindua Kampeni uchaguzi mdogo wa Jimbo la Pandani

   NA IS-HAKA OMAR,PEMBA.

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Zanzibar kesho Machi 14,2021 kinatarajia kuzindua kampeni zake za Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Pandani Wilaya ya Wete  Mkoa wa Kaskazini Pemba.

Kampeni hiyo ya uchaguzi mdogo inazinduliwa kutokana na kufariki kwa aliyekuwa Mwakilishi wa Jimbo hilo kwa tiketi ya Chama Cha ACT-Wazalendo Marehemu Abubakar Khamis Bakar Januari 28,mwaka huu.

Akitoa taarifa juu ya uzinduzi huo Katibu wa Kamati Maalum ya NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Catherine Peter Nao, amefafanua kuwa Mgeni rasmi ktk hafla hiyo anatarajiwa kuwa Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dk.Abdulla Juma Saadalla(Mabodi).

Catherine, alisema kuwa CCM tayari imekamilisha maandalizi yote ya kuanza mikutano ya kampeni zake kwa lengo la kutoa muelekeo,mipango na sera imara za CCM katika Utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2021 ndani ya Jimbo hilo endapo Wananchi watakipa ridhaa Chama Cha Cha Mapinduzi kuongoza nafasi ya uwakilishi ndani ya Jimbo hilo.

Alisema Chama kimejipanga vizuri kuhakikisha kinashinda na kutwaa kiti hicho cha Uwakilishi kutokana na Utekelezaji mzuri wa Ilani ya kwa Wananchi ambao kimeweza kuwafikishia maendeleo endelevu yanayotokana na usimamizi mzuri wa sera zake kwa vitendo.

"Ndugu Wananchi wa Kisiwa Cha Pemba hasa Wana CCM na Wananchi nyote kwa ujumla wa Jimbo la Pandani na maeneo jirani tunakuombeni we muelekeze macho na masikio yenu katika Uchaguzi huu, ambao ni muhimu katika maendeleo ya maisha yenu hivyo chagueni mgombea anauetokana na Chama chenye historia ya kushughulikia maendeleo ya watu, nyinyi ni wadau muhimu katika kuamua hatma ya maisha ya watoto,vijana,wazee na wanawake pamoja na makundi mengine katika jamii.",alisema Catherine.

Akitoa ratiba ya mikutano ya Chama Cha Mapinduzi kwa upande wa CCM ndani ya Jimbo hilo zitakazoanza kwa kuzinduliwa katika Uwanja wa Pandani Tarehe 14/03/2021,Uwanja wa Shenge Juu 17/03/2021,Mzambarau Takao 20/03/2021,Pembeni 21/03/2021,Mlindo na Mjanaza 23/03/2021,Maziwani 24/03/2021,Pandani 25/03/2031 na kufunga itakuwa Januari 26,2021 ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya CCM Taifa ambaye pia ni Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mhe. Hemed Suleiman Abdallah.

Katika Maelezo yake  Catherine, alisema CCM imejipanga kufanya kampeni za kisitaarabu katika mikutano yake yote na kuwasisitiza wanachama,wafuasi na makada wa CCM kuhakikisha wanaepuka kufanya vitendo vinavyoashiria vurugu,machafuko na fujo za uvunjifu wa Amani.

Katibu huyo wa NEC,Idara ya Itikadi na Uenezi amevitaka Vyombo vya Ulinzi na Usalama katika Mkoa wa Kaskazini Pemba, kuhakikisha wanasimamia vizuri Ulinzi na Usalama wa Wananchi kwa kudhibiti vitendo vyote vya vurugu zinazolenga kuharibu kampeni za Uchaguzi huo.

Mgombea wa Kiti cha Uwakilishi kwa tiketi ya CCM katika Uchaguzi huo Ndugu. Mohamed Juma Ali atakabidhiwa vitendea kazi vyake ambavyo ni Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025,Katiba ya CCM ya mwaka 1977 toleo la mwaka 2017, muongozo wa uchaguzi pamoja na nyaraka nyingne zitakazomwezesha kufanya kazi kwa ufanisi mkubwa.

Pamoja na hayo alisema Wasanii mbalimbali wakubwa wa mitindo ya Kizazi kipya,Vikundi vya Taarab vinavyotikiaa mwambao wa pwani,ngoma za asili na Wasanii wakubwa wa maigizo kutoka visiwani na Tanzania bara watatoa burudani katika mikutano mbalimbali ya kampeni za Uchaguzi huo unaotarajiwa kufanyika mwaka  Machi 28,mwaka huu.


No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.