Habari za Punde

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe.Dk. Hussein Ali Mwinyi Amesaini Vitabu Vya Maombolezi Zanzibar.

 
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi leo amesaini vitabu vya maombolezo ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Marehemu Dk. John Pombe Magufuli na kueleza kwamba amepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambaye alikuwa kipenzi cha watu.

Rais Dk. Mwinyi kwa nyakati tofauti alitia saini vitabu hivyo ambapo alianzia katika Ofisi Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM),Zanzibar iliopo Kisiwandui Jijini Zanzibar na kusaini kitabu cha maombolezo.

Akiwa katika Ofisi hizo za CCM Zanzibar, Rais Dk. Mwinyi aliwakaribisha wale wote walioguswa na msiba huo kwenda kusaini kitabu hicho cha maombolezo hapo katika Ofisi Kuu ya CCM, iliopo Kisiwandui Jijini Zanzibar.

Rais Dk. Hussein Mwinyi alieleza kwamba amepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Dk. John Pombe Magufuli na kumuombea kwa Mwenyezi Mungu kuilaza roho ya marehemu mahapa pema peponi.

“Nimepokea kwa masikitiko makubwa msiba wa Mwenyekiti wetu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Marehemu Dk. John Pombe Magufuli. MwenyeziMungu ailaze roho yake mahala pema peponi, Amin”,alisema Dk. Mwinyi.

Rais Dk. Mwinyi pia, alimuelezea Marehemu Dk. John Pombe Magufuli kwamba alikuwa kipenzi cha watu huku akitumia fursa hiyo kuwashukuru wananchi wa Zanzibar kwa kujitokeza  kwa wingi hapo jana (Machi 23.2021) katika kuuaga mwili wa Marehemu Dk. John Pombe Magufuli aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Sambamba na hayo, Rais Dk. Mwinyi aliwaeleza wananchi wa Zanzibar kwamba waridhike na wale wachache ambao watapata fursa ya kwenda kuuzika mwili wa mpendwa wao Marehemu Dk. John Magufuli kijijini kwao Chato hapo Ijumaa (Machi 26) ambao watafanya hivyo kwa niaba yao.

Aliongeza kwamba anafahamu kuwa wananchi wote wa Zanzibar wangependelea kushiriki kikamilifu katika mazishi hayo ya mpendwa wao huko Chato lakini kutokana na hali na mazingira yaliopo waridhike na uwakilishi uliopo ambao umeweza kuwakilisha vyema tokea kuanza kuagwa mwili huo huko Jijini Dar es Salaam, Dodoma, Mwanza hadi kuelekea kule Chato.

Wakati huo huo, Rais Dk. Mwinyi alifika katika ukumbi wa Sheikh Idrisa Abdul Wakil ulioko Kikwajuni Jijini Zanzibar na kusaini kitabu cha maombolezo kufuatia kifo cha Marehemu Dk. John Pombe Magufuli kilichotokea Machi 17. 2021.

Rajab Mkasaba, Ikulu Zanzibar

Postal Address: 2422 Tel.:0777427449. Fax: 024 2231822 

 E-mail: rajabmkasaba@yahoo.co.uk

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.