Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Alhaj Dk. Hussein Ali Mwinyi.
Ni
wajibu wetu kumshukuru Mola wetu Mtukufu; SubhanahuWataala kwa kuturuzuku neema
ya uhai tukaweza kuifikia siku hii ya leo ambapo Waislamu na Wananchi wote wa
Zanzibar na Tanzania kwa ujumla tunaungana na Waislamu wenzetu duniani kote
katika kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mwaka huu wa 2021 Miladia,
sawa na mwaka 1442 Hijria.
Tunamshukuru
Mwenyezi Mungu(SWT) kwa kuturuzuku
hidaya ya uzima hadi tukaweza kuukaribsha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa mara
nyengine, kwani katika kipindi kama hiki mwaka jana, tulikuwa na Waislamu
wenzetu ambao Mwenyezi Mungu (SWT) amewakhitari na wameshatangulia mbele ya
haki. Tunamuomba Mwenyezi Mungu (SWT) awasamehe makosa yao na awape malazi
mema. Kadhalika, na sisi tulio hai atujaalie khatma njema na umri wenye faida.
Amiin!
Katika kuupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani,
tuweke azma na nia ya kuitekeleza ibada hii ya Saumu inayotukabili kwa imani na
yakini kwani ni wajibu wetu kufunga kama ilivyokuwa kwa wale waliotangulia
kabla yetu kama Mwenyezi Mungu (SWT) alivyotuamrisha katika Aya ya 183 ya Surat
Al – Baqarah yenye tafsiri isemayo:
“Enyi mlioamini! mmefaradhishiwa
kufunga (Saumu) kama walivyofaradhishiwa waliokuwa kabla yenu ili mpate kumcha Mungu”
Kwa
hakika, ibada ya Saumu ambayo imetukabili ina mchango mkubwa katika kuimarisha uchamungu,
jambo ambalo ni jema na litatupa manufaa hapa Duniani na kesho Akhera. Kwa
hivyo, tuukaribishe MweziMtukufu wa
Ramadhani kwa furaha na matumaini, na tujiandae kunufaika kutokana na neema na
fadhila mbalimbali zilizo katika kipindi chote cha Mwezi huu tunaoukaribisha. Tuhimizane
kutekeleza ibada za Faradhi vilevilenatukithirishe kufanya ibada za Sunna ili kupata radhi za
Mola wetu Mlezi.
Ndugu Wananchi,
Miongoni mwa ibada ambayo imesisitizwa
kuifanya kwa wingi ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni kusoma Qurani, kwani
mwezi huu ndio ulioteremshwa Kitabu Kitukufu cha Qurani ambacho ni mwongozo
wetu. Mwenyezi Mungu ametubainishia
katika Aya ya 185 ya Surat Al-Baqarah kwa tafsiri isemayo;
“Mwezi wa Ramadhani ambao imeteremshwa ndani yakehii Qurani ili iwe uongofu
kwa watu,na hoja zilizo wazi za uongofu na upambanuzi (baina ya haki na
batili)”. Hadi mwisho wa aya.
Kwa hivyo, ni wajibu wetu kuutumia Mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa kuisoma sana Qurani kwani kufanya hivyo kuna fadhila kubwa mbele ya Mwenyezi Mungu (SWT). Tujitahidi kuendeleza darsa Misikitini, kufanya mihadhara mbalimbali ya kutoa tafsiri ya Qurani ili usomaji wetu uzidi kuleta faida kwa kuyafahamu mafundisho yake. Kwa kufanya hivyo, tutaweza kunufaika zaidi na kupata upambanuzi utakaotuwezesha kuyaelekea zaidi mambo ya haki na kujiepusha na batili ili tupate radhi za Mwenyezi Mungu (SWT).
Ndugu Wananchi,
Katika kutafuta
fadhila za Mwezi Mtukufu wa Ramadhani tumehimizwa kujitahidi sana kutekeleza
ibada ya sala zote za Faradhi na sala za Sunna, kuomba dua,kusoma nyiradi mbali
mbali, kufanya itikafu, na kutekeleza Sunna
nyengine zinazoambatana na Mwezi wa Ramadhani.
Ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani unapatikana usiku wenye heshima kubwa wa Laylatul Qadir. Tunaelezwa kuwa, ibada ya usiku huo imebarikiwa kuliko ibada za miezi elfu moja na kwa hekimaza Mola wetu, hakutubainishia kuwa usiku huo ni wa tarehe ipi. Hivyo, tuna wajibu wa kutafuta usiku huo kwa kufanya ibada nyingi hususan katika kumi la mwisho.
Katika kuonesha uzito wa kisimamo cha usiku kwa ajili ya kufanya ibada, Mtume wetu Muhammad (SAW) katika moja ya hadithi zake amesema kwamba.
“Mwenye
kusimama usiku wa Ramadhani kwa kufanya ibada hali ya kuwa na Imani na kutarajia
thawabu, amesamehewa mtu huyo, yote yaliyotangulia miongoni mwa makosa yake”(Bukharina Muslim).
Kwa hivyo, tumuombe Mola wetu atuwezeshe kutekeleza ibada
hiyo katika Mwezi Mtukufu wa Ramdahni ili tuweze kunufaika na fadhila za ibada
za usiku ikiwemo kusamehewa madhambi
yetu yaliyopita kwani kwa hakika mwanadamu sio mkamilifu ila Mola pekee Subhanahu
Wataala.
Ndugu wananchi,
Jambo jengine
tunalohimizwa kulitekeleza zaidi ndani ya Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ni kutoa
sadaka hasa kwa watu wenye mahitaji, Mayatima, Wazee, Masikini na Mafakiri. Tunaelezwa kuwa ibada hii ina malipo makubwa
mbele ya Mwenyezi Mungu (SWT) na inaongeza baraka, mapenzi na kuhuwisha
mahusiano mema ndani ya jamii.
Mashekhe wetu wanatufunza kuwa katika mwezi Mtukufu wa Ramadhani Bwana Mtume (SAW) kutoa kwake sadaka, kuliongezeka kuliko miezi mingine. Kwa vile yeye ni Kiongozi wetu, tuna wajibu wa kumfuata na kuitekeleza Sunna hii kama walivyoitekeleza masahaba zake na wote waliofuata mwendo wake mwema na kufanikiwa kutokana na mafundisho yake. Tumuombe Mwenyezi Mungu (SWT) atupe nguvu na uwezo wa kuyatekeleza mambo haya ya kheri.
Ndugu wananchi,
Nilipokutana
na wafanyabiashara wakubwa wanaoagiza chakulatarehe 04 Machi, 2021 niliwataka,
washirikiane na Serikali kufanya maandalizi mazuri katika kuhakikisha kwamba,
bidhaa zote hasa za chakula muhimu kwa wananchi wa Zanzibar ziwe zinapatikana
kwa kipindi cha Mwezi Mtukufu wa Ramadhani na baada ya hapo, kwa wingi na ubora
stahiki, ili bei za bidhaa hizo zisiongezeke kama inavyotokea katika nyakati
hizo. Tulikubaliana mambo kadhaa ambayo sasa tunaendelea kuyatekeleza, ikiwemo
kutoa kipaumbele katika utoaji ruhusa wa kushusha mizigo kwa meli zinazoleta bidhaa za chakula.
Inafurahisha kuona kwamba licha ya kuwepo kwa changamoto za usafirishaji na upatiakanaji wa bidhaa mbalimbali, shughuli za biashara na upatikanaji wa chakula hapa nchini zinaendelea vizuri, tunapoukaribisha Mwezi wa Ramadhani ikiwa bidhaa zote muhimu zinapatikana.
