Habari za Punde

Uongozi wa UWT Yatoa Elimu ya Kuwajengea Uwezo Wajumbe wa Kamati za Utekelezazi wa Ngazi Mbalimbali za UWT Mkoani.

MWENYEKITI wa CCM Mkoa wa Magharib Unguja, Ndg. Mohamed Rajab, akifungua mafunzo ya kuwajengea uwezo Wajumbe wa Kamati za Utekelezaji za ngazi mbalimbali za UWT Mkoa wa Magharibi Kichama yaliyofanyika katika ukumbi wa Skuli ya Shaah Kwa Mchina Mwanzo Zanzibar.
MWAKILISHI wa Viti Maalum Mkoa wa Magharib Fatma Ramadhan Mandoba, akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo Akina Mama wa Kamati tekelezaji za UWT za Mkoa huo.
MBUNGE wa Viti Maalum Mkoa wa Magharib Amina Idd Mabrouk, akizungumza katika mafunzo ya kuwajengea uwezo Akina Mama wa Kamati tekelezaji za UWT za Mkoa huo.
BAADHI ya Wajumbe wa ngazi mbalimbali za Kamati tekelezaji za UWT Mkoa wa Magharibi walioshiriki mafunzo ya siku moja ya kuwajengea uwezo wa kupambana na vitendo vya udhalilishaji.

Na.Is-haka Omar -Zanzibar.

WAZAZI na Walezi visiwani Zanzibar wametakiwa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia.

 

Rai hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Magharibi Unguja Ndugu Mohamed Rajab, katika ufunguzi wa semina elekezi ya kuwajengea uwezo wajumbe wa kamati za utekelezaji ngazi  mbalimbali za UWT Mkoani humo  yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Skuli ya Sekondari ya Shaah kilichopo kwa Mchina Mwanzo.

 

Alisema vitendo vya udhalilishaji vimeendelea kuongezeka kila kukicha katika jamii jambo linalotakiwa kudhibitiwa kwa nguvu zote.

 

Alisema bado kuna kazi ya ziada ya kuthibiti vitendo hivyo inayotakiwa kufanywa na wazazi ambao ndio waliokaribu na watoto.

 

Amesema vitendo hivyo vikiachiwa vikaendelea kushamili katika jamii na nchi itakosa nguvu kazi ya vijana ambao ni imara sambamba  na ukosema wa viongozi bora.

 

"Wazazi chukueni hatua kali za kulinda watoto wetu ambao wanaharibiwa kila kosa na nyinyi hamfuatilii wala kuchukua hatua sitahiki za kuwafikisha mahakamani wahusika wa matukio hayo" .Alisema Mwenyekiti huyo wakati akifungua mkutano huo.

 

Sambamba na hayo aliongeza kwamba jamii inatakiwa kuchukua za kuhakikisha kila mtoto anapata ulinzi wa kutosha ili  kuwaepusha na janga la udhalilishwaji.

 

Katika maelezo yake Mwenyekiti huyo Mohamed ,alifafanua kwamba vitendo hivyo hawafanyiwi watoto pekee bali hata kwa wanawake wanadhalilishwa kwa kufanyiwa vitendo vya ubakaji na kutelekezewa watoto jambo linalochangia kuongezeka kwa udhalilishaji nchini.

 

Alitumia nafasi hiyo kuwashauri wanaume nchini wale wenye familia kubadilika kitabia kwa kuhakikisha wanalinda kwa nguvu zote familia zao na zilizowazunguka katika jamii zao.

 

"Wanaume tubadikikeni tuhuma za vitendo vya udhalilishaji zinatukabili kwa sababu wapo baadhi yetu hawatosheki na wake zao na badala yake wanaingia mitaani na kuwadhalilisha watoto wadogo tena wengine wanawadhalilisha mpaka watoto wao wa kuwazaa." Alison nasaha hizo Mwenyekiti huyo.

 

Alisema vyombo vya ulinzi na usalama na mahkama nchini waendelee kutenda haki kwa kuhakikisha watuhumiwa wote wanaokutwa na hatia ya kutenda uhalifu huo wanachukuliwa hatua kali za kisheria.

