Habari za Punde

Miradi Yote Iliyopatwa na Mafuriko Pembezoni Mwa Maziwa ni Lazima Isanifiwe Dkt.Gwamaka.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka akitoa maelekezo kwa Kaimu Mkuu wa Chuo cha Wakala wa uvuvi Bw. Bakari Mwichande katika mradi wa soko la Kibilizi uliokumbwa na mafuriko kwenye Manispaa ya Kigoma Ujiji.

Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka kutoka kulia akiwa na Kaimu Mkuu wa Chuo cha Wakala wa uvuvi Bw. Bakari Mwichande (katikati) pamoja na Meneja wa NEMC Kanda ya Magharibi Bernad Dotto wakiwa eneo la Soko la Kibalizi lililokumbwa na mafuriko.

 

Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira NEMC Dkt. Samuel Gwamaka amesema ni lazima miradi iliyopembezoni mwa maziwa isanifiwe ili kuepuka madhara yanayotokana mafuriko kama ilivyotokea kwenye mradi wa soko la Kibilizi uliopo Halmashauri ya mji wa Kigoma.

Ameyasema hayo wakati wa ziara ya kikazi kwenye Halmashauri ya Mji wa Kigoma kwenye Soko la Kibilizi lililokumbwa na mafuriko.

"Miradi yote iliyopata mafuriko pembezoni mwa maziwa iwe ya Serikali au binafsi ni lazima isanifiwe ndani ya miezi sita ili kujua huo mradi unaboreshwa au unavunjwa kuepuka athari za uharibifu wa mazingira katika mradi kama huu wa Kibilizi."

Aidha Dkt. Gwamaka amesema athari za mafuriko kwenye miradi iliyo pembezoni mwa maziwa inasababishwa na uzembe wa kutokuzingatia Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM).

"Tathmini ya Athari kwa Mazingira ni njia pekee ya kuepuka hasara kwenye miradi kama hii, na huu ni uzembe kwa sababu mipaka ya asili ya ziwa haikuzingatiwa kabla ya ujenzi wa mradi huu".

Dkt. Gwamaka alimalizia kwa kusema kwamba miradi iliyopatwa na mafuriko inahatarisha afya za watu na viumbe wa majini, akatolea mfano wa soko la Kibilizi kuwa vyoo vilivyokuwa vikitumika wakati shughuli za soko zikiendelea vimejaa maji yanayoenda ziwani, hali hii itasababisha magonjwa ya milipuko kama kipindupindu au magonjwa ya kuhara hivyo ni lazima tahadhari zichukuliwe kwa Wananchi wanaotumia maji yaliyokaribu na mradi huo.

Naye Kaimu Mkuu wa Chuo cha Wakala wa Elimu na Mafunzo ya uvuvi Kigoma Bw. Bakari Mwichande alisema mafuriko yamewaathiri kwa kiwango kikubwa hali iliyowalazimu kuhama chuoni hapo na kwenda kupanga kwenye jengo lingine kwa sababu ya kujaa maji kwenye vyumba vya madarasa chuoni hapo.

Ameongeza kuwa mafuriko yamesababisha kuharibika kwa miundombinu chuoni hapo kama vile majengo ya maktaba na vyumba vya madarasa.

Odemba Kornel, Mhandisi rasilimali za maji kwenye bonde la Ziwa Tanganyika alisema kina cha maji kimeongezeka kutoka kwenye mipaka ya awali mpaka kufikia eneo ambalo yapo makazi ya watu na shughuli zao kutokana na mvua zilizonyesha, hivyo alitoa tahadharikwa wananchi kufanya kutokufanya shughuli yoyote au kuanzisha makazi ndani ya mita sitini kutoka mwambao wa Ziwa Tanganyika.

No comments:

Post a Comment

ZanziNews Copyright © 2014

Theme images by Bim. Powered by Blogger.