Habari za Punde

Watendaji Wizara ya Habari Vijana, Utamaduni na Michezo watakiwa kutimiza wajibu wao

 Na Jamila Thabit WHVUM         03/03/2021

Wafanyakazi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo wametakiwa kutimiza wajibu wao kwa Serikali ili kuweza kuliletea maendeleo Taifa.

Akizungumza mara baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika Ofisi za Shirika la Utangazaji ZBC Redio Rahaleo, Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Fatma Hamad Rajab amesema wafanyakazi wamekuwa mstari mbele katika kudai haki zao lakini hawatimizi wajibu wao ipasavyo kwa Serikali kutokana na kukiuka taratibu na kanuni mbalimbali za kiutumishi ikiwemo kuingia na kutoka kazini kwa wakati.

Hivyo amewataka Wakuu wa vitengo kuwachukulia hatua za kiutumishi wafanyakazi wasiotimiza wajibu na majukumu yao ili kuchochea uwajibikaji katika kazi zao jambo ambalo litasaidia kuleta mageuzi ya kiutendaji na kuiletea nchi maendeleo ya kasi.

Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Khamis Abdallah Said amesema Serikali ina nia ya kuhakikisha inatoa huduma bora kwa Wananchi  na kutenda haki kwa wafanyakazi hivyo ni vyema kila mmoja kutekeleza wajibu wake ili kuweza kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.

Akizungumza kwa niaba ya Wakuu wa vitengo na wasimamizi wa Ofisi hizo Meneja wa Studio ya Muziki na Filamu Abeid Mfaume Faki ameahidi kuhakikisha wanawasimamia wafanyakazi waendane na kasi ya Serikali kwa kutimiza wajibu wao kwa mujibu wa taratibu na kanuni za kiutumishi.

Baadhi ya wafanyakazi wa Ofisi hizo wamesema ziara hiyo imewapa muamko na ari ya kuhakikisha wanatimiza wajibu wao ipasavyo katika majukumu yao ili kuleta maendeleo Nchini. 

Hata hivyo wamewapongeza Viongozi wa Wizara hiyo kwa kufanya ziara ambayo imetoa taswira njema ya namna ambavyo Serikali ya awamu ya nane ina azma ya kuhakikisha wafanyakazi wanaijenga Zanzibar yenye uchumi imara Kwa kuhakikisha wanawajibika na kufanya kazi zao kwa weledi, kwa maslahi ya Taifa.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.