 

Aliwasihi wananchi kuunga mkono juhudi za kudhibiti uhalifu huo kwa kuhakikisha wanatoa ushahidi pindi wanapotakiwa kufanya hivyo kwa lengo la kuhakikisha watu wanaojihusisha na vitendo hivyo wapata adhabu sitahiki kwa mujibu wa sheria.

 

Akizungumza katika semina hiyo Mwakilishi wa Viti Maalum CCM Mkoa wa Magharibi Fatma Ramachan Mandola, amesema tatizo la udhalilishaji wa kijinsia nchini linatakiwa kutatuliwa kwa ushirikiano baina ya jamii na wananchi kwa ujumla.

 

Alisema kuwa vitendo hivyo vinaongezeka kutokana na uwepo wa tabia ya mihali wa watu kuoneana aibu na huruma kuchukua hatua dhidi ya mtu wanayemfahamu.

 

"Akina mama na wanaharakati msikate tamaa tuendeleze mapambano kwa pamoja ipo siku tabia hizi zisizofaa zitaondoka kabisa katika jamii yetu".alisema Fatma.

 

Pamoja na hayo alimshukru Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapnduzi Dk. Hussein Ali Mwinyi, kwa kuunda mahkama maalum ya shughulikia kesi za udhalilishaji ambayo hivi sasa baadhi ya kesi zimeanza kusikilizwa na kutolewa hukumu.

 

Naye Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa huo Amina Idd Mabrouk, alisema lengo la mafunzo hayo ni kuwajengea uwezo viongozi hao wa UWT ambao ni wajumbe wa kamati za utekelezaji ili nao wakafikishe elimu hiyo kwa jamii inayowazunguka.

 

Alieleza kwamba vitendo vya udhalilishaji vina madhara makubwa katika jamii hivyo havitakiwi kufumbiwa macho bali kila mtu achukue hatua kwa kuhakikisha anachukia kwa vitendo.

 

Alisema licha ya serikali na mashirika mbalimbali ya Kimataifa kuchukua hatua za kudhibiti vitendo hivyo nchini bado vinaendelea kutokana na jamii yenyewe kutotoa ushirikiano unaostahiki kwa vyombo vya kisheria hasa kesi zinapofika mahkamani.

 

Alisema watoto wengi wameharibiwa ndoto zao hasa wanaosoma skull mbalimbali kutokana na kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji wa kijinsia vilivyosababisha kupata msongo wa mawazo.

 

" Vyombo vya habari vinaripoti matukio hayo lakini hayapungui kila siku yanaongezeka tena kwa kasi, hivyo sisi tuliopewa mafunzo haya tukawaelimishe akina mama wenzetu uko mitaani kwetu ili nao waongeze kasi ya ulinzi wa watoto.",alisema Amina.

 

Akifunga mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo Wanawake, Mwenyekiti wa UWT wa Mkoa huo Zainab Ali Maulid, alisema sheria nyingi zimetungwa za kudhibiti matukio ya udhalilishaji lakini bado yanaendelea hivyo Serikali inatakiwa kutafuta njia mbadala ya kudhibi matukio hayo.

 

Akitoa mada za masuala ya udhalilishaji mkufunzi alieleza kwamba takwimu za vitendo hivyo zinaonyesha kwamba jumla ya matukio 155 ya ukatili na udhalilishaji wa kijinsia yameripotiwa Zanzibar mwezi wa Septemba 2020.

 

Katika takwimu hizo wanawake 14 (asilimia 12.2) na watoto ni 101sawa na asilimia 87.8, miongoni mwao wasichana ni 82(asilimia 81.2) na wavulana ni 19 (18.8).

 

Mafunzo hayo ya siku moja yameandaliwa na Mwakilishi wa Viti Maalum Fatma Ramadhan Mohamed Mandoba kwa kushirikiana na Mbunge wa Viti Maalum wa Mkoa huo Amina Idd Mabrouk.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.