Kadhalika, taarifa ya Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo inatoa matumaini ya kuwepo kwa chakula cha kutosha miongoni mwa mazao ya chakula hasa muhogo na ndizi, mazao ambayo hutumiwa na wananchi wengi kwa futari katika Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
Mtakumbuka kwamba tarehe 02 Aprili, 2021niliposalimiana na wananchi baada ya Sala ya Ijumaa katika Msikiti wa Amani,niliwasihi wafanyabiashara waendelee kutoa huduma kwa wananchi kwa misingi ya uadilifu na huruma pamoja na kuzingatia sheria. Kwa pamoja, tuwafikirie wenzetu wenye kipato cha chini hasa katika kipindi hiki ambacho mahitaji ya familia yanaongezeka.Kwa msingi huo huo, wafanyabishara wa bidhaa za nguo wazingatie uwezo wa wananchi, kwani kuwakatia nguo watoto wetu katika kipindi hiki kwa ajili ya Sikukuu ni sehemu ya utamaduni wa wananchi wote wa Zanzibar.
Serikali tayari imeshatoa bei elekezi za bidhaa muhimu za chakula. Kwa hivyo, itachukua hatua kali kwa mfanyabishara yoyote atakaebainika kupandisha bei za bidhaa au huduma kwa utashi au tamaa tu na bila ya kuwepo na sababu ya msingi ya kufanya hivyo.
Ndugu wananchi,
Tunaupokea Mwezi Mtukufu wa Ramadhani wakati nchi yetu
inaingia katika msimu wa mvua za Masika.Natumia fursa hii kukuhimizeni wananchi
pamoja na viongozi na watumishi wa Manispaa zote juu ya umuhimu wa kuzingatia
usafi katika miji yetu na hasa katika masoko na maeneo yanayohusika na uuzaji
wa vyakula ili kujiepusha na maradhi ya mripuko. Tuendelee kusafisha misingi ya
maji na
njia za maji ili kujikinga na mafuriko. Ni vyema sote tuzingatie
maelekezo ya wataalamu wa afya juu ya namna ya kuimarisha usafi ili kujikinga
na mirupuko ya maradhi mbalimbali.
Ndugu wananchi,
Mwezi
Mtukufu wa Ramadhani ni chuo cha kujifunza tabia njema, tustahamiliane na
tuvumiliane, tusaidiane na tuendeleze umoja na upendo miongonimwetu. Aidha, natumia fursa hii kuwakumbusha wananchi wenye dharura maalum na walewasiokuwa
Waislamu waendeleze utamaduni wa kujizuia kula hadharani, kutokuvaa nguo
zisizoendana na maadili yetu, na tuepuke matendo yatakayo wakwaza Waislamu
wenye kutekeleza ibada ya funga.
Ndugu
wananchi,
Nakamilisha risala yangu ya kuukaribisha Mwezi Mtukufu wa
Ramadhani kwa kuwahimiza viongozi wa Mamlaka ya Usafiri na Usalama Barabarani
pamoja na Jeshi la Polisi kuhakikisha
wanasimamia ipasavyo sheria za usalama barabarani wakati wote, na kuongeza
nguvu zaidi katika kipindi hiki ambacho
harakati na mahitaji ya usafiri huongezeka. Wawachukulie hatua kali za
kisheria madereva watakaojaribu kuvunja sheria
za usalama barabarani kwa kwenda mwendo wa kasi na wale wenye tabia ya kuwasumbua wananchi
kwa kuwashusha bila ya kuwafikisha mwisho wa vituo vilivyopangwa na Serikali.
Kadhalika,
nawahimiza viongozi wa Mamlaka ya Maji Zanzibar (ZAWA) kuhakikisha huduma ya
maji zinawafikia wananchi hasa katika
maeneo ambayo huduma hio haipatikani kwa ukamilifu. Masheha wa shehia ambazo
zina matatizo ya maji wawasiliane na ZAWA ili kuhakikisha hatua zinachukuliwa
zikiwemo kuwapelekea wananchi magari ya maji kwa lengo la kuondokana na
usumbufu wa kupatikana huduma hio muhimu.
Nakutakieni
nyote kila la kheri na namuomba Mwenyezi Mungu (SWT) atuwezeshe kuufunga mwezi
wa Ramadhani kwa salama. Tumuombe Mola wetu azikubali ibada zetu zote
tutakazozifanya katika mwezi huo na katika maisha yetu yote.Aameen!
Wassalaamu Aleykum Wa
RahmatuLlahi wa Barakaatuh.
No comments:
Post a Comment